1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri wa magazeti juu ya mkutano wa G20

Abdu Said Mtullya19 Juni 2012

Wahariri wa magazeti wanatoa maoni juu mkutano wa nchi za G 20 unaomalizika leo katika kitongoji cha mapumziko cha Los Cabos nchini Mexico.

Viongozi wa nchi za G20 nchini Mexico
Viongozi wa nchi za G20 nchini MexicoPicha: Reuters

Mhariri wa gazeti la  "Saarbrücker "anasema mkutano  wa nchini Mexico na mingine ya dunia haipaswi kuweka mkazo katika kuzuia athari za mgogoro
tu. Kutokana na uchumi kushuka na idadi ya wasiokuwa na ajira kuongezeka,inapasa kuchukua hatua siyo tu za kuepusha athari za migogoro kuenea bali, sambamba na kuzitekeleza sera za kubana matumizi na kuleta mageuzi,ni muhimu kuchukua hatua za kustawisha uchumi.


Mhariri wa gazeti la "Landeszeitung"  pia anatoa maoni yake juu ya mkutano wa nchi za G20. Mhariri huyo anawasilisha ujumbe kwa viongozi wa nchi hizo kwa kusema  kwamba mgogoro wa madeni haupo barani Ulaya tu. Anasema anaefikiri kwamba mgogoro wa madeni umeishia ndani ya mipaka ya bara la Ulaya anakosea sana. Mfumo wa fedha duniani unahitaji taratibu mpya. Na kwa hivyo viongozi wa nchi za  G20 wanatakiwa wachukue hatua haraka.

Gazeti la "Saarbrücker" linazungumzia  juu ya uchaguzi uliofanyika nchini Ugiriki.Mhariri wa gazeti hilo anasisitiza kwamba bara la Ulaya ni kitu kimoja hata  ikiwa baadhi ya watu hawataki. Mhariri huyo anafafanua kuwa pana njia mbili kwa Umoja wa Ulaya. Ama kila nchi iyadhibiti mambo yake ya bajeti kitaifa au pawepo utaratibu wa nchi  tajiri kuzibeba nchi dhaifu  kifedha. Lakini hakuna anaeyasema   hao kwa sauti kubwa. Ukweli ni kwamba Ulaya ni kitu kimoja. Maana yake ni kwamba matatizo ya nchi moja, pia ni matatizo ya wengine wote.Huo ndiyo mtazamo wa pekee utakaosaidia.

Mhariri wa gazeti la "Sächsiche" anazungumzia hali ya kisiasa ya nchini Misri.Anasema majenerali wa nchi hiyo wanafanya vituko Mhariri huyo anasema Majenerali hao wanaahidi kuyarejesha mamlaka katika mikono ya raia ,lakini  wakati huo huo wanajihakikishia mamlaka wao wenyewe na wanafanya juhudi ili kuzirejesha enzi za hapo awali.

Kwa kadri mvutano wa kugombea mamlaka unavyoendelea ndivyo jamii pia inavyoendelea kugawanyika.Kutokana na hali hiyo hapatakuwa na utulivu nchini Misri.Na jambo la kutisha sana ni kwamba hakuna anaeyashughulikia matatizo   halisi yanayoikabili nchi.

Naye mhariri wa gazeti  la "Südwest Presse" anasema furaha imetoeka nchini Misri. Bunge lililochaguliwa kwa njia za kidemokrasia limevunjwa. Mpango wa kukabidhi mamlaka kwa raia umeshasambaratika.Na wakati wananchi wamepiga kura ya kumchagua Rais, majenerali wameshaamua kumgeuza Rais huyo kuwa kibogoyo. Matumaini ya hapo awali hayapo tena, majamvi yameshakunjwa nchini Misri, tafrija imekwisha.

Mwandishi:Mtullya abdu/Deustche Zeitungen/

Mhariri:Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW