Wahamiaji watano wapigwa risasi Calais
2 Februari 2018Wanne kati ya wahamiaji hao wako mahututi na wengine 22 wamelazwa kutokana na majeraha waliyopata wakati wa mapigano hayo kwenye kambi ya Calais ambayo inawahifadhi mamia ya wahamiaji wengi wao kutoka Eritrea, Ethiopia na Afghanistan, ambao wana matumaini ya kudandia malori kwenda Uingereza.
Maafisa wamesema kuwa vijana wanne wa Eritrea wenye kati ya umri wa miaka 16 na 18 ambao walipigwa risasi kwenye shingo, kifua, tumbo na mgongoni, wako katika hali mbaya. Polisi inamtafuta mwanaume kutoka Afghanistan mwenye umri wa miaka 37, ambaye anatuhumiwa kwa kuwapiga risasi wahamiaji hao.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa, Gerard Collomb ambaye alizuru katika eneo la tukio amesema wahamiaji wengine wanauguza majeraha baada ya kuchomwa kisu. Waziri huyo amesema kiwango cha ghasia katika eneo hilo hazijawahi kushuhudiwa hapo kabla.
''Wakati tunaona idadi ya watu waliojeruhiwa kwa kupigwa risasi, wakiwemo wahamiaji wanne walioko mahututi, tunaweza kusema ghasia hizi hazijawahi kushuhudiwa kabla. Nimewaona polisi wakijitahidi hapo awali, lakini kama wasingekuwepo hapa jana usiku, hali ingekuwa mbaya zaidi, pengine wahamiaji wengi zaidi wangejeruhiwa,'' alisema Collomb.
Ghasia katika eneo hilo zimekuwa zikiongezeka tangu serikali ya Ufaransa ilipoivunja kambi kubwa ya wakimbizi ya muda iliyokuwa ikijulikana kama 'kambi ya msituni' na iliyokuwa ikiwahifadhi kiasi ya wahamiaji 6,000, mwaka 2016.
Ufaransa: Hatuwezi kuvumilia ghasia
Hata hivyo, Ufaransa imesema haiwezi kuzivumilia ghasia zinazoendelea. Polisi wawili pia walijeruhiwa katika mapigano hayo yaliyozuka miongoni mwa raia 100 wa Eritrea na kiasi ya raia 30 wa Afghanistan waliokuwa wamepanga mstari wakisubiri mgao wa chakula na yaliyodumu kwa karibu saa mbili. Mapigano yalizuka baada ya raia wa Afghanistan kufyatua risasi kuwalenga raia wa Eritrea.
Mapigano mengine yalizuka katika eneo la viwandani umbali wa kilimita tano, ambako mamia ya Waeritrea wenye silaha walikuwa wakipambana na kiasi ya Waafghani 20.
Ghasia hizo zimezuka wiki mbili baada ya Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron kuizuru Calais na kuapa kutoruhusu kujengwa kambi nyingine kama hiyo kwenye mji wa Calais au sehemu nyingine yoyote ya Ufaransa.
Baadae Macron alikwenda Uingereza ambako alikutana na Waziri Mkuu Theresa May na kufikia makubaliano kuwa Uingereza itaipa Ufaransa fedha zaidi kwa ajili ya kuwazuia wahamiaji wanaojaribu kuingia Ulaya kwa lengo la kwenda Uingereza, pamoja na kuimarisha usalama katika mji wa Calais.
Julai Mosi mwaka 2017 kiasi ya wahamiaji 16 walijeruhiwa baada ya mapigano kuzuka katika kambi hiyo na Juni 40, mwaka 2016, wahamiaji 40 walijeruhiwa katika mapigano yaliyozuka kwenye mji huo wa bandari.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPA, AFP, AP
Mhariri: Iddi Ssessanga