1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wairaq waendeleza maandamano mjini Baghdad na Nassiriya

Sylvia Mwehozi
30 Novemba 2019

Raia nchini Iraq wameendelea na maandamano kwenye mji mkuu Baghdad na eneo la kusini ya nchi hiyo ikiwa ni ishara ya kutoridhishwa na mipango ya kujiuzulu waziri mkuu na kusisitiza wanasiasa wote laghai kuondoka.

Irak Proteste gegen Regierung in Nasiriya
Picha: Reuters/Stringer

Waziri mkuu Adel Abdul Mahdi alitangaza azma ya kujuzulu siku ya Ijumaa baada ya wito uliotolewa na kiongozi wa juu wa madhehebu ya Washia wa kuitaka serikali kuachia madaraka ili kuhitimisha wiki kadha za machafuko.

Waandamanaji wamechoma matairi na kukizingira kituo cha polisi katika mji wa Nassiriya ulioko kusini mwa Iraq, wakishinikiza zaidi juu ya madai yao ya kufanyika mageuzi licha ya waziri mkuu kuahidi kujiuzulu.

Waandamanaji pia wamewasha moto kwenye madaraja matatu muhimu yanayokatisha mto Euphrates huku mamia ya watu wakikusanyika  kwenye kambi ya maandamano iliyopo katikati ya mji.

Vikosi vya usalama vilitumia risasi za moja kwa moja, mabomu ya gesi na maguruneti dhidi ya waandamanaji kwa karibu miezi miwili na kuwaua zaidi ya watu 400 ikiwemo walioauwa siku za karibuni hususan katika mji wa Nassiriya. 

Mikusanyiko imerejea tena licha ya ukandandamizaji uliofanywa na vikosi vya usalama ambao ulisababisha vifo vya zaidi ya waandamanaji 40 siku mbili zilizopita.

Waziri mkuu wa Iraq Abdul MahdiPicha: picture-alliance/AP Photo/H. Mizban

Mji huo umeshuhudia ghasia mbaya zilizoikumba nchi hiyo tangu maandamano ya kuipinga serikali yalipoanza mjini Baghdad. Kuchomwa kwa ubalozi mdogo wa Iran katika mji mtakatifu wa Najaf ulioko kusini, kulichochea ghasia zaidi na kusababisha waziri mkuu Abdul Mahdi kutangaza nia ya kujiuzulu.

Bunge la nchi hiyo litakutana siku ya Jumapili kwa ajili ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu. Hata hivyo ahadi ya Abdul Mahdi ya kujuzulu haijawaridhisha waandamanaji, ambao wanataka mfumo mzima wa kisiasa kufumuliwa wakidai kuwa umejaa ufisadi na kuwafanya maskini na bila fursa zozote.

Wairaq wengi wanahofu kwamba ghasia hizo zitaendelea kwasababu familia nyingi zinaomboleza kwa kuwapoteza ndugu zao huku serikali ikichukua hatua kidogo kufanya mageuzi. Mkwamo wa kisiasa unatarajiwa kuendelea kabla ya mrithi wa Abdul Mahdi kuchaguliwa na serikali mpya kupatikana.

Tume ndogo ya haki za binadamu ya Iraq imesema siku ya Jumamosi katika taarifa yake kwamba wote waliohusika katika mauaji ya waandamanaji lazima washitakiwe na kwamba itakusanya ushahidi kwa ajili ya uchunguzi.

Taarifa hiyo hata hivyo haikugusia hatua ya waziri mkuu kutaka kujizulu. Kamati ya kimatiafa ya msalaba mwekundu imetoa wito wa kusitishwa kwa mauaji hayo.