1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri Ujerumani wazungumzia sheria ya chuki na uzushi

6 Aprili 2017

Wahariri wanazungumzia mkutano kati ya Marais wa Marekani Donald Trump na Xi Jinping wa China, hali nchini Syria na muswada wa sheria ya kupambana na chuki na habari za uzushi za mitandaoni nchini Ujerumani.

Bundesjustizminister Maas - Kinderehen und Hasskommentare im Internet
Waziri wa sheria wa Ujerumani Heiko Maas ameonya kuwa makumpuni ya mitandao ya kijamii yatatozwa faini kubwa yakishindwa kuchukua hatua za haraka kuhusu machapicho cha chuki na uzushi.Picha: picture-alliance/dpa/P. Zinken

Mhariri wa gazeti la Der Tagesspiegel la mjini Berlin anasema Syria inalilia uingiliaji, lakini si Marekani wala China iliyo tayari kuingilia kati. Usemi huo zinao Urusi na Uturuki, na mkakati wao hauhusiani chochote na maadili na uwajibikaji. Hapa Marekani haijaingilia, na matokeo yake yamekuwa ya kutisha. Hii inashangaza ikilinganishwa na malalamiko ya miaka iliopita, kuhusu madhara hasi pale Marekani ilipoingilia kati.

Wahari wa magazeti ya Lübecker Nachrichten, Staubinger Tagblatt, Fränkischer Tag wamekita maoni yao kuhusu Syria katika muktadha wa mashambulizi ya kikemikali yaliouwa watu zaidi ya 70 na mkutano wa wafadhili wa kimataifa kwa ajili ya nchi hiyo uliomalizika Jumatano mjini Brussels.

Mkuu wa sera ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini akizungumza na waandishi habari wakati wa mkutano wa kimataifa kuhusu Syria mjini Brussels, Aprili 4, 2017.Picha: Reuters/F. Lenoir

Mhariri wa gazeti la Staubinger Tagblatt ameandika kuhusu mkutano wa mjini Brussels akisema: Jumuiya ya kimataifa ina njia moja tu ya kufanya chochote. Inaweza kuziwezesha nchi jirani za Lebanon, Jordan na Uturuki kuchukuwa wakimbizi zaidi. Katika makambi inaweza kusaidia ufadhili wa huduma za afya na uwezeshaji wa kijamii; vijana wanaweza kusaidiwa kielemu au kupewa mafunzo ya kiufundi. Wanawake na wanaume wanaweza kusomeshwa, kwa sababu wao ndiyo kizazi kitakachoijenga upya nchi yao kisiasa, kiuchumi na kijamii, na pia linapokuja suala la demokrasia.

Sheria ya kupambana dhidi ya chuki na uzushi mitandaoni

Serikali ya Ujerumani imeidhinisha muswada wa sheria ambayo itayatoza faini kubwa makampuni ya mitandao ya kijamii kama vile Facebook na twitter, ikiwa yatashindwa kufuta mara moja machapicho ya kuchochea chuki, kukashifu au maudhui nyingine zinazokiuka sheria za Ujerumani, mfano habari za uzushi. Waziri wa sheria  Heiko Maas alirudia onyo lake kwamba makampuni ya mtandaoni yanayoshindwa kufuta maudhui ya jinai wenyewe wanaweza kukabiliwa na faini za hadi euro milioni 50.

Juu ya sheria hiyo mpya, mhariri wa gazeti la Münchner Merkus ameandika: Matamshi ya chuki na habari za uzushi ni vitu viwili vinavyotisha. Kwa bahati mbaya serikali inajaribu kuzuwia vitisho hivi kwa kutengeneza kitisho kingine kikubwa zaidi: Sheria ya waziri Maas inazuwia uhuru wa mawazo na utofauti wa maoni. Nani anayo mamlaka ya kuamua iwapo madai kuhusu mtu fulani ni ya kweli au la? Mitandao ya utafiti ya serikali au serikali yenyewe? Au Mitandao ya Kijamii kama Facebook na twitter? Katika Jamii iliyo huru, wote hao hawajapewa jukumu la kuwa polisi wa maoni. Mahakama tayari zinasaidia kupambana na kuenea kwa matamshi ya chuki na kashifa. Na dhidi ya habari za uzushi, uhakiki kupitia vyombo vya kitaaluma vinavyofanya utafiti makini, na hicho ndicho kinaitwa uandishi habari.

Eneo la mapumziko la Eau Palm Beach ambako rais wa China atakaa wakati wa ziara yake atakapokutana na rais Donald Trump.Picha: Reuters/J. Skipper

Mkutano kati ya marais Donald Trump na Xi Jinping

Naye mhariri wa gazeti la General-Anzeiger la hapa Bonn, anasema kufutwa tu kwa ujumbe wa chuki na uzushi kwenye mitandao siyo suluhisho endelevu kwa ugonjwa huu mbaya wa zama zetu. Mhariri wa gazeti la Stuttgarter Zeitung ameandika juu ya mkutano kati ya Rais wa Marekani Donald trump na mwenzake wa China Xi Jinping. Anasema kadiri Trump anavyozidi kusisitiza juu ya kaulimbiu yake ya Marekani kwanza, ndipo China inavyojiweka sawa kuchukuwa nafasi iliokuwa nayo Marekani ulimwenguni. Lakini mhariri wa gazeti la Die Zeit ameandika:

Xi anataka kuepusha makabiliano yoyote na Marekani au hata kuyachelea, kwa sababu anafahamu hawezi kushinda bado. Nguvu ya kijeshi na kiuchumi ya Marekani iko juu sana ikilinganishwa na China. Kutotabirika kwa Trump ni jambo hatari kwa Xi. Lakini wakati huo Trump anafungua fursa kubwa kwa Wachina. Kama kuna wakati mzuri zaidi kwa China kupanua ushawishi wake kimyakimya na kwa taratibu, basi wakati huo ndiyo huu. Trump anaacha milango wazi, wanapaswa tu kupita.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/deutsche zeitungen

Mhariri: Daniel Gakuba

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW