1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahanga wa shambulio la Ugaidi wakumbukwa

Mjahida8 Januari 2015

Kengele zimepigwa katika kanisa katoliki la Notre Dame mjini Paris, wakati raia wa Ufaransa walipowakumbuka wahanga wa shambulizi la kigaidi katika ofisi ya jarida la Charlie Hebdo

Wafaransa wanyamaa kimya kwa dakika moja kuwakumbuka wahanga wa shambulio la Charlie Hebdo
Wafaransa wanyamaa kimya kwa dakika moja kuwakumbuka wahanga wa shambulio la Charlie HebdoPicha: Reuters/P. Wojazer

Raia hao wamekusanyika katika makao makuu ya ofisi ya jarida la tashtiti la Charlie Hebdo, kuweka maua na kutoa heshima zao mahali kulikotokea shambulizi la kigaidi hapo jana.

Bendera nchini humo zilipepea nusu mlingoti, ishara ya kuomboleza vifo vya watu 12 waliouwawa hapo jana. Watu hao ni pamoja na waandishi wanane wa habari, maafisa wawili wa polisi, mfanyakazi mmoja na mgeni aliyetembelea ofisi hiyo.

Maua, mishumaa na ujumbe uliwekwa mahali palipotokea shambulioPicha: picture-alliance/dpa/Paul Zinken

Raia waliokuwa katika eneo hilo waliweka kalamu, kuwasha mishuma na hata vijikaratasi vilivyokuwa na ujumbe wa huzuni na kulaani kitendo hicho. Mwanamke mmoja alisema kwa sauti “Mshikamano na Uhuru” huku akibubujikwa na machozi. Na ilipofika saa sita juu ya alama hivi ndivyo hali ilivyokuwa nchini Ufaransa.

Wafaransa walinyamaa kwa dakika moja kuwakumbuka wahanga wa shambulio hilo la kigaidi. Baadaye raia hao waliimba wimbo wa taifa, huku wakilia, wengi wakiwa na kalamu na penseli ishara ya wachora vibonzo waliolengwa katika shambulio hilo.

Wakati huo huo Rais wa Ufaransa Francois Hollande amewataka wananchi kuungana dhidi ya ugaidi na kutovumiliana. Rais Hollande pia ameongoza mkutano wa dharura uliohudhuriwa na Rais wa zamani Nicholas Sarkozy, Waziri Mkuu Manuell Valls, Viongozi wakuu wa Usalama pamoja na viongozi wengine wa juu serikalini.

Naye Pierre Desirat, mkaazi wa Paris aliye na miaka 48, amesema amesikitishwa na tukio la jana na amejitokeza kuonesha mshikamano kwa raia wenzake wa Ufaransa.

Polisi waendelea kushika doria katika sehemu tofauti nchini UfaransaPicha: Reuters/G. Fuentes

"Nimekuja hapa kuwa pamoja na wenzangu kuonesha mshikamanokwa jarida hili, waandishi habari, na polisi na Ufaransa yote kwa Ujumlana ilioumizwa kutokana na tukio la jana. Nimekuja tu kama raia wa kawaida," alisema Pierre Desirat.

Bado hali niya wasiwasi nchini Ufaransa.

Huku hali ya wasiwasi ikiendelea kutanda nchini humo, polisi wanaendelea kuwatafuta ndugu wawili wanaoaminika kujihami kwa silaha wanaohofiwa huenda wakatekeleza shambulizi jengine la kigaidi.

Wanaume hao Cherif Kouachi,aliye na miaka 32 na kakaake Said Kouachi aliye na miaka 34 wanaaminika kutekeleza shambulizi dhidi ya jarida la Charlie Hebdo kutokana na gazeti hilo kuwahi kuchora kibonzo kilichomkejeli au kumtashtiti mtume wa dini ya kiislamu, mtume Mohammed.

Wakati hayo yakiarifiwa Serikali ya Uingereza imesema imeimarisha zaidi usalama katika mipaka yake ikiwemo katika bandari na vituo vya ukaguzi maeneo wanayofanyia kazi nchini Ufaransa, kutokana na shambulio la kigaidi, naye kiongozi wa kanisa katoliki Papa Francis, ameongoza ibada ya misa ya kuwakumbuka wahanga wa shambulio hilo huku akikemea ukatili dhidi ya binaadamu.

Ujumbe unaosema mimi ni Charlie "JE SUIS CHARLIE"Picha: charliehebdo.fr

Aidha hii leo kumekuwa pia na taarifa za mashambulizi mengine dhidi ya polisi kusini mwa Ufaransa, ambako watu waliokuwa kwenye gari wamewapiga risasi polisi wawili na kumuua mmoja wa kike. Waendesha mashtaka nchini humo wamesema wanalichunguza tukio hilo kama tukio la kigaidi.

Mwandishi Amina Abubakar/dpa/AP/Reuters

Mhariri Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW