1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri wamulika uamuzi wa serikali ya Uengereza kuhusu katiba ya Umoja wa Ulaya

7 Juni 2005

Uamuzi wa serikali ya Uengereza wa kuakhirisha kura ya maoni ya katiba ya Umoja wa Ulaya, ndio mada iliyochambuliwa kwa mapana na marefu na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

Gazeti la mjini Berlin „Die Welt“ linaandika:

„Waengereza wameonyesha kweli wao ni wakweli. Katika wakati ambapo, licha ya „la“ ya Ufaransa na Uholanzi, viongozi kadhaa wa serikali na hata madhamana wanaomzunguka mwenyekiti wa kamisheni kuu ya Umoja wa Ulaya, Barroso, wanajidanganya na kudai kijuu juu eti utaratibu wa kuidhinishwa katiba ya Umoja wa Ulaya uendelezwe, serikali ya mjini London inasema kinaga ubaga kile ikionacho: “Mataifa mawili ya mstari wa mbele barani Ulaya yameikataa katiba ya Umoja wa Ulaya. Hasa Uengereza, nchi yenye kujivunia demokrasia ya jadi, imekua tangu enzi za kale bila ya katiba. Haielewi kwa hivyo kwanini hali hiyo iwe muhali kwa Umoja wa Ulaya. Cha muhimu zaidi ni kujishughulisha na kile mtu alicho nacho. Paris na Berlin haziwezi kujiwekea matumaini ya dhati eti mkutano wa dharura unaweza kufikia uamuzi kuhusu mustakbal wa Ulaya. Uamuzi wa London unabidi umtanabahishe Schröder.“

Gazeti la "Stuttgarter Nachrichten" lina maoni sawa na hayo, na linasema:

„Wanafanya kana kwamba hakuna "No" ya Ufaransa na "Nee" ya Wadachi; Schröder na Chirac wanashikilia tuu utaratibu wa kuitishwa kura ya maoni ya katiba uendelezwe katika nchi zilizosalia zanachama. Wanafikiri wapigakura hawajui kipi chema kwao, ndio maana matakwa yao hayazingatiwi. Tony Blair ameonyesha kuna njia nyengine pia inayoweza kufuatwa. Waziri mkuu wa Uengereza ametathmini vilivyo hali ya mambo na kuamua ipasavyo kuambatana na matakwa ya wananchi wenzake. Busara hiyo imempatia fursa aonekane kuwa ni mtu anaetetea masilahi ya pande zote mbili: Kiongozi wa taifa anaetamka „ Ndio“ kwa Ulaya lakini wakati huo huo anatilia maanani pia hofu za wapinzani. Kwa namna hiyo, mageuzi yana nafasi nzuri ya kusonga mbele, serikali ya mjini London itakapokua mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya mnamo nusu ya pili ya mwaka huu.“

Gazeti la "Kölnische Rundschau" linahisi:

„Hata kama kuna wasiotaka kuamini, katiba ya Umoja wa Ulaya imekataliwa. Uengereza imeonelea bora kuakhirisha utaratibu wa kuiidhinisha katiba hiyo. Kwa maneno mengine, Ujerumani na Ufaransa zimepatiwa wasaa wa kukabiliana na ukweli wa mambo. Hakuna shaka yoyote lakini, kinachowazungusha akili waingereza sio suala la jinsi ya kuinusuru katiba hiyo, bali lile la kutaka kujua ulaya ya kesho itafuata njia gani? Na hapo ndipo hitilafu za maoni zinapojitokeza.“

Hata gazeti la mjini Gera, "Ostthüringer Zeitung" linahisi uamuzi wa Uengereza unamaanisha „mwisho“ wa katiba ya Umoja wa Ulaya. Gazeti linaandika:

„Uengereza imeizika katiba ya Umoja wa Ulaya. Mahubiri ya kaburini yalitolewa kwa upole kabisa, lakini matokeo yake ni yale yale, hayakubadilika; kuakhirisha haimaanishi chengine isipokua „kuachana tena milele.“ Kwamba katiba hiyo idurusiwe, si suala linalowashughulisha tena wakaazi wa kisiwani. Jinsi madhamana wa mjini Brussels wanavyo tapa tapa kujaribu kutoa tafsiri nyengine ya kura ya maoni ya Ufaransa na Uholanzi, ni jaza kwa wenye kuushuku umoja wa Ulaya.“

Gazeti la mjini Karlsruhe, "Badische Neueste Nachrichten" linauangalia uamuzi wa Uengereza kuwa ni sawa na „ukombozi“. Gazeti linaandika:

„Kwa kuikataa kistaarabu, Blair amefanikiwa katika nyanja mbili kwa wakati mmoja: siasa ya nje na siasa ya ndani pia. Ametambua kutokana na hali namna ilivyo hivi sasa, kura ya maoni ya katiba isingepita. Kisiwani uchumi unanawiri, nchini Ujerumani na Ufaransa injini ya kiuchumi ina lega lega - na hilo tuu ndio muhimu.

Kinyume na hayo, gazeti la mjini Erfurt,"Thüringer Allgemeine" linakosoa kile wakiitacho "uzembe" wa waziri mkuu Blair. Gazeti linaandika:

„Tony Blair amekwepa. Na wakati ulikua muwafak. Ingawa waziri mkuu wa Uengereza, sawa na viongozi wengine wa taifa na serikali za Umoja wa Ulaya, ameahidi kutia njia utaratibu wa kuidhinisha katiba ya Umoja wa Ulaya, lakini „la“ ya Ufaransa na Uholanzi imezusha kizungumkuti. Rais Jacques Chirac amedhoofika vibaya sana kuweza kupasa sauti kupigania masuilahi ya ulaya. Kansela Gerhard Schröder anajikuta na mguu mmoja ndani na mmoja nje. Na sasa hasa ndio anawatia munda wenzake, ingawa kura ya maoni ilikua iitishwe mwaka mmoja kutoka sasa."

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW