1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri walalamikia udhaifu ICC

Abdu Said Mtullya15 Machi 2012

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanatoa maoni yao juu ya hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya mjini the Hague kwa Thomas Lubanga. Lakini wengi wanasema Mahakama ya ICC ina udhaifu.

Mwendesha mashtaka Mkuu wa ICCLusi Moreno Ocampo
Mwendesha mashtaka Mkuu wa Mahakama Kuu ya ICC,Luis Moreno OcampoPicha: AP

Mhariri wa gazeti la "Westfalen Blatt" anasema hukumu iliyotolewa kwa Thomas Lubanga imethibitisha kwamba maditketa na wahalifu wa kivita hawataweza tena kujifanya viwizi ishara zinapotolewa na jumuiya ya kimataifa.

Hukumu hiyo ilikuwa ya kwanza kutolewa na Mahakama ya mjini The Hague tokea ilipoanzishwa mnamo mwaka wa 2002.Mhariri wa gazeti la "Westfalen Blatt" anatilia maanani kwamba Mahakama hiyo inatofautiana na zile zilizohukumu kesi za Yugoslavia ya zamani na za Rwanda.

Mahakama ya Kimataifa ya mjini The Hague ilianzishwa katika msingi wa mkataba wa kimataifa. Hoja hiyo inaifanya Mahakama hiyo iwe na nguvu. Lakini mhariri huyo anasema Mahakama hiyo bado ina udhaifu.Nchi muhimu hazimo,ikiwa pamoja na Marekani,China na Urusi.

Mhariri wa gazeti la "Frankfurter Rundschau" pia anasema hukumu iliyotolewa jana na Mahakama ya Kimataifa ya mjini The Hague ilikuwa hatua ya kihistoria .Anasema hukumu hiyo imetoa ishara kwa wahalifu kwamba hawana tena mahala pa kujificha. Lakini mhariri wa "Frankfurter Rundschau" pia anasikitika juu ya udhaifu wa mahakama ya mjini The Hague.

Mhariri huyo anaeleza kuwa hukumu iliyotolewa dhidi ya Thomas Lubanga imeilinda hadhi ya Mahakama ya ICC japo ilichukua muda mrefu sana kuifikia. Lakini hukumu hiyo pia ni tuhuma juu ya nchi zilizojiweka mbali na Mahakama hiyo, ikiwa pamoja na Marekani,China,Sudan na Israel.

Gazeti la "Financial Times Deustchland" pia linasema kwamba Mahakama ya Kimataifa ya mjini The Hague bado ina udhaifu,mambo mengi hayajakamilishwa.

Mhariri wa gazeti hilo anafafanua kuwa kesi iliyomkabili Lubanga ilichukua muda mrefu sana kiasi kwamba watu walikuwa na mashaka iwapo hukumu ingelifikiwa. Pia mtuhumiwa mwenyewe aliwekwa katika kizimba cha uchunguzi kwa muda mrefu. Kutokana na hayo inapasa kufikiria njia za kufupisha muda wa kesi, kama jinsi ilivyo katika mahakama nyingine duniani.

Gazeti la "Die Welt" linasema itachukua muda mrefu kabla ya kazi ya Mahakama ya mjini The Hague kuweza kuwa na nguvu ya kuzuia uhalifu duniani. Lakini kuanzishwa kwa mahakama hiyo ilikuwa hatua ya lazima.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri:Abdul-Rahman