1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump apokelewa kishujaa Israel, kuhutubia Knesset

13 Oktoba 2025

Rais wa Marekani Donald Trump anatarajiwa kuhutubia bunge la Israel wakati makubaliano dhaifu ya kusitisha vita Gaza yakiendelea kuheshimiwa. Waisraeli wamempongeza Trump kwa kufanikisha kurejeshwa kwa mateka

Marekani Kambi ya Angala ya Andrews 2025 | Donald Trump kabla ya kusafiiri kwenda Mashariki ya Kati
Rais Trump atalihutubia bunge la Israel (Knesset) kabla ya kueleke nchini Misri, kuongoza mkutano wa kimataifa kujadili awamu ya pili ya mpango wa amani GazaPicha: Evan Vucci/AP Photo/dpa/picture alliance

Rais wa Marekani Donald Trump anatarajiwa kupokelewa kishujaa katika bunge la Israel, Knesset, Jumatatu, huku makubaliano dhaifu ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas yakiingia siku ya nne.

Hali hii inajiri wakati wa kuanza kwa mchakato wa kuachiliwa kwa mateka wa Kiisrael na wafungwa wa Kipalestina, hatua ndogo lakini muhimu katika juhudi za kumaliza vita vilivyodumu kwa miaka miwili.

Mapigano hayo yalianza Oktoba 7, 2023, baada ya shambulio la Hamas lililosababisha vifo vya watu zaidi ya 1,200 nchini Israel na kuchukuliwa kwa mateka 251. Mashambulizi ya angani na ardhini ya Israel yameiharibu Gaza, na mamlaka ya afya ya eneo hilo ikisema zaidi ya Wapalestina 67,000 wameuawa.

Trump, akizungumza ndani ya ndege ya Air Force One kabla ya kuwasili Israel, alisema, "Vita imekwisha. Nahisi eneo hili litaanza kurejea katika hali ya kawaida.” Wakati huohuo, Umoja wa Mataifa umetangaza kuanza tena misaada ya kibinadamu, ikiwemo gesi ya kupikia na dawa kuingia Gaza kwa mara ya kwanza tangu Machi.

Makubaliano haya yameleta matumaini mapya, lakini wachambuzi wanasema amani ya kudumu bado ni ndoto. Hali hiyo itajadiliwa katika mkutano wa viongozi zaidi ya 20 unaotarajiwa kufanyika leo mjini Sharm el-Sheikh, Misri, chini ya uongozi wa Trump.

Miongoni mwa watakaohudhuria mkutano huo ni Rais wa Palestina Mahmoud Abbas, huku serikali ya Israel ikithibitisha haitashiriki moja kwa moja katika majadiliano hayo.

Picha ya droni ikionyesha watu waliokusanyika kwenye "Uwanja wa Mateka" mjini Tel Aviv, wakiwa wameshikilia mabango makubwa yenye maandishi "RAIS wa NOBEL TRUMP" baada ya kuanza utekelezwaji wa mpango wa kusitisha vita Gaza, Oktoba 11, 2025.Picha: Amir Goldstein/REUTERS

Trump apata pongezi nchini Israel huku shinikizo za kisiasa zikiongezeka

Wizara ya Habari ya Israel imesema mateka 20 waliobaki hai wanatarajiwa kurejeshwa Jumatatu, ikifuatiwa na miili ya mateka 28 waliouawa. Kwa upande mwingine, wafungwa 1,700 wa Kipalestina waliokamatwa tangu Oktoba 2023 wataachiwa baada ya mateka wa Israel kurejea salama.

Katika Ukanda wa Gaza, wakazi wanaorejea kaskazini wanasema hawaamini macho yao. "Tulitembea kilomita 15 kutoka Deir al-Balah hadi Gaza City,” alisema Rami Mohammad-Ali, 37. "Tunafurahia kurejea, lakini ni uchungu kuona uharibifu huu wote na mabaki ya miili barabarani.”

Jumamosi, maelfu ya watu walijitokeza Uwanja wa Mateka mjini Tel Aviv wakimshangilia Trump, huku wakimpigia kelele za upinzani Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu. Hali hiyo ilionyesha wazi mgawanyiko wa kisiasa unaoendelea ndani ya Israel.

