1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waislamu waadhimisha Ramadhan

29 Juni 2014

Waislamu wanaokadiriwa kufikia bilioni 1.6 duniani Jumapili (29.06.2014) wanaanza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan ambapo hujizuwiya kula na kunywa kwa kutwa nzima na kuepuka kila aina ya maovu

Waaumini wakati wa kufturu mwezi wa Ramadhan nchini Sudan.
Waaumini wakati wa kufturu mwezi wa Ramadhan nchini Sudan.Picha: picture-alliance/AP

Mwezi huu mtukufu umegubikwa na machafuko ambayo hayakuwahi kushuhudiwa kabla ya umwagaji damu na uhasama wa madhehebu wenye kutishia kuisambaratisha Mashariki ya Kati ambacho ni kitovu cha Uislamu.

Damu inamwagika nchini Syria. Wanamgambo wa itikadi kali wameteka sehemu kubwa ya ardhi ya Iraq.Lebanon,Libya, Pakistan,Afghanistan na Misri zote zinapambana na Waislamu wa itikadi kali.Mamilioni ya wakimbizi wa vita hivyo wametawanyika kila mahala.

Juu ya kwamba umwagaji damu umeiondosha kwa kiasi kikubwa raha ya Ramadhan,mamilioni ya Waislamu watafunga kwa masaa kwa kutaraji msamaha wa Mwenyenzimungu.

Ramadhan ni nini ?

Ni mwezi wa mtukufu wa kufunga ambapo kwayo Waislamu wanajinyima chakula, maji ya kunywa na aina nyengine ya starehe kuanzia jua linapokuchwa hadi macheo. Ramadhan ni mwezi ambao Waislamu wanaamini kwamba Mwenyeenzimunga alianza kumteremshia Quran Mtume Muhammad (SAW).Kwa waumini huu ni mwezi wa tafakuri na ibada,kukumbuka shida za wengine na kutowa sadaka.

Kuanza na kumalizika kwa Ramadhan

Uislamu unafuata tarehe ya muandamo wa mwezi kwa hiyo kuanza kwa Ramadhan kunatafautiana kila mwaka. Mwezi huu huanza kuadhimishwa mara tu baada ya kuonekana kwa mwezi mchanga. Kuonekana kwa mwezi mpya mwishoni mwa mwezi wa Ramadhan kunaashiria siku kuu ya Idd al- Fitr tamasha la siku tatu la kuadhimisha kumalizika kwa Ramadhan.

Waumini wakati wa sala mwezi wa Ramadhan Cameroon.Picha: picture-alliance/Godong

Kwa nini Waislamu wanafunga?

Funga ni mojawapo ya nguzo tano za Uislamu.Waislamu wanataja sababu nyengine za kufunga ni pamoja na : kujifunza hisia za maskini,kujifunza namna ya kuidhibiti nafsi na kujisabilia kwa Mwenyeenzimungu.Uislamu hauruhusu wazee, watoto, wanawake wajawazito,wagonjwa au wasafiri kufunga.Katika baadhi ya nchi kama vile Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu watu wasio Waislamu hawaruhusiwi kula,kunywa au kuvuta sigara hadharani wakati wa mwezi wa Ramadhan.Nchi nyengine msimamo huo umeregezwa.

Kujifurahisha

Yumkini ukawa ni mwezi wa tafakuri lakini Ramadhan unaweza pia kuwa ni wakati wa kujifurahisha.Kama vike Krismasi au Siku ya Kutowa Sukrani kwa Mungu katika mataifa ya magharibi,Ramadhan ni wasaa kwa familia na marafiki kukutana kwa mazungumzo wakati wa mlo wa kufunguwa saumu unaojulikana kama iftar.Kuna tabia ya mtu kujilia kupindukia na kushabikia vitu vitamu.Kwa kawaida bei za bidhaa wakati wa Ramadhan hupanda mno.

Muumini akisoma Quran mwezi wa Ramadhan nchini Yemen.Picha: Reuters

Ramadhan na vurugu

Wanamgambo wa Kisunni nchini Iraq huko nyuma wamekuwa wakiongeza mashambulizi yao wakati wa mwezi wa Ramadhan kwa imani kwamba mashambulizi hayo hususan ya kujitowa muhanga wakati wa Ramadhan huwa yana baraka kubwa na thawabu kubwa zaidi kutoka kwa Mungu.

Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia Jumapili amewashutumu watu wenye itikadi kali za kidini na kuahidi kutowaachilia magaidi wachache wawatishe Waislamu.

Ibada katika mwezi wa Ramadhan mjini Mecca Saudi Arabia.

Katika hotuba yake ya kuukaribisha mwezi wa Ramadhan amesema Uislamu ni "dini ya umoja,udugu na kusaidiana" lakini baadhi ya watu wakidanganywa na wito usio sahihi wanaelewa vibaya mageuzi kwa kuyachanganya na ugaidi.

Amesema lengo lao ni kutia chokochoko miongoni mwa Waislamu akimaanisha kundi la wanamgambo la Dola la Kiislamu la Iraq na Sham (ISIS).

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP/AFP

Mhariri : Oummilkher Hamidou

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW