1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajawazito kurejea shuleni Tanzania

24 Novemba 2021

Serikali ya Tanzania imetangaza itawaruhusu tena wanafunzi waliopata ujauzito kurejea shuleni nchini ya mfumo rasmi wa elimu nchini humo.

Tansania Schüler Symbolbild
Picha: picture-alliance/robertharding

Tangazo hilo ni mabadiliko makubwa ya kisera na ni sehemu ya kile serikali imekitaja kuwa juhudi pana ya  kuondoa vikwazo vya upatikanaji wa fursa sawa ya elimu kwa wote. Kutoka mjini. Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu Sayansi, na Teknolojia nchini Tanzania Profesa Joyce Ndalichako wakati akizungumza na wandishi wa habari Jijini Dodoma kuelekea katika kilele cha maadhimisho miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika hapo Desemba 9 mwaka huu.

Akijibu maswali kutoka kwa wandishi wa habari Waziri Profesa Ndalichako amesema kuwa kumekuwepo na mafanikio pamoja na changamoto za hapa na pale katika sekta ya elimu nchini Tanzania na kwamba serikali inaendelea kutoa vikwazo vya upatikanaji wa fursa ya elimu kwa wanafunzi nchini humu waliokatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali  ikiwemo waliotiwa ujauzito na hivyo kushindwa kuendelea na masomo yao.

Mashaka ya kuongezeka kwa matukio ya ujauzito mashuleni.

Wadau kutoka asasi za kiraia za TanzaniaPicha: DW/S. Khamis

Hata hivyo kumekuwepo na mitizamo tofauti kuwa endapo wanafunzi wa kike wataruhusiwa kuendelea na masomo wakiwa wajawazito au pindi watakapojifungua, hali hiyo italeta kishawishi kwa mabinti wadogo kuanza kujihusisha na masuala ya ngono kabla ya wakati wao, ingawa waziri huyo amesema hakuna mwanamke anaependa kupata ujauzito kabla ya ndoa.

Licha ya serikali ya Tanzania kutoa kauli hiyo kuelekea katika kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika, watetezi wa masuala ya haki za binadamu nchini Tanzania wamekuwa na maoni tofauti. Bi. Anna Henga ni Mkurugenzi wa kituo cha sheria na haki za binadam nchini Tanzania, LHRC anasema ni habari njema ingawa bado inaleta mashaka katika utekelezaji kwa kuwa hakuna sheria inayolisimamia jambo hilo.

Ikumbukwe ya kwamba katika miaka ya nyuma mtoto wa kike nchini Tanzania aliyetiwa mimba hakuruhusiwakuendelea na masomo chini ya mfumo rasmi wa elimu hatua amabyo  mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binadamu yaliitaja kuwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

DW: Dodoma