1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajawazito Ukraine wahofia kujifungua kabla ya wakati

30 Januari 2024

Wanawake wajawazito nchini Ukraine wanahofia kujifungua watoto wao kabla ya wakati katika hospitali ya eneo la Donetsk linalokabiliwa na vita nchini humo, kutokana na kile kinachotajwa kuwa ni matatizo ya muda mrefu.

Dnipro, Ukraine | Wanawake wa Ukraine wakifuatilia jambo kwa umakini
Wanawake wa Kiukraine wakiwaangalia wafanyakazi wa idara ya dharura hawapo pichani.Picha: Clodagh Kilcoyne/REUTERS

Nusu ya akina mama wajawazito wako peke yao kwa sababu waume zao wanapigana vita tangu Urusi ilipoivamia Ukraine. 

Yana Lyakh ni mmoja wa kina mama hao wajawazito aliye katika hospitali hiyo nchini Ukraine .

Mwanamke huyo wa umri wa miaka 26, ana ujauzito wa miezi minane na mumewe yuko katika mstari wa mbele wa vita hivyo vya Urusi nchini Ukraine.  

Mji wao wa nyumbani unakabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa vikosi vya Urusi.

Soma pia:Urusi na Ukraine zashutumiana mashambulizi ya droni

Ili kutafuta mahali salama, Lyakh alihamia katika wodi ya wajawazito katika hospitali hiyo wiki kadhaa kabla ya tarehe yake ya kujifungua .

Lyakh ameliambia shirika la habari la AFP kwamba yuko katika hospitali hiyo kwa sababu ya dhiki.

Ameongeza kwamba hospitali hiyo ya akina mama wajawazito ndio ya kipekee katika eneo zima la Donbas yenye kitengo cha watoto wachanga na mashine ya kuwahudumia watoto waliozaliwa kabla ya wakati.

Licha ya tahadhari za uvamizi wa anga na makombora, hospitali hiyo imefanya kazi bila kufungwa tangu Urusi ilipovamia nchi hiyo kwa takriban miaka miwili sasa. 

Katika kitanda kingine, Katya Brendyuchkova ambaye pia ana ujauzito wa miezi minane, alikuwa anapata matibabu.

 Brendyuchkova anasema kwasasa anakabiliwa na matatizo na kwamba kuna uwezekano wa kujifungua kabla ya wakati.

Juhudi za kuwasaidia kina mama wanaojifungua watoto njiti Uganda

03:57

This browser does not support the video element.

Mumewe ni mwanajeshi lakini anafanya kazi katika mgodi wa makaa ya mawe huko Pokrovsk.

Soma pia:Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz azitolea mwito nchi wanachama wa EU waongeze msaada wa fedha kwa Ukraine

Pokrovsk ni mji ulioko takriban kilomita 30 kutoka kwa moja ya maeneo yenye mapigano makali ya kung'ang'ania eneo la Avdiivka, mji wa kimkakati ambao vikosi vya Urusi vimejaribu kuuteka kwa miezi kadhaa.

Katika hospitali hiyo ya orofa mbili, madirisha mengine yamelindwa kwa mifuko ya mchanga.

Sehemu ya chini ya jengo hilo imegeuzwa kuwa eneo la kujificha kutokana na mashambulizi ya mabomu na pia kuwekwa majenereta yanayotoa umeme wakati unapokatika.

Idadi ya watoto wanaozaliwa yapungua kwa kasi

Madaktari wa magonjwa ya wanawake na wauguzi wameondoka na idadi ya wagonjwa pia imepungua baada ya wakazi wengi kutoroka Mashariki mwa Ukraine mwanzoni mwa uvamizi.

Mtoto mchanga muda mfupi baada ya kuzaliwaPicha: Lisi Niesner/REUTERS

Lyubov Datsyk, mkuu wa idara ya matibabu na upasuaji wa akina mama wajawazito, amesema idadi ya watoto wanaozaliwa imepunguakutoka karibu 1,000 mwaka kabla ya vita hadi 500 mwaka 2022 na 622 mwaka jana.

Takriban asilimia 20 ya watoto waliozaliwa mwaka 2023 walikuwa njiti, hii ikiwa idadi iliyoongezeka kutoka asilimia 10 kabla ya vita.

Madaktari hawana shaka kwamba uvamizi wa Urusi nchini humo ndio uliochangia hali hiyo.

Soma pia:Mahakama ya ICJ kutoa uamuzi ikiwa inayo mamlaka ya kusikiliza kesi iliyofikishwa na Ukraine dhidi ya Urusi

Wafanyakazi katika hospitali hiyo wanasema kumekuwa na visa vya akina baba kuuawa wakati wake zao wakiwa hospitalini na wakati mwingine wanaamua kutowaambia akina mama hao hadi baada ya kujifungua. Vinginevyo, mama mjamzito tayari anajua kuwa ni mjane.

Tsyganok ameliambia shirika la habari la AFP kwamba uvamizi wa Urusi tayari umewagubika watoto hao kabla ya kuzaliwa.

Wanasema kwamba wanapopata watoto wao, wanataka wawe na maisha mazuri ya baadaye lakini  kwasasa wanazaliwa ndani ya vita. Watoto wa vita.

Lyakh anapanga kusafiri kujifungua mjini Dnipro, jiji kubwa lililo umbali wa kilomita 150 kuelekea Magharibi.

Baada ya hapo, yeye na binti yake, ambaye anapanga kumpa jina Sofia, watahamia mji mkuu wa Kyiv. 

Lyakh anasema anataka kwenda mahali pengine lakini hadi sasa, hakuna fursa hiyo, na maadamu mume wake ana kazi thabiti, watasalia katika eneo hilo kwa muda.