1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waingereza wengi wataka kubakia EU

17 Desemba 2017

Uchunguzi uliofanyika hivi karibuni Uingereza kuhusu  Brexit waonesha waingereza wengi wanataka kubakia Umoja wa Ulaya badala ya kujitenga na umoja huo. Utafiti wa maoni uliofanywa na shirika la BMG ulihusisha watu 1509

Anti Brexit 
London Houses of Parliament Anti Brexit Protest
Picha: Reuters/P. Nichols

Wakati waziri mkuu Thereza May akiingia katika duru ya pili ya mazungumzo kuhusu nchi yake kujiondowa kwenye Umoja wa Ulaya au kile kinachoitwa Brexit ,uchunguzi wa maoni ulioitishwa na gazeti la kila siku la nchini Uingereza la Independent unaonesha kwamba zaidi ya nusu ya Waingereza wanataka kubakia sehemu ya Umoja wa Ulaya. Uchunguzi uliondeshwa na shirika la utafiti la BMG kwaniaba ya gazeti hilo la Independent  unaonesha kwamba asilimia 10 zaidi ya waingereza wanataka nchi yao ibakie ndani ya Umoja wa Ulaya.

Shirika la utafiti la BMG limewahoji watu 1,509 kuanzia tarehe 5 hadi 8 wanaoishi Uingereza  na kuwauliza je nchi hiyo ibakie kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya au ijiondoe kabisa katika Umoja huo? Wale waliojibu suali hilo asilimia 51 walisema wanaunga mkono kuendelea kubakia ndani ya Umoja wa Ulaya wakati asilimia 41 ya waliojibu waliunga mkono kujiondoa na asilimia 7 ya waliohojiwa walisema hawajui upande gani wa kuunga mkono ingawa baada ya kushinikizwa wajibu au waondolewe kuwa sehemu ya matokeo ya utafiti huo,ilibainika kwamba asilimia 55.5 waliunga mkono kubakia Umoja wa Ulaya na idadi ya waliounga mkono kujitowa ikafikia asilimia 44.5.

Picha: Reuters/B. Tessier

Gazeti la Independent linadai kwamba tafauti hiyo mitazamo imeongezeka kwa kiwango kikubwa tangu ulipofanyika mchakato wa kura ya maoni. Michel Turner mkuu wa uchunguzi  wa maoni ya wananchi katika shirika la utafiti la BMG  ameliambia  gazeti la Independent kwamba mara ya mwisho maoni ya waliotaka nchi hiyo ijitenge kuongoza dhidi ya wale waliotaka nchi hiyo ibakie Umoja wa Ulaya ilikuwa ni mwezi Februari mwaka 2017 na tangu wakati huo kumekuwa na mtazamo tafauti miongoni mwa maoni ya raia ambapo wengi wameonekana kubadili mkondo na kuunga mkono nchi hiyo ibakie ndani ya Umoja wa Ulaya.

Hata hivyo watu wanapaswa kufahamu kwamba unapochimba ndani kabisa ya utafiti huu inaonesha kwamba mabadiliko haya ya mtazamo yanatolewa zaidi na wale ambao kwa hakika hawakushiriki katika mchakato wa kupiga kura ya maoni kuhusu Brexit mnamo mwaka 2016 huku ikitajwa kwamba kiasi watu 9 kati ya 10  waliopiga kura hiyo ya Ndio au Hapana bado mitazamo yao haijabadilika. Ikumbukwe kwamba Juni 2016 kura ya maoni nchini Uingereza kuhusu kujitenga na Umoja wa Ulaya, asilimia 52 ya wapiga kura waliunga mkono kujiondoa kwenye Umoja huo wakati asilimia 48 walipiga kura kubakia na idadi ya waliojitokeza katika kura hiyo ilikuwa ni asilimia 72.2.

Picha: picture alliance/AP Photo/V. Mayo

Kwa hivyo Turner ameongeza kusema kwamba kwa mujibu wa utafiti wao wa maoni umeonesha kiasi mwaka mmoja nyuma wale walioshindwa kwenda kupiga kura ya maoni walikuwa wamegawika lakini utafiti huu unaonesha kwamba sasa walio wengi kati ya kundi hilo wanaunga mkono kubakia katika Umoja wa Ulaya.

Uingereza inapanga kuachana kabisa na Umoja wa Ulaya mwezi Marchi mwaka 2019.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Source:DW

Mhariri:John Juma

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW