1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hadi sasa zaidi ya 300 hawajulikani waliko

Admin.WagnerD6 Agosti 2015

Zaidi ya wahamiaji 200 wanahofiwa kufa maji baada ya boti waliyokuwa wakisafiria katika bahari ya Meditarrania kuzama hapo jana. Boti hiyo iliyokuwa imejaza abiria kupita kiasi imezama Karibu na ufuo wa Libya.

Meli ya Italia ikiwaokoa wahamiaji
Meli ya Italia ikiwaokoa wahamiajiPicha: Reuters/M. Soszynska

Boti hiyo inayoaminika kuwabeba zaidi ya wahamiaji 600 wakiwemo watoto na wanawake ilikumbwa na matatizo maili kadhaa kutoka Libya na kutoa wito wa kutaka kusaidiwa ambao ulipokelewa na askari wa majini wa Italia katika kisiwa cha Sicily.

Msemaji wa askari wa majini wa Italia Filippo Marini amesema kiasi ya wahamiaji 400 wameokolewa huku miili 25 ikiopolewa kutoka majini kufikia sasa.

Meli ya jeshi la majini ya Ireland na nyingine iliyotumwa na shirika la kimataifa la madaktari wasio na mipaka MSF zilikuwa za kwanza kuwasili katika eneo la mkasa kusaidia katika operesheni za uokozi.

Watoto kadhaa waokolewa

Kulingana na maafisa wa Ireland, watu 367 wakiwemo wanawake 12 na watoto 13 wameokolewa katika operesheni hiyo huku wengine sita akiwemo mtoto wa chini ya mwaka mmoja na mhanga mwingine aliyevunjika mguu wamepelekwa katika kisiwa cha Lampedusa.

Boti za wahamiaji zinakuwa zimejazwa kupita kiasiPicha: Reuters/Irish Navy

Msemaji wa shirika la kushughulikia wakimbizi la umoja wa Mataifa UNHCR Melisa Fleming amesema kulingana na taarifa kutoka kwa walionusurika, boti hiyo iliyokuwa imejaa kupita maelezo ilipinduka baada ya wahamiaji hao kusogea upande mmoja baada ya kuiona meli ya kijeshi iliyokuwa inakuja kuwaokoa na hivyo uzito ukaegemea upande mmoja.

Meli saba, helikopta kadhaa na ndege isiyoendeshwa na rubani zinasaidia katika operesheni ya kuwatafuta wahanga wa ajali hiyo. Kulingana na shirika la kimataifa la kushughulikia wahamiaji IOM zaidi ya wahamiaji elfu mbili wamekufa majini mwaka huu wakijaribu kuvuka bahari hiyo ya Meditarrania kuingia barani Ulaya.

Ajali hiyo ya jana inahofiwa kuwa huenda ikawa mbaya zaidi tangu kiasi ya wahamiaji 800 kufariki majini mwezi Aprili mwaka huu. Mkasa huo wa hivi punde unatarajiwa kuangaziwa zaidi katika mjadala mkali kuhusu ongezeko la wahamiaji barani Ulaya, suala ambalo limekuwa msumari moto kwa nchi wanachama wa umoja wa Ulaya.

Libya imekuwa uchochoro wa wahamiaji wanaoingia Ulaya kwa njia haramu

Nchi za Ulaya zatakiwa kuwajali wakimbizi

Hapo jana Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean Claude Junker ameziambia serikali za nchi wanachama wa umoja huo kuwa zina wajibu wa kuwasaidia wahamiaji wanaowasili barani Ulaya kwa maelfu na sio kufuatwa mfumo wa siasa za kujali maoni na fikra za umma za kutaka wahamiaji hao kurejeshwa makwao.

Junker amesema amevunjwa moyo kuwa mawaziri wa umoja wa Ulaya walishindwa mwezi uliopita kukubaliana jinsi ya kugawana wahamiaji 40,000 wengi wao kutoka Syria na Eritrea walioshukia Italia na Ugiriki na kuongeza mawaziri na sio wananchi ndiyo walio na jukumu la kuchukua hatua za kuwasaidia wahamiaji.

Umoja wa Ulaya ulikuwa umependekeza mfumo wa kuzishurutisha nchi wanachama kugawana mzigo wa wahamiaji, pendekezo ambalo linapingwa na baadhi ya nchi 28 za umoja huo.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi