Wajerumani ughaibuni wakabiliwa na shinikizo la kupiga kura
22 Januari 2025Christian Wagner, msemaji wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock anatoa ushauri kwa Wajerumani wanaoishi nje ya nchi: kwamba iwapo wanataka kuhakikisha kura zao zinahesabiwa katika uchaguzi wa Bunge Februari 23, wanapaswa kupata nyaraka zao za uchaguzi sasa.
Wagner anasema hilo linapaswa kufanyika sasa, kwa sababu kupata karatasi za kupigia kura na wanachama wa vyama vya siasa kwa muda muafaka, kuzijaza na kuzituma fomu hizo nchini Ujerumani kwa wakati, sio jambo rahisi.
Soma pia: Jinsi Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alivyopoteza umaarufu wake
Tarehe ya uchaguzi wa mwaka huu imewekwa baada ya Kansela Olaf Scholz wa chama cha Social Democratic, SPD kupoteza kura ya imani naye katika Bunge katikati ya mwezi Desemba, hatua iliyofungua njia ya kwa Rais Frank-Walter Steinmeier kutangaza kufanyika uchaguzi wa mapema Februari 23, 2025.
Wagner anaonya kuwa muda wa mwisho uliowekwa, baadhi ya Wajerumani wanaoishi nje wanaweza wasipate karatasi za kupigia kura kwa wakati kulingana na nchi wanazoishi. Anasema katika uchaguzi wa kawaida, balozi za Ujerumani na balozi ndogo zilizoko nje huwa zinajiandaa kwa miezi kadhaa kabla ya uchaguzi, lakini sasa wana wiki chache tu.
Upigaji kura kwenye ubalozi wa Ujerumani
Wajerumani wanaoishi nje ya nchi ambao wanataka kupiga kura wanatakiwa kujiandikisha kwenye orodha ya wapiga kura katika mojawapo ya maeneo ya bunge 299 nchini Ujerumani.
Lakini, nchi nyingine hushughulikia kwa njia tofauti. Kwa mfano wakati Uturuki ilipofanya uchaguzi wa duru ya pili wa urais Mei 2023, takribani raia milioni 1.5 wa Uturuki wanaoishi Ujerumani walikuwa na haki ya kupiga kura. Walipiga kura kwenye maeneo 17 tofauti, ikiwemo kwenye balozi zilizoko Ujerumani.
Hilo haliwezekani katika uchaguzi wa Bunge la Ujerumani, kwa sababu Ujerumani, hakuna kipengele cha kupiga kura tu katika balozi. Kulingana na Wagner, hilo halipo katika mfumo wa uchaguzi, lakini sasa inawezekana kutuma baruapepe kwenye wilaya ya uchaguzi nchini Ujerumani na kuomba nyaraka hizo kutumwa.
Soma pia: Steinmeier alivunja bunge na kupisha njia ya uchaguzi wa mapema
Wagner anasema hakuna ulazima wa kujiandikisha nje ya nchi, hivyo wanaweza tu kukadiria ni Wajerumani wangapi wanaishi nje ya nchi, na ni wangapi kati yao wana haki ya kupiga kura. Anasema wanakadiria jumla ya watu milioni tatu au nne. Wajerumani wengi zaidi wanaishi nje ya nchi, lakini sio wote wana haki ya kupiga kura.
Kama sheria, Wajerumani ambao wameishi Ujerumani kwa muda usiokatizwa wa takribani miezi mitatu baada ya kufikisha umri wa miaka 14 wana haki ya kupiga kura.
Kwa maneno mengine, Wajerumani ambao wameishi Ujerumani kwa muda mfupi tu mara kwa mara, hawana haki ya kupiga kura. Hiyo inatumika pia kwa wale wenye pasi za kusafiria za Ujerumani ambao hawajawahi kuishi katika Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani.
Ni Wajerumani 130,000 tu waishio ughaibuni walipiga kura 2021
Yote hayo yanaonekana kuwa magumu, na pengine ndiyo moja ya sababu kwa nini takribani Wajerumani 130,000 tu kati ya wapiga kura milioni tatu hadi nne wanaoishi nje ya nchi, ndiyo walipiga kura katika uchaguzi uliopita wa Bunge wa mwaka 2021.
Wengi wa hao waliishi katika nchi za Umoja wa Ulaya na nchi nyingine za Ulaya kama vile Uingereza na Uturuki. Wajerumani 7,700 tu nchini Marekani, 5,300 barani Asia na 1,500 tu barani Afrika, Canada na Asutralia, kwa pamoja walipiga kura.
Soma pia: Uhakiki wa Ukweli: Je, madai ya Musk na Weidel yana ushahidi?
Muda unazidi kuyoyoma kwa Wajerumani wanaoishi nje ya nchi ambao wanataka kutuma maombi. Wagner ameahidi kwamba balozi 154 za Ujerumani duniani kote na balozi ndogo 50 bila shaka zitasaidia katika kuwasilisha nyaraka za uchaguzi.
Wagner anasema Wajerumani hao wanaweza kupeleka nyaraka zao za kupiga kura zilizokamilika katika ubalozi zikiwa zimefungwa kwenye bahasha. Kutoka hapo, Ofisi ya Mambo ya Nje ya Ujerumani itazisafirisha hadi kwenye ofisi za Berlin au Bonn.
Kisha nyaraka hizo zitatumwa kwa njia ya posta kwenye maeneo ya Bunge, ambako lazima zipokelewe ifikapo majira ya saa kumi na mbili jioni Februari 23.