Trump atakuwa Rais wa nne wa Marekani kuwahi kuhutubia Knesset, akifuata nyayo za Jimmy Carter, Bill Clinton, na George W. Bush. Spika wa Knesset Amir Ohana alimwita Trump "rafiki mkubwa zaidi wa taifa la Kiyahudi katika historia ya kisasa.”

Wakosoaji wa Netanyahu, wakiwemo familia za mateka, wanamshutumu kwa kuchelewesha makubaliano ili kunufaisha washirika wake wa kisiasa wa mrengo wa kulia. Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) tayari imetoa hati ya kukamatwa kwake kwa tuhuma za uhalifu wa kivita — madai anayoyakana.

Binti wa Rais wa Marekani, Donald Trump, Ivanka Trump akizungumza wakati mumewe Jared Kushner (Kulia-nyuma) na mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff (kushoto) wakitazama wakati wa mkutano kwenye Uwanja wa Mateka mjini Tel Aviv, Oktoba 11, 2025.Picha: Jack Guez/AFP/Getty Images

"Bodi ya Amani” yatiliwa mashaka kabla ya mkutano wa Misri

Trump anapanga kutangaza awamu ya pili ya mpango wake wa amani unaojumuisha kuunda "Bodi ya Amani” itakayosaidia kusimamia Gaza baada ya vita, kwa ushirikiano na waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair. Hata hivyo, maswali bado mengi kuhusu nani atakayeitawala Gaza na mustakabali wa Hamas.

Wakati huo huo, wizara ya mambo ya ndani ya Hamas imesema itapeleka vikosi vya usalama katika maeneo yaliyokuwa yakidhibitiwa na jeshi la Israel, hatua ambayo baadhi ya wachambuzi wanaiona kama kichocheo cha vurugu mpya.

Mazungumzo kati ya Israel na Hamas kuhusu orodha ya wafungwa wa Kipalestina wanaotarajiwa kuachiwa bado yanaendelea. Hamas inasema Israel imeondoa baadhi ya majina ya viongozi wake wakuu katika orodha ya awali, jambo linaloweza kuhatarisha mkataba.

Wizara ya Sheria ya Israel imethibitisha kuwa wafungwa 250 waliopatikana na hatia za mauaji wataachiwa, lakini majina kama Marwan Barghouti na Ahmed Saadat hayajumuishwi. Wakati huo huo, Waziri wa Ulinzi Israel Katz ameonya kuwa jeshi litaendelea kuvunja mitandao ya handaki za Hamas baada ya kurejeshwa kwa mateka.

Mchambuzi wa Kipalestina Akram Attallah ameiambia Reuters kwamba mpango wa Trump "umeundwa kwa namna inayoinufaisha Israel,” akiongeza kuwa Hamas "itapoteza nguvu za majadiliano mara tu itakapokabidhi mateka.”

Mpango wa kusitisha mapigano Gaza waafikiwa

03:28

This browser does not support the video element.

Gaza yakabiliwa na janga jipya la kibinadamu licha ya matumaini mapya

Kurejea kwa wakazi wa Gaza kaskazini kumeonyesha ukubwa wa maafa baada ya miaka miwili ya vita. Mashirika ya misaada yanasema zaidi ya hema 300,000 zinahitajika kuwahifadhi wakimbizi milioni 1.5 waliopoteza makazi.

Kwa upande wa Israel, hatua ya Trump inaonekana kama mafanikio makubwa ya kidiplomasia, lakini wachambuzi wanaonya kuwa bado kuna hatari ya kuvunjika kwa makubaliano. Mkutano wa Misri unatarajiwa kuamua hatima ya mpango huo unaoonekana kama jaribio la kurejesha ushawishi wa Marekani Mashariki ya Kati.

Trump anatarajiwa kutumia hotuba yake Knesset kuhimiza "njia mpya ya ujenzi, uponyaji na umoja wa mioyo,” maneno ambayo pia yamekuwa yakirudiwa na Netanyahu katika matangazo ya televisheni.

Hata hivyo, kwa wakazi wa Gaza kama Rami Mohammad-Ali, matumaini hayo bado ni magumu. "Tunapenda amani, lakini hatuna nyumba za kurejea,” alisema kwa uchungu.

Kwa sasa, dunia inasubiri kuona kama matumaini haya ya muda mfupi yataweza kubadilika kuwa amani ya kudumu katika eneo lililokumbwa na vita kwa miongo kadhaa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW