1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaYemen

Wahouthi waelekea Saudi Arabia kwa mazungumzo ya amani Yemen

15 Septemba 2023

Waasi wa Kihouthi nchini Yemen wanaoungwa mkono na Iran, wamesema wanatumai kutatua changamoto ziliopo, wakati wakielekea Saudi Arabia kushiriki mazungumzo yanayonuiwa kumaliza vita vilivyodumu miaka minane Yemen.

Moshi ukionekana katika moja ya majengo yaliyoshambuliwa mjini sanaa
Moshi ukionekana katika moja ya majengo yaliyoshambuliwa mjini sanaa Picha: Hani Al-Ansi/dpa/picture alliance

Ujumbe wa waasi hao wa kihouthi wenye uhusiano wa Karibu na Iran ambayo ni hasimu wa muda mrefu wa Saudi Arabia, uliondoka jana jioni kwa ziara yao ya kwanza ya wazi tangu muungano unaoongozwa na Saudi Arabia, ulipoiingilia kijeshi Yemen mwaka 2015.

Mapigano nchini Yemen yalitulia kwa kiasi kikubwa baada ya usitishaji mapigano uliosimamiwa na Umoja wa Mataifa

Ziara ya waasi hao ni ishara ya matumaini ya hivi karibuni ya kusitisha mapigano yaliyosababaisha mgogoro mkubwa na mbaya wa kibinaadamu nchini humo.

Kiongozi wa juu wa kisiasa wa kundi hilo  Mohamed Ali al-Huthi aliandika katika mtandao wa X uliokuwa Twitter zamani, kwamba anatumai kutakuwa na majadiliano muhimu kwa manufaa ya watu wote na kwamba changamoto zilizopo zitatatuliwa. Amesema mazungumzo yanaweza tu kufanyika chini ya muungano huo akitilia maanani kwamba uamuzi wa mzingiro na kuusimamisha uko mikononi mwa muungano huo.

Waasi wa Huthi wanaoungwa mkono la Iran kwenda Saudi Arabia

Kipengee muhimu cha kupunguza uhasama ni kurejea kwa mahusiano mazuri kwa Saudi Arabia na Iran waliokuwa maadui wa muda mrefu.

Marekani yapongeza juhudi za kutafuta amani ya Yemen

Rais wa Marekani Joe Biden Picha: Celal Gunes/AA/picture alliance

Marekani mshirika wa Saudi Arabia imepongeza  ziara ya Wahouthi ikisema kusitisha vita vya Yemen ni moja ya vipaumbele vya sera ya kigeni ya rais Joe Biden. Mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani Jake Sullivan amesema nchi yake imetoa mwito kwa pande zote husika katika vita hivyo, kuangalia mafanikio ya kusitisha mapigano kwa watu wa Yemen.

Televishani ya kitaifa ya Saudi Arabia imesema mazungumzo ya sasa yanalenga kupata suluhu ya kudumu ya mkwamo wa kisiasa yemen yatakayoioandoa nchi hiyo kutoka hali ya mgogoro had uthabiti wa kweli.

Yemen: Baraza jipya la Aden na hatari ya mzozo na wanaoungwa mkono na UAE

Miongoni mwa matakwa ya wahouthi ni wafanyakazi wa umma kulipwa mishahara yao na serikali ya Yemeni na kuanzishwa kwa safari nyengine za ndege katika maeneo mapya kutoka uwanja wa ndegee wa sanaa.

Yemen iliingia katika mgogoro wakati waasi wa Houthi walipoudhibiti mji mkuu Sanaa mwezi September mwaka 2014 na kuiondoa madarakani serikali iliyokuwa inatambuliwa kimataifa, hali iliyosababisha Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia kuanzisha operesheni ya kijeshi mwezi Machi mwaka 2015.

Mapigano ya Yemen yamesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kuwalazimisha wengine kuyahama makaazi yao ikiacha thuluthi tatu ya idadi ya watu wakitegemea misaada ya kiutu.

afp/ap