1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waislamu wa EU wana imani na demokrasia, ubaguzi ukiongezeka

22 Septemba 2017

Waislamu walioko nchi za  Umoja wa ulaya wanaamini demokrasia na kujihisi kuwa sehemu ya jamii ya nchi husika. Hii ni kulingana na utafiti mpya ambao ni wa kwanza kufanywa miongoni mwa waislamu katika Umoja wa Ulaya.

Syrien Ramadan Markt Damaskus
Picha: Getty Images/AFP/L. Beshara

Kulingana na utafiti huo  uliofanywa kwa waislamu 10,500, ni kwamba Waislamu walioko Ulaya wana imani kubwa na taasisi za kidemokrasia kuliko wananchi kwa ujumla, japo wengi wao wanahisi kubaguliwa kwasababu ya dini yao, Utafiti huo uliochapishwa na Shirika la umoja wa ulaya linalohusika na haki za msingi lililoko Vienna FRA umeonyesha kwamba asilimia 76 ya waislamu wa Ulaya wanahisi kwamba ni sehemu ya jamii ya nchi wanazoishi, wakati sehemu kubwa ya waislamu wanapinga  vurugu.

Shirika la FRA ilifanya utafiti huu miongoni mwa wahamiaji na kizazi cha pili cha wahamiaji kutoka Uturuki, Afrika na Asia katika mataifa 15 ambayo ni wanachama wa umoja wa ulaya.

Kulingana na mkurugenzi wa FRA Michael O'Flaherty, matokeo haya ya uchunguzi yanakinzana na madai ya kuwa waislamu hawajaunganishwa katika jamii zetu.  Alisema, "hata hivyo, kwamba Waislamu ambao wanabaguliwa au ambao ni waathirika wa uhalifu wa chuki wanahisi hawana mafungamano na jamii zao."

Ni asilimia 68 tu ya waliohojiwa  wanaohisi kuathirika na ubaguzi  na walisema kuwa mafungamano na nchi zao ni imara ikilinganishwa na asilimia 81 ambao hawakuwa na uzoefu huo mbaya. Matokeo yanaonyesha kwamba ubaguzi unaongezeka.
Karibu mmoja kati ya watano waliohojiwa walisema kuwa wamebaguliwa na wamiliki wa nyumba, waajiri au viongozi wa umma katika miaka mitano iliyopita kwa sababu ya dini yao. Katika utafiti wa 2008, idadi ilikuwa moja tu katika 10. Kutengwa kwa watu ni tofauti kati ya nchi za umoja wa ulaya. Waafrika walihisi kubaguliwa zaidi nchini Ujerumani, Uholanzi na Denmark, huku waturuki wakihisi kubaguliwa Uholanzi na nchini Ugiriki.

Huku kukiwa na mijadala ya umma juu ya viwango vya uhalifu kati ya wageni na mashambulizi ya kidini, watafiti waliwauliza waislamu kama itakuwa sawa kutumia vurugu katika kukabiliana na matusi ya dini au ya kikabila.
Zaidi ya asilimia 85 walisema vurugu haikubaliki katika visa hivyo,wakati karibu asilimia 10 walisema inakubalika  katika hali fulani.Wahamiaji wasiokuwa waislamu wanapendelea kujiepusha zaidi na vurugu.

Picha: AP

Waislamu wanahesabika kuwa asilimia nne ya idadi ya watu katika Umoja wa ulaya.

Utafiti huu ulifanyika mwaka jana kati ya wakazi wa muda mrefu katika umoja wa ulaya isipokuwa wale ambao wamefika tangu kuongezeka kwa wakimbizi mwaka 2015. Nchi nyingi wanachama zina mikakati ya serikali ya kuwajumuisha wageni, na wengi wanatarajia wahamiaji kukabiliana na mazingira mapya, lakini ripoti hiyo inasema  wahamiaji hawapati fursa kubwa ya kushiriki katika jamii.

Shirika la FRA limesema kuwa wahamiaji wangeweza kukuza mizizi yao barani ulaya iwapo mamlaka husika zitakusanya maoni yao kabla ya kuendeleza sera. Kwa namna fulani, waislamu wameonekana kuwa watu walio na uwazi zaidi kuliko wazungu wa kawaida, utafiti umeonyesha. Wakati asilimia 30 ya wananchi wa Umoja wa ulaya wakisema watakuwa na wasiwasi ikiwa mtoto wao alikuwa na uhusiano na muislamu, asilimia 17 pekee ya waislamu wana shida na ndoa za dini tofauti.

Mwandishi: Fathiya Omar

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW