Wahamiaji wanyanyaswa nchini Libya
5 Julai 2016Katika ripoti hiyo iliyopewa kichwa "Libya imejaa ukatili" Amnesty international ilichukua ushahidi wa wahamiaji 90, wakiwemo wanawake 15, waliohojiwa katika vituo vya mapokezi huko Italia na Sicily baada ya kutoroka Libya miezi michache iliyopita. Kundi hilo linasema dhuluma za kingono zimekuwa jambo la kawaida kiasi cha kwamba baadhi ya wanawake hutumia vidonge vya kuzuia uja uzito kabla hawajaanza safari ya kuvuka bahari.
Afisa wa shirika hilo la Amnesty Magdalena Mughrabi amesema wakimbizi na wahamiaji wameelezea jinsi watekaji nyara na makundi ya uhalifu walivyowadhulumu walipokuwa nchini Libya.
Libya ni makao ya wakimbizi na wahamiaji 250,000. Shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia masuala ya wakimbizi linakadiria tangu Aprili 19, 2015 takriban watu 5000 wamefariki wakijaribu kuvuka bahari ya Mediterania kutoka Libya kuelekea Ulaya.
Amnesty imeitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua na kukabiliana na chanzo kikuu cha uhamiaji na kuongeza idadi ya watu wanaopewa hifadhi ulaya ama wanaopewa visa za kibinadam.
Libya ilitumbukia kwenye mzozo kufuatia kuondolewa mamlakani kwa Moamar Gadhafi aliyetawala kwa zaidi ya miaka 40 kabla uasi wa mwaka 2011 uliopelekea mapigano ya ndani kwa ndani.
Licha ya mkataba wa kisiasa uliosimamiwa na umoja wa mataifa mwezi Disemba, nchi hiyo ingali imegawanyika kisiasa kati ya pande dhaifu zinazoongozwa na makundi hasimu ya wapiganaji. Wahamiaji hao waliiambia Amnesty international kwamba wapo watu waliouwawa na watekaji nyara hao kutokana na kiu au njaa.
Ripoti hiyo inasema kwamba wengine walipigwa risasi ama kuuwawa kwa nguvu za umeme, na katika kisa kimoja mhamiaji mmoja mlemavu alitupwa jangwani na hao wasafarishaji watu haramu.
"Walikua hawana utu kabisa," alisema kijana mmoja mwenye umri wa miaka 20, kutoka Eritrea, aliyeingia Libya mwezi Oktoba. Wanawake hasa ndio walio katika hatari ya kubakwa na kudhulumiwa kingono.
"Simulizi zao zinaonyesha hali za kutisha wanazozikimbia nchini mwao wale wanaokuja ulaya," alisema Mughrabi.
Kubakwa kwa wanawake
Mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 22 ameliambia shirika hilo la Amnesty kuwa alibakwa zaidi ya mara moja wakati akiwa amezuiliwa katika eneo moja lililoko karibu na mji wa Ajdabiya, Libya mashariki. "Unapoelekezewa bunduki basi hauna namna," alieleza.
Mwanamke mwengine alieleza jinsi mhamiaji mmoja wa kike alivyobakwa na kundi la watekaji nyara hao baada ya kushindwa kulipa ada ya kusafirishwa.
Katika mojawapo ya visa vya kusikitisha zaidi mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 21 aliliambia shirika hilo kwamba alikuwa miongoni mwa kundi la wanawake 11 wa kikristo kutoka Eritrea, waliotekwa nyara na wanamgambo wa IS Julai mwaka 2015. Walizuiliwa katika eneo lililo chini ya ardhi kwa miezi tisa, wakalazimishwa kubadili dini na kuwa waislamu na kisha kutumiwa kama watumwa wa ngono.
Wakati huo huo inaripotiwa kwamba idadi ya wahamiaji waliowasili nchini Italia katika nusu ya kwanza ya mwaka huu ilikuwa sawia na miaka miwili iliyopita, imesema wizara ya mambo ya ndani ya Italia.
Wizara hiyo imesema kwamba jumla ya watu 70, 930 waliwasili nchini humo kati ya mwezi Januari na Juni hiyo ikiwa ni takriban idadi sawa na ile ya walioingia nchini humo mwaka 2015 ingawa idadi hiyo ilikuwa imezidi ya wale waliowasili mwaka 2014.
Mwandishi: Jacob Safari/AP/AFP
Mhariri:Iddi Ssessanga