1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiSudan

Waislamu waanza mfungo wa Ramadhani

23 Machi 2023

Waumini wa dini ya Kiislamu duniani leo hii wameanza siku ya kwanza ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani ambao kwa kawaida unadumisha ibada ya majuma manne.

Symbolbild | Datteln
Picha: Olga Sergeeva/Zoonar/picture alliance

Nguzo hii katika dini hiyo inatimizwa wakati mataifa na serikali nyingi katika eneo la mashariki ya kati zikiwa katika hatua za kujaribu kutatua migogoro inayoendelea kuwa mibaya zaidi, kuanzia vita vya Ukraine na athari za tetemeko la ardhi la Uturuki na Syria ambalo limesababisha vifo vya zaidi ya watu 52,000.

Katika kipindi cha majuma hayo manne, maelfu ya Waislamu watafunga, kwa maana ya kutokula na kunywa mchana kutwa kabla ya kukusanyika pamoja baada ya ibada ya magharibi kwa futari, mlo wa pamoja kifamilia.

Kwa mujibu wa imani ya dini ya Kiislamu, kufunga kunatengeneza hali ya utiifu na kuwa karibu zaidi na Mungu na kadhalika kuwakumbusha mateso ambayo wanayapitia watu walio katika hali ya umasikini.