1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahispania waandamana, mawaziri wa euro wakutana

20 Julai 2012

Watu kadhaa wamekamatwa na wengine kujeruhiwa mjini Madrid, ambako waandamanaji wanapinga hatua za kubana matumizi, huku mawaziri wa fedha wa kanda ya euro wakitarajiwa kupitisha mpango wa uokozi kwa nchi hiyo.

Waandamanaji mjini Madrid, Hispania.
Waandamanaji mjini Madrid, Hispania.Picha: Reuters

Polisi ya nchi hiyo inasema kwamba watu 15 wamekamatwa na wengine 35 wamejeruhiwa baada ya polisi kuwarushia waandamanaji risasi za mpira kuwatawanya walipokuwa wakizunguka jengo la bunge. Msemaji wa polisi amesema hivi leo kwamba polisi 10 ni miongoni mwa majeruhi.

Maandamano ya jana katika mji mkuu, Madrid, yalikuwa moja kati ya matukio 80 ya aina hiyo yaliyofanyika kwenye miji kadhaa nchini Uhispania kupinga hatua za kubana matumizi ambazo serikali ya kihafidhina inazichukua, ikidai kwamba ni muhimu kuiepusha nchi hiyo na hatima kama za Ugiriki, Ireland na Ureno.

Mawaziri wa fedha wakutana

Wakati hayo yakiarifiwa, mawaziri wa fedha kutoka mataifa 17 wanachama wa kanda ya euro wanatarajiwa leo kuthibitisha masharti ya mkopo kwa benki za Uhispania. Miongoni mwa masharti yaliyomo kwenye hati ambayo mawaziri hao wataijadili kupitia mkutano wa njia ya simu, ni lile la kuwapo kwa uangalizi madhubuti kwa benki zitakazopokea mkopo huo.

Mkuu wa Kanda ya Euro, Jean-Claude Juncker (kushoto) na Waziri wa Fedha wa Finland, Jutta Urpilainen.Picha: Reuters

Pia hati hiyo inataka hadi mwishoni mwa mwezi huu serikali ya Uhispania iwe imeshawasilisha mipango yake ya kupunguza nakisi ya bajeti hadi chini ya asilimia 3 ya pato jumla la nchi hiyo kufikia mwaka 2014.

Mawaziri hao wa fedha wamekubali kuikopesha Uhispania hadi euro bilioni 100 na maamuzi ya leo yanaweza kuruhusu kuanza kutolewa euro bilioni 30 za awali. Hata hivyo, kiwango hasa cha fedha zinazohitajika kuzifufua benki za Hispania kitajuilikana mwezi Septemba baada ya kila benki kuhakikiwa upya.

Ujerumani, Finland zakubali kuisaidia Uhispania

Mapema leo bunge la Finnland limepitisha mpango wa kuisaidia Uhispania, ambapo sehemu ya nchi hiyo katika kiwango cha euro bilioni 100 itafiia hadi euro bilioni 1.9. Bunge la Ujerumani lilipitisha hatua hiyo hapo jana.

Waziri wa Fedha wa Ujerumani, Wolfgang Schäuble.Picha: dapd

"Sababu ni kuwa hatua zilizochukuliwa na Uhispania za mageuzi ya kimsingi ni sahihi na muhimu. Kama ilivyo kwa mataifa mengine, kwa Uhispania pia bado ipo katikati ya mageuzi haya, lakini bado hayajakamilika. Na mageuzi haya yanaweza tu kufanya kazi vyema ikiwa matatizo kwenye sekta nyengine yanatatuliwa." Amesema waziri wa fedha wa Ujerumani, Wolfgang Schäuble, akieleza sababu za Ujerumani kukubali kuisaidia Uhispania.

Serikali ya Uhispania ililazimika kupitisha hatua kali za kubana matumizi na kukata mafao, mishahara na malipo ya uzeeni kwa lengo la kupunguza deni lake na kuimarisha imani ya taasisi zake za kifedha.

Hatua hizo, hata hivyo, zimeongeza ugumu wa maisha kwa Wahispania wengi ambao tayari walishakuwa katika hali ngumu kutokana na ukosefu wa ajira, na kufeli kwa sekta ya benki.

Mabenki katika nchi hizo yamezama kwenye dimbwi la hasara baada ya kushindwa kwa uwekezaji kwenye nyumba, huku serikali ya nchi hiyo ikishindwa kuziokoa na kuzusha wasiwasi kwamba huenda nayo Uhispania ikahitajia kupatiwa msaada wa uokozi kama mataifa mengine ya kanda ya sarafu ya euro.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Othman Miraji

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW