1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahamiaji wahamishwa kambi ya Idomeni

Yusra Buwayhid24 Mei 2016

Polisi nchini Ugiriki wameanza operesheni ya kuwahamisha maelfu ya wahamiaji kutoka kambi ya muda ya Idomeni . Wakati huo huo wahamiaji wengine 2,000, waokolewa bahari ya Mediterenia.

Griechenland Behörden beginnen mit Räumung des Flüchtlingslagers in Idomeni
Picha: Reuters/Y. Kolesidis

Msemajji mkuu wa serikali ya Ugiriki kuhusu mgogoro wa wahamiaji, Giorgos Kyritsis, amesema polisi hawatotumia nguvu na kwamba operesheni hiyo inategemea kuchukuwa takriban siku 10 hadi kukamilika.

Kwa mujibu wa polisi mabasi sita ya mwanzo yaliyobeba watu 340 yaliondoka kambi ya Idomeni masaa machache yaliyopita wakati ilipoanza operesheni hiyo, yakielekea kambi mpya iliyopo mji wa kaskazini mwa Ugiriki wa Thessaloniki. Hakuna taarifa zozote za vurugu hadi sasa.

Idomeni ni kambi ya muda isiyokuwa na uwezo wa kukidhi majitaji ya wahamiaji, wengi wao wakiishi katika mahema na wakati wa mvua kubwa eneo hilo linajaa matope na uchafu. Polisi pamoja na mamlaka za serikali wanasema, wahamiaji hawo sasa watahamishiwa katika kambi rasmi.

Awali, eneo hilo lilikuwa ni njia kuu inayotumiwa na wahamiaji pamoja na wakimbizi kuingilia nchi za Ulaya kaskazini. Lkaini sasa kambi ya Idomeni inakisiwa kuwa na wahamiaji 8,400 - ikiwa ni pamoja na watoto- wengi wao kutoka Syria, Afghanistan na Iraq.

Wahamiaji UgirikiPicha: picture-alliance/AP Photo/S. Palacios

Lakini pale Macedonia ilipoamua kufunga mipaka yake mwezi Machi, kambi hiyo ilikuwa na zaidi ya watu 14,000. Hata hivyo polepole idadi ilipungua baada ya wahamiaji kutanabahi, kuwa hakuna dalili ya kufunguliwa mpaka wa Macedonia na kukubali njia mbadala za hifadhi kutoka kwa mamlaka husika.

Zaidi ya wahamiaji na wakimbizi 54,000 wamekwama nchini Ugiriki baada ya nchi za Balkan na Ulaya kufunga mipaka yake, ili kuzuwia wimbi kubwa la watu wanaokimbia vita na umasikini nchi wanazotoka, kuingia ndani ya mipaka yao.

Wahamiaji 2,000 waokolewa Mediterenia

Wakati hayo yakiendelea,walinzi wa pwani wa Italia wamewaokoa takriban wahamiaji 2,000 katika bahari ya Mediterenia nje ya mwambao wa Libya, wanaotokea nchi za Afrika wakijaribu kupenya barani Ulaya.

Uwokozi huwo ulifanyika kupitia operesheni 15 tofauti. Boti mbili za uwokozi za Italia zilibebea zaidi ya wahamiaji 500, huku boti nyengine mbili za madaktari wasio na mipaka zilibebea wahamiaji wengine 788. Halikadhalika boti za jeshi la majini la Ireland pamoja na boti za mizigo zilizokuwa zikipita njia, zilisaidia katika operesheni hiyo ya uwokozi.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, katika mwaka huu pekee zaidi ya wahamiaji na wakimbizi 190,000 wamejaribu kuingia barani Ulaya kupitia safari hatari za majini. Huku 1,359 wakiwa wamefariki njiani. Wanaofanikiwa wanaingia barani humo kupitia nchi kama Italia, Ugiriki, Cyprus pamoja na Uhispania.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/ape/rtre

Mhariri:Yusuf Saumu