1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahamiaji wawapokea wenzao wanaowasili kutoka Afghanistan

28 Desemba 2021

Wahamiaji waliofanikiwa kuanza maisha upya Marekani wanawasaidia wenzao wanaofika baada ya kupitia masaibu kama yao.

The Wider Image: From Kabul to Kentucky: Afghans put down roots in refugee haven
Picha: Amira Karaoud/Reuters

Baada ya kupitia masaibu kama hayo mwanzoni wanafahamu umuhimu wa kuwapa wenzao waraja na kuwatuliza mioyo, hivyo wanawapa mapokezi ya kuwaliwaza punde wanapowasili Marekani.

Tram Pham, anabubujikwa machozi anapokumbuka jinsi mwanzoni maisha yalivyokuwa magumu nchini Marekani.

Lakini pia anakumbuka furaha aliyopata kama mhamiaji wa umri wa miaka 22 kutoka Vietnam, wakati nesi alizungumza naye kwa lugha yake ya mama, na kumuongoza hatua kwa hatua kufanyiwa vipimo vya afya vinavyohitajika kwa wageni wote.

Umoja wa Ulaya wajipanga kwa wimbi la wakimbizi wa Afghanistan

Takriban miongo mitatu imepita, na Pham ambaye sasa ni nesi rasmi katika kliniki ileile alikohudumiwa mwanzo iliyoko San Jose jimbo la California, anatumai kulipiza wema ule alotendewa na familia yake.

Kliniki ya TB and Refugee iliyoko Santa Clara inawahudumia wahamiaji kutoka Afghanistan, walioanza kuomba hifadhi nchini Marekani mwezi Agosti.

Picha iliyopigwa kutoka angani ikionyesha mahema ya wahamiaji kutoka Afghanistan ndani y akambi ya kijeshi ya Marekani iliyoko Ramstein, Ujerumani.Picha: Olivier Douliery/AFP/Getty Images

Pham hawezi kuzungumza Kifarsi wala Kipashto, lakini anaweza kuwatuliza wagonjwa ambao wamekumbwa na msongo wa mawazo kwa kukosa ajira au kodi za nyumba. Anaeleza jinsi siku moja alimshika mkono ajuza mmoja kutoka Afghanistan aliyetokwa machozi akimuelezea masaibu yalomsibu.

"Naona wagonjwa kutoka ulimwenguni kote huja hapa. Naam, wagonjwa kutoka Vietnam. Kila ninapowaona wagonjwa ambao ni wahamiaji, ninajiona mwenyewe,” amesema.

Ujerumani: Hatma ya wakimbizi milioni 1.8 haijulikani

Kliniki hiyo iliyoko Santa Clara, ni sehemu ya mnyororo wa mashirika ya misaada ya serikali ambayo yametwikwa jukumu la kutekeleza mpango wa Rais Joe Biden wa kuwahamisha takriban Waafghani 100,000 kutoka Afghanistan ifikapo Septemba 2022. Tayari Waafghani 48,000 wameshahamishwa hadi katika kambi za kijeshi za Marekani.

Hata hivyo operesheni hiyo imeathiriwa zaidi na upungufu wa bajeti kwa mipango ya wahamiaji uliopitishwa chini ya utawala wa rais w azamani Donald Trump.

Mfumo wa afya wa Afghanistan katika hatari ya kuporomoka

Licha ya hayo, kwa wale ambao wamehamishwa tayari, jamii imewapokea vizuri. Krish O'Mara ambaye ni kiongozi wa huduma za Kilutheri kwa wahamiaji- amesema ”tunajua kwamba mwanzo huwa mgumu na si kazi ya wiki moja au mwezi mmoja. Mafanikio yake hutokana na juhudi za miaka mingi. Na hapo ndipo tulipo.”

Shirika hilo lisilo la kiserikali linafanya kazi katika majimbo yasiyopungua mawili, tayari limewasaidia Waafghani 6,000 waliowasili Marekani kuanza Maisha mapya tangu msimu wa jua mwaka huu. Miongoni mwa wahamiaji hao, 1,400 wamepokelewa kaskazini mwa Virginia, 350 jimbo la Texas, 275 katika mji wa Washington na Oregon.

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken akikutana na wahamiaji wa Afghanistan nje ya kituo cha kuwahamisha wahamiaji kilichoko Ramstein Ujerumani.Picha: Olivier Douliery/AP Photo/picture alliance

Katika ile kliniki iliyoko San Jose, wakuu wako mbioni kuwaajiri wahudumu Zaidi kuwahudumia wahamiaji 800 wanaotarajiwa katika jimbo hilo ifikapo mwezi Septemba.

UN: Afganistan inakabiliwa na hatari ya janga kubwa la njaa

Nelda David ambaye ni meneja katika kliniki hiyo amesema wahudumu katika kituo hicho kilichoanzishwa miongo minne kuwasaidia raia wa kusini mashariki mwa Asia baada ya vita vya Vietnam, wako tayari kuwapokea wahamiaji. Isitoshe wengi wa wauguzi na wasaidizi wao wenyewe walikuwa wahamiaji kwa hivyo wanaelewa changamoto zinazowakabili wanapoanza Maisha upya katika nchi mpya.

Kwa kukutana na wauguzi kama Pham ambao awali walikuwa wahamiaji, kunawapa wahamiaji wapya faraja, matumaini, ujasiri na mfano wa kuigwa.

Mhamiaji mmoja kwa jina Deena Attaei anayezungumza Kifarsi amesema, "wamefaulu maishani. Wanafanya kazi hapa. Lugha yao ya imeimarika. Ninatumai siku moja nami nitafanikiwa na nisimame kivyangu.

(APE)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW