1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahouthi, serikali ya Yemen mazungumzoni Sweden

5 Desemba 2018

Wawakilishi wa serikali ya Yemen inayoungwa mkono na Saudi Arabia wameelekea Sweden, ambako tayari ujumbe wa waasi wa Kihouthi ulishawasili mazungumzo ya kusaka amani yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa.

Shiiten Jemen Houthis
Picha: picture-alliance/AP Photo/H.Mohammed

Ujumbe wa serikali ya Yemen uliondoka mjinji Riyadh, Saudi Arabia, mapema leo Jumatano, huku chanzo kimoja ndani ya serikali hiyo kikiliambia shirika la habari la Ujerumani, dpa, kwamba wanatazamiwa kuwasili mjini Stockholm jioni.

Tayari ujumbe wa Wahouthi ulishawasili nchini Sweden tangu jana Jumanne, wakisindikizwa na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen, Martin Griffiths. 

Juhudi za awali za mjumbe huyo kuitisha mazungumzo kama haya mjini Geneva, Uswisi, zilishindikana mwezi Septemba pale wajumbe wa Kihouthi waliposhindwa kutokea. 

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasema hatazamii hatua za haraka kueleleka muafaka wa kisiasa, lakini watategemea kutakuwa japo na hatua ndogo ndogo zitakazosaidia kulishughulikia tatizo la hali mbaya ya kimaisha inayowakabili sasa Wayemen.

Hata hivyo, pande zote mbili, ule wa serikali inayotambuliwa kimataifa na kuungwa mkono na Saudia na Marekani na ule wa Wahouthi unaoungwa mkono na Iran, zinasema kuwa zinataka amani.

Mjumbe mmoja wa serikali kwenye mazungumzo hayo ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wana matumaini kuwa mazungumzo haya yatafanikiwa kwa kuwa Wahouthi wameonesha kuwa makini zaidi mara hii.

Ajenda za Stockholm

Abd Rabbo Mansour Hadi, rais wa Yemen anayetambuliwa na jumuiya ya kimataifa na kuungwa mkono na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia.Picha: picture-alliance/dpa/AP Photo//Yemen's Defense Ministry

Mazungumzo haya ya Sweden yanategemewa kujielekeza kwenye ujengaji wa imani kati ya pande mbili, kuufungua uwanja wa ndege wa Sana'a, kuuondoa mzingiro wa kijeshi uliowekwa na Wahouthji kwenye mji wa kusini magharibi wa Taiz na kumalizia makubaliano ya kubadilishana wafungwa yaliyosainiwa na pande hizo mbili. 

"Mambo yote yanaweza kuzungumzwa. Hatujajibana kwenye masuala maalum. Hata hivyo, ili kujenga imani baina yetu, kutakuwa na nyaraka nyingi - nyaraka kuhusu mateka, uchumi, misaada ya kiutu - ili kujenga imani kwa ajili ya mazungumzo ya amani, na ili kutoa suluhisho la pamoja kwa mzozo wa Yemen," alisema mwakilishi wa Wahouthi kwenye mazungumzo hayo, Ghaleb Mutlaq.

Kwa upande mwengine, Rais Abd-Rabb Mansour Hadi atatakiwa naye kutoa fedha za serikali zinazohifadhiwa nje ya nchi kwa ajili ya kuwalipa wafanyakazi wa serikali wanaofanya kazi kwenye maeneo yanayodhibitiwa na waasi.

Mgogoro wa Yemen ulianza baada ya Wahouthi kuuchukuwa mji mkuu, Sana'a, na sehemu kubwa ya eneo la kaskazini mwa nchi mwaka 2014. Mwezi Machi mwaka huu, muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia ukisaidiwa na Marekani ulijiingiza kwenye vita hivyo kuusaidia upande wa serikali.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga