Wajerumani kupiga kura leo kuchagua bunge na Kansela
26 Septemba 2021Mgombea wa Ukansela wa chama cha SPD Olaf Scholz mwenye umri wa miaka 63 ambaye amefanya kazi kwa karibu na Merkel kama waziri wake wa fedha kwa zaidi ya miaka minne iliyopita, ndiye mgombea anayeongoza. Mpinzani wake mkuu Armin Laschetaliye na umri wa miaka 60 kutoka muungano wa vyama vya kihafidhina vya CDU/CSU alikuwa anasuasua wakati wa kampeni lakini amejikongoja na kupunguza pengo katika utafiti wa kura za maoni kwa asilimia kidogo katika siku za hivi karibuni.
Tofauti hiyo ndogo itakuwa na umuhimu mkubwa wakati vyama vyote vikijiweka tayari kwa ajili ya kutafuta washirika wa kuunda muungano baada ya matokeo kutolewa. Kwa mara ya kwanza katika historia, chama cha kijani kimemsimamisha mgombea wa Ukansela mwaka huu Annalena Baerbock na wanatarajiwa kuibuka nafasi ya tatu.
Merkel ameongoza muungano wa kihafidhina wa vyama vya CDU na chama dada cha Bavaria CSU, kushinda katika chaguzi nne zilizopita. Ni kiongozi wa pili kukaa madarakani muda mrefu baada ya Helmut Kohl. Wachambuzi wengi wanaonelea muungano wa vyama vitatu kama uwezekano mkubwa wa matokeo ya uchaguzi.
Kama Ujerumani itasalia na muungano wa CDU/CSU itakuwa na jukumu la kutimiza ahadi za kupunguza kodi ikiwalenga zaidi watu wa kipato cha kati na juu, kudhibiti deni la taifa na ajenda ya mabadiliko ya tabia nchi. Ikiwa serikali itaelekea kushoto, punguzo la kodi litawanufaisha wafanyakazi wa kipato cha kati na wale wa kipato cha chini.Uchaguzi wa Ujerumani: Wagombea wahitimisha kampeni
Linapokuja suala la miungano, kujumuishwa kwa vyama vya kijani, FDP na kile cha mrengo wa kushoto die Linke, ni suala litakalochochea sera mpya mezani. Chama cha kijani kinataka kushughulikia zaidi mazingira na nishati mbadala, FDP kwa upande wao wanapigia upatu kodi ya chini na watetezi wa biashara wakati chama cha Die Linke kinataka matajiri kukatwa kodi kubwa.
Wakati vituo vya kupigia kura vitakapofungwa saa 12 jioni, utabiri wa kwanza wa matokeo utatolewa na utabiri mwingine utafuatia hapo baadae.