Waislamu waungane
2 Mei 2007Mkutano huu wa Waislamu nchini Ujerumani si tukio la siku moja, bali umepangwa kuwa ni mazungumzo yatakayoendelea kwa muda kati ya Waislamu na serikali ya Ujreumani. Mara ya kwanza, wawakilishi wa madhehebu na makundi mbali mbali ya Waislamu nchini Ujerumani pamoja na wajumbe wa serikali ya Ujerumani walikutana mwezi wa Septemba mwaka uliopita.
Waziri wa mambo ya ndani, Wolfgang Schäuble, ambaye ameanzisha mazungumzo haya na kualika washiriki, leo alisema ameridhika na matokeo ya mkutano wa leo na kusema kuwa baada ya nusu mwaka ya kuanzisha mazungumzo kuna maendeleo mazuri: “Sisi sote tumekubali kuwa mazungumzo haya ni muhimu na kuwa yanaendelea vizuri. Bila shaka kuna masuala kadhaa ambayo sisi wajumbe wa serikali tunawaambia wawakilishi wa Waislamu nchini Ujerumani kuwa tunataka kuendelea kuyazungumzia zaidi. Kwa mfano tunasema kuwa kulingana na msingi wa uhuru katika katiba ya Ujerumani watoto, wasichana na wavulana wafundishwe pamoja shuleni. Hapa kuna maoni tofauti na tutaendelea kujadiliana.”
Hakuna matokeo kamili ya mkutano huo, lakini kwa mujibu wa waziri Schäuble, wajumbe wote walikubaliana katika masuala mengi yanayohusiana na katiba, kwa mfano kuwa serikali na dini zinatenganishwa.
Msemaji wa baraza kuu la ushirikiano wa Waislamu wa Ujerumani, Bw. Ayub Axel Köhler alimuunga mkono waziri Schäuble katika kusifu mkutano huu, lakini wakati huo huo alikosoa kutofikiwa lengo lolote. Baraza hilo limeundwa miezi kadhaa iliyopita na ni ushirikiano kati ya jumuiya nne tu za Kiislamu.
Waziri wa ndani Schäuble anawataka Waislamu kuunda shirika la pamoja. Sababu anatoa Bi Maria Böhmer wa chama cha Kihafidhina CDU: “Ni kitambulisho cha dini ya Kiislamu kwamba ina madhehebu tofauti. Jumuiya hizo nne ambazo ziliungana katika baraza la ushirikiano zinawakilisha asilimia 10 au 15 tu ya Waislamu wote walioko nchini Ujerumani. Mimi naamini inapasa wale ambao hawamo katika baraza hilo, vilevile wawe na usemi .”
Kwa sababu hiyo, kwa ujumla viongozi 15 wa Kiislamu kutoka madhehebu mbali mbali walialikwa kwenye mkutano huu wa Berlin. Tangu mkutano uliopita wa mwaka jana, halmashauri mbali mbali zilipewa jukumu la kuzungumzia masuala maalum ambayo matokeo yake yakizingatiwa kwenye mkutano wa leo.