Wahispania waafiki katiba ya Ulaya
21 Februari 2005Madrid:
Hispania imekuwa nchi ya kwanza ya Umoja wa Ulaya kuikubali katiba mpya ya Umoja huo katika kura ya maoni iliyopigwa jana. Maafisa wa Hispania na Umoja wa Ulaya wanatumaini kuwa nchi nyingine zitafuata nyayo. Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani zinaonyesha kuwa Wahispania wengi wamepiga kura ya "Ndiyo". Wapigaji kura wanne kati ya watano wameafiki katiba hiyo. Wenye haki ya kupiga kura zaidi ya asili mia 42 wamepiga kura. Waziri Mkuu wa Hispania, Jose Luis Rodriquez Zapatero, amesema kuwa kura yao ni ujumbe murua kwa raia wengine wa Ulaya waliokuwa wanasubiri uamuzi wao. Ameongeza kusema kuwa leo Ulaya imeshinda, katiba ya Ulaya imeshinda na Hispania nayo imeshinda. Anatumaini kuwa nchi jirani za Ulaya zitafuata mfano wa Hispania.