1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri wa Ujerumani wazungumzia mzozo wa Darfur

7 Julai 2023

Hofu haina mwisho katika jimbo la Darfur. Jeshi la Ujerumani laondoka Mali. Macky Sall hatagombea urais wa Senegal. Kenya yaruhusu ukataji miti na kambi ya kampuni ya Wagner yashambuliwa Libya.

Sudan West Darfur | Geneina
Picha: Str/AFP

Gazeti la die Tageszeitung ambalo liliandika kuhusu vita katika jimbo la Darfur magharibi mwa Sudan. Hakuna mwisho kwa hofu jimbo la Darfur, ndivyo alivyoandika mwandishi wa gazeti hilo, Dominic Johnson. Wakimbizi sasa wanakadiria idadi ya vifo imefikia 8,000, idadi ya wahanga wa mauaji ya kiholela yaliyofanywa na wanamgambo wa kikosi cha Rapid Support Forces, RSF, katika mji wa magharibi wa El-Geneina jimboni Darfur tangu katikati ya mwezi Juni.

Katika ripoti ya hivi karibuni redio ya taifa ya Sudan, Radio Dabanga, iliwanukuu wakimbizi kutoka mji mkuu wa Darfur Magharibi, El Geneina, ambao walifanikiwa kufika mji wa Adré katika nchi jirani ya Chad. Mmoja wao aliiambia redio hiyo kwamba wapiganaji wa RSF wameuharibu kabisa mji wa El Geneina na hakuna kilichobaki.

Mji wa El Geneina ulikuwa makazi kwa maalfu ya watu, lakini takriban nusu kati yao wanaishi katika kambi za wakimbizi baada ya kulazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na vita katika miongo iliyopita. Kwa mujibu wa maelezo ya wakimbi, mbali na vitongoji viwili tu, mji wote umeharibiwa.

Wapiganaji wa RSF walianza mashambulizi katika kambi za wakimbizi mnamo Aprili mwaka huu na mnamo Juni 14 wakamuua gavana wa jimbo la Darfur Magharibi katika mji wa El Geneina na tangia hapo wamechukua madaraka. Watu wa kabila la Masalit ambao waliponea chupu chupu kuuwawa na wanamgambo wa RSF walikimbia kutoka eneo hilo kuyanusuru maisha yao.

Bundeswehr yaondoka Mali

Gazeti la Die Zeit liliandika kuhusu jeshi la Ujerumani kuondoka nchini Mali. Mwandishi wa gazeti la Die Zeit Bastian Berbner aliandika kwamba jeshi la Ujerumani, Bundeswehr, limechukua miaka kadhaa nchini Mali kujaribu kulinda na kudumisha amani na usalama, lakini sasa sharti liondoke. Mwandishi huyo aliwatembelea wanajeshi wa Ujerumani ambao wanajiuliza kile ambacho wamekifanikisha wakati wakiwa nchini Mali.

Kuna njia moja tu ya ndege; barabara ya lami ya mita 2,500 karibu na mji wa jangwani wa Gao. Anayeudhibiti mji huo wa mashariki mwa Mali basi ana fursa ya kuutawala, kwa sababu eneo hilo ni mojawapo ya maeneo yanye hali mbaya sana ya hewa duniani na halikaliki. Kuna barabara chache sana huko. Hakuna njia za reli. Mto wa Niger ambao katika baadhi ya maeneo maji yake yana kima cha kufikia magotini tu, ni vigumu sana kuutumia kwa safari.

Mwisho wa njia hii ya ndege, upande wa magharibi ndiko kwenye kambi ya jeshi la Ujerumani, Bundeswehr, mkabala na Umoja wa Mataifa. Kisha kuna jeshi la Mali ambalo ndilo linalosimamia eneo zima. Na upande wa mashariki ni Warusi. Mhariri anauliza ni nani anayeruhusiwa kusafiri kwa ndege na wakati gani? Kwa raia wa Mali jibu la swali hili litaamua kinachowafikia kutoka angani, kama ni chakula, maji, msaada au kifo.

Macky Sall, rais wa SenegalPicha: Lewis Joly/AP/picture alliance

Macky Sall hatogombea urais wa Senegal

Hakuna awamu ya tatu kwa rais wa Senegal Macky Sall. Ndivyo lilivyoandika gazeti la Tageszeitung. Katika hotuba ya televisheni iliyosubiriwa kwa hamu kubwa, rais huyo alisema hatagombea awamu ya tatu ya urais katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Februari mwakani.

Mwandishi wa gazeti la die Tageszeitung Dominic Johnson ameandika kwamba kwa ahadi hiyo, rais Macky Sall aliepusha machafuko mabaya ambayo hayangekuwa na mithili, angalau kwa sasa. Mwandishi huyo pia amesema kauli ya rais Sall imetuliza hali ya mambo nchini Senegal na kuepusha wimbi la ghadhabu la vuguvugu linalompinga.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine pia liliandika kuhusu uamuzi wa rais Macky Sall kutogombea urais wa Senegal. Mwandishi wa gazeti hilo mjini Cape Town nchini Afrika Kusini, Claudia Bröll, alisema rais Sall alifikia uamuzi huo kufuatia machafuko yaliyoshuhudiwa katika mandamano ya kupinga uwezekano wa yeye kugombea muhula wa tatu. Tetesi kwamba Sall angegombea awamu ya tatu kinyume na katiba ulisababisha mtafuruku na wasiwasi katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi ambayo kimsingi imekuwa thabiti.

