Wahariri wa Ujerumani waziona zama mpya ya siasa
25 Septemba 2017Mhariri wa Frankfurter Allgemeine Zeitung anasema ni wazi kuwa Kansela Angela Merkel wa chama cha Christian Democratic Union (CDU) hana wafuasi wengi, anasema mhariri huyo, akiongeza kwamba hivyo ndivyo hali ilivyokuwa hadi wiki nne zilizopita, wakati chama mwenza cha Christian Social Union (CSU) kikipiga kampeni zake kwa uchaguzi wa jana.
Lakini kisha ule umashuhuri wa Kansela Merkel ulioshuka vibaya kutokana na mzozo wa wahamiaji, ukapanda tena juu kwa sababu ya mambo mawili: utulivu wa kisiasa na uchumi imara.
Na mgombea mwenzake wa ukansela kutoka chama cha Social Democrats (SPD), Martin Schulz, akajikuta akishindwa kuushusha tena umashuhuri huo, licha ya kutumia mapungufu ya hapa na pale na hali ya Wajerumani kutoridhika na baadhi ya mambo yanayotokezea, ili kuwabadilisha mawazo yao.
Ukweli ni kuwa wapigakura hawakutaka kufahamu, maana ni kama kwamba alikuwa anataka kuonesha kuwa SPD ilikuwa kwenye upinzani miaka minne mizima iliyopita, na ilhali ilikuwa sehemu ya serikali hii hii.
Waliopoteza hasa ni CDU na SPD
Mhariri wa gazeti la Süddeutsche Zeitung anasema kuwa kwa SPD iliyojikuta kuwa imepoteza zaidi ya asilimia 5 na CDU iliyopoteza zaidi ya asilimia 8 kwenye uchaguzi wa jana, kuna habari njema moja tu: nayo ni kuwa Krismasi inakuja baada ya miezi mitatu kutoka sasa.
SPD na CDU ndio waliopoteza sana kwenye uchaguzi huu.
Kwa CSU, chama ndugu cha CDU, matokeo ya uchaguzi huu huko Bavaria ni kituko zaidi. Chama hiki kimetupwa, kimepoteza fahari yake.
Kwa SPD, Martin Schulz ameshindwa kukizamua kutoka shimo kilichozama, na ndio maana akatangaza hapo hapo kuwa atakwenda kwenye upinzani moja kwa moja.
Hiyo ni hatua njema ya kukisaidia kuishi.
Ujerumani yachukuwa mwelekeo mpya?
Baada ya kukiona chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Alternativ fuer Deutschland (AfD) kikiwa na ongezeko la takribani asilimia 8 kwenye uchaguzi wa jana, mhariri wa gazeti la Rheinische Post anasema hizi ni zama za mwishoni mwa jamhuri iliyojengwa kwa umakini mkubwa na kwa maridhiano baada ya vita vya pili vya dunia.
"Taifa hili linaelekea kwenye siasa kali za mrengo wa kulia", anasema mhariri huyo.
Pakiwa na sauti zisizonyamazika na zaidi ya wabunge 80 kwenye bunge la shirikisho, yaani Bundestag, wenye kupingana na mfumo ulioasisi dola hii, wenye ghadhabu dhidi ya wageni, na azma ya kuandika fasili nyengine ya demokrasia "hapana shaka, Ujerumani imeanza kuchukuwa njia nyengine kuelekea hatima yake yenyewe."
Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa
Mhariri: Saumu Yussuf