1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waislamu na Wakristo Sri Lanka kusali majumbani

26 Aprili 2019

Waislamu nchini Sri Lanka wametakiwa wasihudhurie ibada ya Ijumaa misikitini na badala yake wasali majumbani kwao, sawa na wenzao wa Kikristo ambao nao pia wametakiwa kutofika makanisani.

Sri lanka Colombo Soldaten vor einer Moschee
Picha: Getty Images/AFP/J. Samad

Hii ni baada ya idara ya ujasusi nchini humo kuonya kuhusu uwezekano wa mashambulizi mengine mabomu yaliyotegwa kwenye magari, huku kukiwa na hofu ya machafuko ya kulipiza kisasi kufuatia mashambulizi ya Jumapili ya Pasaka.

Chama kikuu cha Waislamu nchini Sri Lanka, Ceylon Jamiyathul Ullama, kimewataka Waislamu kuswali nyumbani Ijumaa iwapo kuna haja ya kuzilinda familia na mali zao. Naye Kadinali Malcolm Ranjith ametoa wito kwa mapadre kutofanya misa makanisani hadi kutakapotolewa taarifa zaidi kuhusiana na suala hilo. Kadinali huyo amesema usalama ni muhimu.

Jeshi limesema kuwa karibu wanajeshi 10,000 wamewekwa kushika doria katika maeneo ya ibada. Baadhi ya raia wa nchi hiyo kama Maryanam Douglas lakini wanasema bado wana hofu. 

Kiongozi mkuu wa ugaidi afariki

"Ninaogopa sasa hivi bila shaka lakini tutakwenda, tutakwenda katika makanisa yetu," alisema Douglas.

Polisi wanamkagua dereva wa lori katika hatua za kuweka ulinziPicha: picture-alliance/AP Photo/E. Jayawardena

Huku hayo yakiarifiwa mshukiwa anayedaiwa kuwa ndiye aliyekuwa kiongozi wa kundi ambalo uongozi wa Sri Lanka lilihusika na mashambulizi hayo ya siku ya Pasaka, alikufa katika shambulizi lililofanywa katika hoteli ya Shangri-La ambayo ni mojawapo ya hoteli sita zilizolengwa.

Polisi imesema katika ukurasa wake rasmi wa Twitter kwamba Mohamed Zahran ambaye ni kiongozi wa kundi la kigaidi la National Towheed Jamaat aliuwawa katika mojawapo ya mashambulizi tisa ya kujitoa muhanga.

Rais wa Sri Lanka Maithripala Sirisena amewaambia waandishi wa habari mjini Colombo kuwa watu 140 nchini humo wameshatambuliwa kuwa wanahusika na kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS.

Rais amemlaumu waziri wa ulinzi na mkuu wa polisi

Sirisena ametoa wito wa ushirikiano wa kisiasa kwa sasa:

Rais Maithripala Sirisena akiwa katika mojawapo ya eneo la tukioPicha: picture-alliance/AA/The Presidential Office of Sri Lanka

"Natoa wito kwenu nyote, sote tufanye kazi pamoja kulipa nguvu jeshi, kuifanya hali ya maisha kurudi kama kawaida na kubuni mazingira ambayo watu wanaweza kuishi kwa furaha na bila wasiwasi," alisema Sirisena.

Rais huyo amemlaumu waziri wa ulinzi wa nchi hiyo ambaye alijiuzulu jana na mkuu wa polisi ambaye amesema ataachia ngazi karibuni, kwa kushindwa kutoa taarifa kwa wakati kutoka kwa mashirika ya kijasusi ya kimataifa kuhusiana na mpango wa mashambulizi hayo.

Usiku wa Alhamis, wizara ya afya ya Sri Lanka iliishusha idadi ya waliofariki kutokana na mashambulizi hayo ya kupangwa. Taarifa kutoka kwenye wizara hiyo imesema karibu watu 253 waliuawa, idadi hiyo ikiwa karibu thuluthi tatu moja ya ile idadi iliyotolewa na polisi ya watu 359.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW