Wairaq waliobakwa na IS watibiwa Ujerumani
29 Februari 2016Wapiganaji wa jihadi wa kundi linalojiita Dola la Kiisalamu IS walipokuwa wakiliteka eneo la kaskazini mwa Iraq, walikivamia pia kijiji cha watu wa jamii ya Yazidi. Wanawake na watoto wa kike ni miongoni mwa walioathiriki na uvamizi huwo. Kundi hilo lilifanya mauaji ya idadi kubwa. Halikadhalika liliwateka nyara maelfu ya wanawake na watoto wa kike, pamoja na kuwaweka wengine katika utumwa wa kingono. Hali hiyo ilipelekea maelfu ya watu wa kijiji hicho kuyakimbia makaazi yao.
Umoja wa Mataifa umeyaelezea mashambulizi hayo dhidi ya watu wa jamii ya Yazidi, kuwa ni mauwaji ya maangamizi. Daktari Jan Ilhan Kizilhani anayeongoza mradi huo wa Ujerumani, anasema kwamba ni hali inayohitaji ushughulikiaji wa haraka. Na jimbo hilo la kusini magharibi la Baden-Wurttemberg limeutengea mradi huwo kiasi cha euro milioni 95, na kumpa mamlaka kamili Kizilhani ya kuamuwa ni waathirika wapi wanaostahili matibabu.
Wanawake wahanga watengwa na jamii
Daktari huyo anasema wanawake na watoto wengine 1,200 ambao waliwahi kukamatwa na wanamgambo wa kundi la IS wanapata matibabu ya aina hiyo katika maeneo mengine nchini. Aidha aliongeza kwamba wengine 3,800 wanakadiriwa kuwa bado wameshikiliwa na kundi hilo, na pindi watakapopatikana nao watapata matibabu hayo.
Kizilhani anasema wanawake wanaofanikiwa kukimbia baada ya kukamatwa na kundi la IS, wengi wanajikuta wanatengwa katika jamii zao zenye mitazamo ya kihafidhina. Pia wanakuwa hawana njia ya kupata matibabu ya kisaikolojia, ya kuwasaidia kupambana na hali waliyobabiliana nayo walipokuwa mateka wa kundi la IS.
Watu wa jamii ya Yazidi wanafuata imani ya dini inayochukiwa na kundi la IS, kwa hali hiyo wanawake wanaobakwa na wakati mwengine kubeba mimba za wanamgambo wa IS wanaangaliwa kama fedheha katika jamii yao.
Mtoto wa miaka minane abakwa
Daktari huyo anasema kuna visa ambacho hatoweza kuvisahau cha mtoto wa kike mwenye umri wa miaka minane, aliyekutana naye katika kambi ya wakimbizi Agosti iliyopita. Ambaye asilimia 80 ya mwili wake umefunikwa na majeraha ya kuunguwa kwa moto. Mtoto huyo aliunguwa kiasi cha kwamba alipoteza pua pamoja na masikio.
Baada ya kukumatwa na wanamgambo wa IS akiwa na ndugu yake mwengine wa kike kwa wiki kadhaa, wakiwa wanabakwa na kuadhibiwa, ndugu hao wawili walifanikiwa kukimbia. Usiku mmoja wakati akiwa amelala katika kambi ya wakimbizi, aliota kwamba wanamgambo wa IS walikuwa wapo nje ya kambi hiyo. Kwa hofu, mtoto huyo alijimwagia mafuta ya petroli na kujiwasha moto, kwa nia ya kujiharibu uzuri wake ili wapiganaji wa IS wasimbake tena kwa mara nyengine.
Kizilhan aliharakisha matibabu ya mtoto huyo ili apate kuishi. hadi sasa bado yupo hospitali hapa Ujerumani, na licha ya kwamba ameshafanyiwa operesheni kadhaa bado anahitaji operesheni nyengine 30 za ngozi na upasuaji wa mifupa.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/afpe
Mhariri: Sekione Kitojo