1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri wasifu uhusiano baina ya Ujerumani na Poland

Abdu Said Mtullya22 Juni 2011

Wahariri wa magazeti wasema uhusiano baina ya Ujerumani na Poland umeendelea kuwa mzuri

Kansela Angela Merkel na Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk.Picha: DW

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumia juu ya uhusiano baina ya Ujerumani na Poland kufuatia ziara ya Kansela Merkel nchini Poland. Pia wanazungumzia juu ya matatizo ya Ugiriki.

Mhariri wa gazeti la Märkische Oderzeitung anasema uhusiano baina ya Ujerumani na Poland ni mzuri. Mhariri huyo anatilia maanani mpango wa ushirikiano uliofikiwa baina ya nchi mbili hizo unaozima moto wa kiongozi wa upinzani Jaroslaw Kaczynski ambae ni mpinzani mkubwa wa Ujerumani.

Mhariri huyo anasema uhusiano wa kiuchumi baina ya Poland na Ujerumani pia ni mzuri, hata hivyo anasema watu wanasubiri kuona mpango wa ushirikiano uliofikiwa baina ya nchi mbili hizo ukitekelezwa.

Mhariri wa gazeti la Landeszeitung pia anasifu uhusiano mzuri uliopo baina ya Ujerumani na Poland na anasema ni jambo la kufurahisha kuona jinsi uhusiano huo ulivyoendelea kuwa mzuri, hasa mtu akitambua kwamba nchi mbili hizo zilipambana katika vita kuu vya pili. Anaeleza kuwa uhusiano huo mzuri unatokana na juhudi za Waziri Mkuu wa sasa nchini Poland bwana Donald Tusk.

Itakumbukwa, anasema mhariri huyo kwamba ,aliekuwa kiongozi wa Poland miaka sita iliyopita, Lech Kaczynski na nduguye Jaroslaw walikuwa wanatoa kauli za kiadui dhidi ya Ujerumani na nchi nyingine za Umoja wa Ulaya.

Mhariri wa Nordwest Zeitung anasema ziara ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel nchini Poland imewasilisha ujumbe mmoja ulio wazi kabisa: "Kwamba viongozi wa nchi hizo wanaangaza macho yao katika mustakabal wa nchi zao."

Mhariri huyo anaeleza kwamba kutokana na sera za Waziri Mkuu wa Poland Bwana Tusk , zinazoenzi ujirani mwema na Ujerumani, nchi mbili hizo sasa zimesogeleana karibu kwa hatua zisizokuwa na mithili katika historia ya hivi karibuni ya nchi zao. Gazeti limetilia maanani kwamba mkutano wa kilele wa viongozi wa Ujerumani na Poland na makubaliano yaliyofikiwa yanaashiria dhamira ya kuendeleza maslahi ya kiuchumi baina yao barani Ulaya.

Gazeti la Der neue Tag linatoa maoni juu ya mgogoro wa Ugiriki na linawataka viongozi wa Ufaransa na Ujerumani watoe kauli za ukweli. Linasema pana haja kwa Umoja wa Ulaya,Ufaransa na Ujerumani kutamka kweli kwamba, Umoja wa Ulaya ni chombo cha kuhamishia fedha baina ya nchi wanachama.

Jambo la pili ,inapasa kusema kweli kwamba ikiwa Ugiriki itafilisika,Umoja wa sarafu ya Euro utasambaratika!

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri/-Abdul-Rahman