Kenya yaruhusu tena ukataji miti

Kenya imeruhusu tena ukataji wa miti huku rais wa nchi hiyo William Ruto akipania kuimarisha uchumi na wanaharakati wa mazingira kwa upande wao wakitahadharisha juu ya kutokea athari kubwa. Mwandishi wa gazeti la die Tageszeitung Simone Schlindwein aliandika kwamba rais Ruto alisema uamuzi huo ulichelewa, wakati alipokuwa akitoa hotuba mbele ya waumini mjini Molo, takriban kilometa 200 kaskazini magharibi mwa mji mkuu, Nairobi.

Gazeti lilimnukuu rais Ruto akisema hatuwezi kuiruhusu miti iliyozeeka kuoza maporini huku jamii zinateseka kutokana na ukosefu wa kuni na mbao, huu ni ujinga. Siku moja kabla rais Ruto alikuwa ameshiriki shughuli ya upandaji miti katika wilaya tatu za eneo la Bonde la Ufa. Eneo la kusini la Bondo la Ufa lilikuwa maarufu kwa sekta ya mbao, ambamo vijana na wanaume ambao hawakufanikiwa kupata elimu katika viwango vya juu walipata ajira kama wakataji miti na wabebaji wa magogo au maseremala.

William Ruto, rais wa KenyaPicha: Ihsaan Haffejee/AA/picture alliance

Kambi ya Wagner yashambuliwa Libya

Gazeti la Tagesspiegel liliandika kuhusu wapiganaji mamluki wa Urusi nchini Libya. Gazeti liliandika kwamba  kampuni ya wapiganaji mamluki ya Wagner walishambuliwa katika kambi ya jeshi ya Al Khadima nchini Libyainayotumiwa na kampuni hiyo. Kambi hiyo ilishambuliwa kwa ndege isiyo rubani mwishoni mwa wiki iliyopita. Kambi hiyo inapatikana karibu na mji wa Kharruba, kiasi kilometa 150 kusini mashariki mwa mji wa bandari wa Benghazi. Jeshi la Libya lilinukuliwa likisema hakukuwa na wahanga katika hujuma hiyo.

Kambi hiyo ilishawahi kushambuliwa kwa makombora mnamo mwezi Januari mwaka huu, ambapo ndege ya Urusi iliharibiwa. Serikali ya Libya imethitisha shambulizi hilo jipya, lakini afisa wa jeshi la Libya amesema chanzo chake hata hivyo hakifahamiki.

Gazeti limesema Marekani inashukiwa kwa kuwa inaona mgogoro kati ya kiongozi wa kampuni ya Wagner Yevgeny Prigozhin na utawala wa Urusi kama fursa ya kuongeza shinikizo dhidi ya kampuni hiyo katika eneo la Mashariki ya Kati na barani Afrika. Mwanzoni mwa wiki iliyopita, Marekani ilitoa orodha ya vikwazo vipya dhidi ya kampuni inazoamini zinasaidia kuifadhili kampuni ya Wagner Mashariki ya Kati. Serikali ya Marekani bado haijatoa kauli yoyote kuhusu tukio hilo.

Ujerumani ina kibarua kipevu kuelekea kombe la EURO 2024

Kevin-Prince Boateng, mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya kandanda ya Ghana, bado anaona kuna kazi kubwa katika kikosi cha timu ya taifa ya soka ya Ujerumani. Liliandika gazeti la mtandaoni la Welt Online. Kevin-Prince Boateng anaona bado timu ya taifa ya Ujerumani ina kibarua kipevu sana cha kufanya mwaka mmoja kabla mashindano ya kandanda ya kuwania kombe la EURO 2024 yatakayoandaliwa hapa Ujerumani. Mzaliwa huyo wa mji mkuu Berlin, ambaye ni balozi wa mashindano ya Ulaya, amesema matumaini yapo kwa Ujerumani kuwa timu ya kuogopwa tena.

Akizungumza siku ya Jumatatu mjini Berlin, Kevin Prince Boateng pia alisema timu ya taifa ya Ujerumani kwa sasa siyo ile inayofahamika na ukali wake, na hii inaonekana kwa jinsi mashabiki walivyopoteza morali na hamu ya kuitazama inapocheza. Hii ni kutokana na jinsi wanavyocheza kwa sasa, timu hiyo ikishindwa kuleta ushindi nyumbani. Kevin Prince Boateng, mchezaji wa klabu ya Hertha Berlin inayocheza katika ligi kuu ya Ujerumani, Bundesliga, aliwahi kuichezea Ghana mechi mbili za kombe la dunia dhidi ya Ujerumani.

(Inlandspresse)