1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahamiaji wasio halali watakabiliwa na hali ngumu zaidi sasa

3 Januari 2006

Wahamiaji wasio halali wanaotaka kuingia katika nchi za Ulaya sasa watakabiliwa na hali ngumu baada ya majeshi ya Morokko na Uhispania kukamilisha ujenzi wa kizuizi cha waya katika eneo lisilomilikiwa baina ya mpaka wa nchi hizi mbili.

maisha magumu yanayowakabili wakimbizi
maisha magumu yanayowakabili wakimbiziPicha: AP

Kwa miaka mingi sasa bara ulaya limekuwa gizani kuhusu hali halisi inayowakabili wahamiaji wasio halali hadi hivi majuzi wakati visa vya kuuwawa wahamiaji hao wasio halali vilipokithiri na kugonga vyombo vya habari ulimwenguni kote.

Idadi ya watu 14 hadi 16 wenye asili ya kiafrika waliuwawa kwa kupigwa risasi mwezi oktoba mwaka uliopita wakati walipojaribu kuiingia katika maeneo mawili ya Ceuta na melila huko nchini Uhispania ambayo Morroko inayadai kuwa ni maeneo yake.

Baada ya tukio hilo serikali ya Morokko ikaanzisha mpango wa kuwarudisha makwao wahamiaji wasio halali huku wahamiaji wengine wakinyimwa ruhusa ya kuingia nchini Morokko na hata wengine kuachwa wakiwa wamekwama jangwani bila ya chakula au maji.

Vitendo hivyo vilisababisha kuanzishwa kwa kampeni za kutetea haki za binadamu na kutokea wakati huo Moroko na Uhispania zimetia saini makubaliano ya kuwafukuza wahaniaji wasio halali kutoka nchi hizo.

Hadi kufikia sasa hali ya wakimbizi 50 walioomba hifadhi nchini Morokko bado haijulikani. Wakimbizi hao bado wako katika kambi ya wakimbizi ya Guelmim kusini mwa Morokko.

Morokko ilitia saini makubaliano ya kulinda haki za wakimbizi ya mwaka 1951 na hivyo basi inatarajiwa kuheshimu haki za wakimbizi.Mehdi Lahlou mtafiti wa maswala ya uhamiaji kutoka Moroko anasema kwamba hadi kufikia mwezi oktoba mwaka 2005 serikali ya Morokko imemsafirisha muhamijai asie wa halali mmoja tu kati takriban wahamiaji 3000 na hii ni kutokana na shinikizo kutoka kwa nchi za umoja wa ulaya na utawala wa Uhispania.

Anasema kabla ya kutokea vurumai ya kuingia katika miji ya Ceuta na Melilla, wakimbizi wa kiafrika walikuwa kamwe hawasumbuliwi na mtu yeyote seuze walinda usalama tena walikuwa wakiishi bila ya makaratasi yeyote ya utambulisho katika mji wa Rabat na wala hawakuwa na ugomvi au kutokuelewana na wenyeji.

Lakini ghafla wahamiaji hawa wanajikuta mashakani na hali kuwabadilikia kwani siku hizi wakikamatwa mara moja hupelekwa katika kambi ya kijeshi ya Bouyzakern karibu na mji wa Guelmim ulio katika sehemu iliyo na ukame mkubwa kusini mwa Morokko.

Huko wakimbizi hawa hufikwa na mashaka makubwa kwani maisha hugeuka na kuwa magumu zaidi kuanzia kwenye makaazi ambayo huwalazimu kuishi bila ya mahali pa kujisaidia na huko inawalazimu kuishi kwa taabu huku wakisubiri shirika la wakimbizi la umoja wa mataifa UNHCR kushughulikia maombi yao ya hifadhi.

Wengi wa wanaokabiliwa na shida hizi ni wakimbizi kutoka Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Ivory Coast, Liberia na Sierra Leonne.

Kati kati ya mwezi Novemba mwaka jana kundi la mashirika yasiyo ya kiserikali kutoka Morokko, Ubelgiji na Uhispania liliandika barua ya wazi kwa serikali husika pamoja na katibu mkuu wa umoja wa mataifa Koffi Annan juu ya shida zinazowakabili wakimbizi hawa.

Wanawake na watoto wanaendelea kuteseka kwa kupigwa,kudhalilishwa na kutumiwa vibaya na mara nyingine hata kuuwawa kwa sababu ya kutaka kutimiza ndoto ya kuwa na maisha mazuri ambayo hayapatikani katika nchi zao.

Ukimbizi husababishwa na vita, umasikini, udikteta na uongozi mbaya yote haya huwafanya raia wa nchi hizi kujazana kinyume cha sheria katika miji ya Paris, Madrid, Roma, Brussels; Rabat Algiers, Tunis, Tripoli na miji mingine mingi mikubwa duniani.

Suluhisho sio kuzihama nchi na kusongamana katika nchi za bara ulaya anasema mtafiti Lahlou.

Kwani maisha sio mazuri sana kwa wanaotafuta hifadhi ya ukimbizi kwa wengi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW