1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Wahariri watano watiwa mbaroni Hong Kong

Josephat Charo
17 Juni 2021

Polisi ya Hong Kong iliwatia mbaroni mhariri mkuu na viongozi wanne wa vyeo vya juu wa gazeti linalounga mkono demokrasia la Apple Daily baada ya kukivamai chumba cha habari cha gazeti hilo kwa mara ya pili

Hongkong | Festnahme von Apple Daily Mitarbeiter durch Sicherheitsgesetz
Picha: Vernon Yuen/NurPhoto/picture alliance

Zaidi ya maafisa 500 walifanya operesheni alfajiri ya leo ambayo maafisa wanasema ilisababishwa na makala zilizochapishwa na gazeti la Apple Daily kutoa mwito viongozi wa Hong Kong na China wawekewe vikwazo.

Msemaji wa jeshi la polisi, Steve Li, alisema wahariri wa gazeti la Apple Daily wana dhamana kwa maudhui, mtindo na kanuni za kuripoti habari. Na kwa hivyo waliwakamata wahariri hao watano kwa kuuhatarisha usalama wa taifa.

"Katika operesheni hii tumewakamata wanaume wanne na mwanamke mmoja wenye umri wa miaka 74 na 63 mtawalia. Wote ni wakurugenzi wa kampuni yenye mafungamano na gazeti la Apple Daily. Kosa lao ni kula njama na mataifa ya kigeni na taasisi za nje na kuhatarisha usalama wa taifa."

Maafisa walizikamata mali za gazeti la Apple Daily zenye thamani ya dola milioni 2.3 za kimarekani, ikiwa ni mara ya kwanza sheria ya usalama wa taifa ya kukamata mali inatumiwa moja kwa moja dhidi ya kampuni ya vyombo vya habari, mbali na mtu binafsi.

Ryan Law, wa pili kutoka kulia, Mhariri Mkuu wa gazeti la Apple Daily, akikamatwa na maafisa wa polisi Hong Kong Alhamisi (Juni 17, 2021)Picha: AP Photo/picture alliance

Hii ni mara ya kwanza kwamba maudhui ya ripoti za vyombo vya habari yamesababisha watu kutiwa ndani chini ya sheria mpya ya usalama wa taifa mjini humo. Katika ujumbe wake kwa wasomaji, gazeti la Apple Daily lilionya kuwa uhuru wa vyombo vya habari Hong Kong unaning'inia kwenye kamba nyembamba, lakini gazeti hilo limeapa kujiweka kifua mbele kuutetea.

Ukamataji wa wahariri wakosolewa vikali

Chama cha magazeti kiliileza operesheni hiyo kama ukiukaji mkubwa wa uhuru wa vyombo vya habari usio mithili uliodhihirisha wazi dhahiri shahiri ni kwa jinsi gani nguvu ya polisi ilivyoongezeka na kuwa kubwa zaidi chini ya sheria mpya ya usalama wa taifa.

Akijibu tuhuma hizo, waziri wa habari wa Hong Kong John Lee alisema hawaulengi uhuru wa vyombo vya habari wala kazi ya uandishi habari, bali wanawalenga wageni wanaotumia kazi ya uandishi kama chombo cha kuuhatarisha usalama wa taifa. Hata hivyo alikataa kutaja ni makala zipi zilizokiuka sheria ya usalama wa taifa wala ikiwa wale waliosambaza mtandaoni, walionunua gazeti la Daily Apple au hisa zake, huenda nao wakawa hatarini.

Sharron Fast, mhadhiri wa chuo kikuu cha uandishi habari cha Hong Kong aliyaeleza matamshi ya waziri Lee kuwa sio sahihi na ni uongo mtupu.

Gazeti la Apple Daily na mmiliki wake anayetumikia kifungo gerezani Jimmy Lai kwa muda mrefu limekuwa mwiba kwa serikali ya mjini Beijing likichukua msimamo wa kutoomba msamaha wa kuunga mkono vuguvugu la kupigania demokrasia katika kisiwa cha Hong Kong na kuwakosoa vikali viongozi wa kiimla wa China.

(afp)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW