Wahouthi kuwaondoa wanajeshi kutoka bandari za Yemen
11 Mei 2019Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya mkuu wa kamati ya Umoja wa Mataifa inayosimamia mpango huo, Jenerali Michael Lollesgaard. Jenerali huyo Mholanzi amesema anaukaribisha uamuzi huo wa waasi hao wa kishia wanaoungwa mkono na Iran wa kujiondoa katika bandari muhimu za Hodeida, Saleef na Ras Issa.
Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Wahouthi nchini Yemen, Mohammed Ali al-Houthi amesema kwenye ujumbe wa mtandao wa Twitter kuwa hatua hiyo ya upande mmoja ya wahouthi kukubali kuwaondoa wanajeshi wao kutoka bandari tatu muhimu ilitokana na hatua ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia kukataa kuyatekeleza makubaliano ya Stockholm ambayo yaliweka msingi wa mchakato wa kupatikana amani.
Muungano wa kijeshi wa Waislamu wa madhehebu ya Sunni ukiongozwa na Saudi Arabia uliingilia kati nchini Yemen Machi 2015 katika hatua ya kupambana na waasi wa Houthi na kumrejesha madarakani Rais Abed Rabbo Mansour Hadi. Kwa mujibu wa wajumbe wa Umoja wa Mataifa, waasi wa Houthi walikuwa wamekataa kuondoka katika bandari hizo kwa sababu walihofia kuwa muungano huo wa kijeshi ungekamata udhibiti wa bandari hizo.
Serikali ya Yemen inayoungwa mkono na Saudia haijasema kama upande wake utachukua uamuzi kama wa Wahouthi. Pia wanatarajiwa kuondoka katika ngome za karibu na viunga vya mji wa Hodeidah katika awamu ya kwanza kabla ya awamu ya pili ambapo pande zote mbili zitahitajika kusonga nyuma zaidi.
Waziri wa habari wa Yemen Moammar al-Eryani alikosoa pendekezo la Houthi kuondoka Hodeidah, akiliita "linalopotosha" na lisilokubalika kama halitarihusu "ufatiliaji wa pamoja na ukaguzi" kama inavyohitajika kwenye mkataba wa Desemba.
Muungano huo wa kijeshi unaoongozwa na Saudi unadai kuwa waasi hao wanazitumia bandari hizo kuingiza silaha kwa njia ya magendo, wakati nao waasi wakisema wangeishiwa na bidhaa muhimu kama mungano huo ungechukua udhibiti wa bandari hizo.
Mataifa ya Magharibi, ambayo baadhi yao yanaupa silaha muungano huo pamoja na taarifa za kijasusi, yanashinikiza kumalizika kwa mgogoro huo, unaoonekana katika kanda hiyo kuwa vita vya wakala kati ya Saudi Arabia na Iran.