1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Amnesty: Wahusika wa vita DRC wamekiuka sheria ya vita

Angela Mdungu
20 Januari 2025

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema pande zinazohusika na vita kati ya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na waasi wa M23, huenda zimekiuka sheria za vita.

Vita Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Baadhi ya wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakilinda doria Jamhuri ya Kidemokrasi ya KongoPicha: Wang Guansen/Xinhua/picture alliance

 Amnesty International limesema uwezekano huo unatokana na pande hizo hasimu kuyashambulia maeneo yenye msongamano mkubwa wa raia.

Taarifa ya Amnesty International iliyotolewa leo Jumatatu imeeleza kwamba, zaidi ya raia 100 waliuwawa Mashariki mwa Jamhuri  ya Kidemokrasia ya Kongo katika nusu ya kwanza ya mwaka 2024. Mauaji hayo ni matokeo ya mashambulizi  ya roketi bila ya kuchagua maeneo yanayolengwa na hivyo kusababisha madhara ya jumla ikiwemo kwenye maeneo ya raia wa kawaida. Kulingana na ripoti hiyo, Jeshi la Kongo pamoja na waasi wa M23 wanahusika na ongezeko la matumizi ya silaha zisizokidhi viwango vinavyokubalika katika sheria ya vita.

Ripoti hiyo imesema, tangu kundi la M23 linalodai kuwalinda watu wa jamii ya Kitutsi lilipoibuka tena mwishoni mwa mwaka 2021 likisaidiwa na wapiganaji 3,000 hadi 4,000 wa Rwanda, limefanikiwa kuyateka maeneo mengi ya Mashariki mwa Kongo yenye utajiri wa  madini na kusababisha mgogoro wa kiutu na maelfu ya watu wameyakimbia makazi yao.

Huku likiapa kuyakomboa maeneo yake yaliyonyakuliwa na wanamgambo hao, jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo limefanya mashambulizi ya kulipa kisasi, likisaidiana na wanamgambo wanaoiunga mkono serikali ya Kinshasa.

Katika mapambano kati ya mwezi Januari na Julai mwaka uliopita, mabomu yenye madhara kwa eneo kubwa yalitumiwa zaidi ya mara 150 katika maeneo yenye msongamano wa watu wengi kwa mujibu wa ripoti ya Amnesty international.

Mashambulizi ya jeshi la Kongo na waasi huenda yakawa uhalifu wa kivita

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limeongeza kuwa mashambulizi hayo yaliyowauwa zaidi ya raia 100 na kuwajeruhi mamia wengine yalikiuka sheria ya kimataifa ya kiutu na kuna uwezekano kuwa yalikuwa uhalifu wa kivita.

Amnesty limesema kwamba mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC inapasa kuyachunguza mashambulizi hayo kama uhalifu wa kivita kwa madhumuni ya kuwafikisha mbele ya sheria wote wanaotuhumiwa kuhusika.

Wakimbizi waliolazimika kuyahama makazi yao Goma kutokana na vita wakiwasili Minova Kusini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya KongoPicha: ALEXIS HUGUET/AFP

Soma zaidi: M23 wachukua udhibiti wa maeneo ya uchimbaji madini Kongo

Ripoti ya shirika hilo hata hivyo imeeleza kwamba mamlaka za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimeonesha kuwa haziko tayari kutoa ushirikiano. Itakumbukwa kuwa mwaka 2024, mahakama ya ICC ilisema kuwa inaanzisha uchunguzi katika mzozo huo.

Akitoa wito kwa pande hizo mbili za mzozo, Katibu Mkuu wa Amnesty International Agnes Callamard amesema zinapaswa kuacha kuwashambulia raia mara moja.

Katika wiki za hivi karibuni, mapambano nchini humo yamekuwa yakiongezeka licha ya juhudi za kusimamisha mapigano zinazoongozwa na Angola. Jumamosi jioni, waasi wa M23 walipata mafanikio mapya baada ya kufanikiwa kuidhibiti miji miwili ya Lumbishi na Kivu Kusini ambako kuna machimbo ya madini.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW