Wahispania wajitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa Jumapili
23 Julai 2023Idadi ya kura zilizopigwa katika uchaguzi unaofuatiliwa kwa karibu nchini Uhispania, inaashiria mwitikio mkubwa wa wapiga kura licha ya joto kali. Takribani asilimia 40.5 ya wapiga kura walikuwa tayari wameshiriki zoezi hilo kufikia majira ya mchana. Takwimu hizo hazijumuishi kura zilizopigwa kwa njia ya posta zinazofikia milioni 2.5.
Serikali ya mrengo wa kushoto ya Waziri Mkuu Pedro Sánchez iko hatarini kupoteza wingi wake katika uchaguzi wa Jumapili. Kura za maoni zinapendekeza kuwa, chama cha kihafidhina cha People's Party (PP) huenda kikatoa mshindi na kinaweza kuunda serikali ya muungano na chama kingine cha mrengo wa kulia.
Uchaguzi wa Jumapili unaangukia katikati ya msimu wa likizo kuu nchini Uhispania, na wapiga kura wengi walisema kwamba wamepiga kura kura zao mapema ili kuepuka joto kali la mchana.