1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi Wahouthi waapa kulipiza kisasi shambulizi la Israel

22 Julai 2024

Waasi wa Houthi wameahidi kile walichokiita hatua kubwa ya kulipiza kisasi dhidi ya shambulizi kali la Israel kwenye bandari ya Hodeida. Hii ni wakati msuguano wa kikanda ukiendelea kutanuka kutokana na vita vya Gaza.

Wapiganaji wa Kihuthi
Wapiganaji wa KihuthiPicha: Khaled Abdullah/REUTERS

Shambulizi la Israel nchini Yemen, lilisababisha moto kwenye tanki za mafuta katika bandari hiyo muhimu na lilijiri siku moja baada ya shambulizi baya kabisa lililofanywa na Wahouthi nchini Israel.

Jana Jumapili, Israel ililiharibu kombora lililorushwa kutokea Yemen na kuyashambulia maeneo ya kusini mwa Lebanon. Wakaazi wa kusini mwa Gaza waliripoti kutokea kwa mapigano katika eneo la Rafah. 

Msemaji wa kijeshi wa Wahouthi Yahya Saree alisema jibu la waasi hao kwa uchokozi wa Israel dhidi ya nchi yao haliepukiki na litakuwa kubwa zaidi.

Soma pia:Israel yaendelea kuvurumisha mashambulizi ya ardhini Gaza

Mapigano hayo ya kikanda yanajiri wakati Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu akielekea Washington wiki hii, ambayo imekuwa ikijaribu kutafuta makubaliano ya kusitishwa mapigano katika vita hivyo vilivyodumu kwa miezi tisa kati ya Israel na wanamgambo wa Kipalestina Hamas huko Gaza.