Wairan wakumbuka mwaka mmoja tangu kifo cha Mahsa Amini
16 Septemba 2023Kumbukumbu hiyo imefanyika wakati wanaharakati wakidai kuwa kuna msako mpya wa kuzuia kuibuka tena kwa maandamano ambayo yaliitikisa miji mikubwa nchini Iran mwaka 2022.
Amini, msichana wa jamii ya Wakurdi aliyekuwa na miaka 22, alikufa siku chache baada ya kukamatwa na polisi wa maadili kwa tuhuma za kuvaa mavazi yanayokiuka maadili ya mavazi kwa wanawake ambayo yanazingatiwa tangu baada ya mapinduzi ya kiislamu ya Iran ya mwaka 1979.
Familia yake inasema, Mahsa Amini alikufa baada ya kupigwa na kitu kizito kichwani, ingawa mamlaka za Iran zimekanusha. Hasira kuhusu kifo chake ilisambaa kwa kasi na kugeuka kuwa maandamano yaliyovunja mwiko, ambapo wanawake walishuhudiwa wakivua hijabu hadharani na kutoa changamoto kwa serikali ya Iran inayofuata mfumo wa dini ya Kiislamu chini ya kiongozi wa juu wa kidini Ayatollah Ali Khamenei.
Soma zaidi: Polisi Iran yafyatua risasi, dhidi ya waombolezaji wa Amini
Miezi kadhaa baadaye maandamano hayo yalipunPolisi Iran yafyatua risasi, dhidi ya waombolezaji wa Aminigua nguvu na hatua kali zilianza kuchukuliwa ambapo kwa mujibu wa Shirika la Kutetea Haki za Binadamu lenye makao yake Iran, IHR, linasema kuwa vikosi vya usalama viliwaua watu 551.
Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch nalo liliripoti kuwa takriban watu 22,000 walikamatwa. Mamlaka nchini humo zinasema kuwa maafisa kadhaa wa usalama waliuwawa katika kile walichokiita "machafuko" yaliyochochewa na serikali za kigeni na vyombo vya habari vyenye nia ovu.
Limeongeza pia kuwa wanafamilia takribani 36 wa watu waliouwawa au walionyongwa walihojiwa, kukamatwa, kushtakiwa au waliwekwa korokoroni mwezi mmoja uliopita
Wanaume saba wameshanyongwa baada ya kuhukumiwa katika kesi zinazohusiana na maandamano hayo.
Soma zaidi: Iran yawanyonga watatu kwa mauaji ya polisi
Waandishi habari wawili waliofanya kazi kubwa kuiweka hadharani kesi ya Amini, Niloufar Hamedi na Elahe Mohammadi wako jela kwa takriban mwaka mmoja. Waandishi hao waliripoti tangu msichana huyo alipokuwa hospitali hadi wakati wa mazishi yake.
Baba wa Mahsa Amini akamatwa kwa muda na kuachiliwa huru
Katika hatua nyingine, makundi ya kutetea haki za binadamu yameripoti kuwa, baba wa Mahsa Amini, Amjad Amini, alikamatwa kwa muda mapema leo Jumamosi huku kukiwa na ulinzi mkali wa vikosi vya polisi.
Mtandao wa haki za binadamu wa jamii ya Wakurdi umesema kuwa Amini alitahadharishwa asifanye kumbukumbu ya kifo cha mwanaye. Baada ya muda mchache aliachiwa huru. Shirika la habari la Iran, IRNA lilikanusha taarifa za kukamatwa kwake. Mapema leo mitandao ya kijamii na ripoti za makundi ya haki za binadamu yalisema kuwa kulikuwa na ulinzi mkali kuzunguka nyumbani kwa Amin huko Saqez magharibi mwa Iran.
Kulingana na machapisho katika mitandao ya kijamii, wazazi wa Amini walisema katika taarifa yao mapema wiki hii kuwa, licha ya serikali kutoa tahadhari, wangefanya kumbukumbu ya kiutamaduni katika kaburi la binti yao.