1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajerumani hawataki kuongozwa la Laschet

28 Septemba 2021

Chama cha CDU kilishindwa kwa asilimia chache katika uchaguzi mkuu na chama cha SPD

BdTD Deutschland | Nach der Bundestagswahl - Abbau der Wahlwerbung
Picha: Peter Gercke/dpa/picture alliance

Kitendawili cha nani ataunda serikali mpya nchini Ujerumani bado hakijateguliwa,wabunge wa kundi la wahafidhina,CDU/CSU wanazidi kupaaza sauti kumkosoa mgombea ukansela Armin Laschet  ambaye anaendelea kupania kutaka kuunda serikali ijayo,licha ya kushindwa kwenye uchaguzi.

Kambi ya wahafidhina inayoongozwa na chama cha Christian Democratic CDU  ilishindwa kwenye uchaguzi wa Jumapili wa shirikisho, na chama cha Social Democratic SPD kikiongozwa na mgombea wake ukansela Olaf Scholz ambacho kilipata ushindi mwembamba, lakini licha ya kushindwa huko kwa kambi ya wahafidhina, kiongozi wake Armin Laschet anasema atajaribu kuunda serikali.

Vyama vilivyochukua nafasi ya tatu na nne ni wanamazingira yaani The Greens na waliberali FDP waliokuwa namba nne. Na vyama hivyo tayari vimekwishaanza mazungumzo yao ya pamoja kufikia uamuzi ikiwa wataunda serikali ya mseto na SPD au CDU. Kimsingi Olaf Scholz aliyetangazwa mshindi kwenye uchaguzi wa Jumapili chama chake cha SPD ndicho kilicho na mamlaka ya kuunda serikali.

Picha: Sean Gallup/Getty Images

Uchunguzi wa kura ya maoni uliofanywa nchini unaonesha wajerumani wengi hawataki Armin Laschet awe Kansela. Uchunguzi wa taasisi ya utafiti ya Civey ambayo imefanywa kwa niaba ya gazeti la mjini Ausburg-Ausburger Allegemeine umeonesha kwamba asilimia 71 ya wajerumani waliohojiwa walisema sio sawa chama cha CDU kuunda serikali wakati matokeo ya uchaguzi wa nchi nzima umeonesha kimepoteza uungwaji mkono na kushikilia nafasi ya pili.

Uchunguzi huo umeonesha asilimia 55 tu ya wapiga kura wa CDU wanasimama pamoja na Armin Laschet. Uchunguzi kama huo umefanywa pia na gazeti la kihafidhina la  Bild na umeonesha asilimia 58 ya waliohiojiwa hawakufikiri kwamba CDU ina ridhaa ya kuongoza serikali ijayo.

Wana CDU wanamkosoa Laschet wakati pia chama ndugu cha CSU kikijikuta kwenye mkumbo wa kunyooshewa kidole baada ya kushindwa vibaya sana kwenye matokeo ya uchaguzi wa shirikisho kwa kiwango ambacho hakijawahi kutokea tangu mwaka 1945. Lawama kubwa zaidi anabebeshwa Laschet ambaye kampeini yake ilisheheni dosari chungunzima na kadhia,akionekana mtu asiyekuwa na haiba ya uaminifu wala uchapa kazi  kama aliyokuwa nayo Merkel.

Picha: Gero Breloer/dpa/picture-alliance

Kauli zinaendelea kusikika kutoka pande mbali mbali za kumtaka bwana Laschet akae pembeni. Lisa Badum msemaji wa chama cha kijani bungeni anasema wahafidhina wameshindwa na mwelekeo uko unaonesha waziwazi.Lisa anaamini chama chake kilijifunza kwenye uchaguzi wa mwaka 2017 na wamejiimarisha na kupata ushindi mkubwa wa kura za vijana wakati wahafidhina wamepoteza kwenye uchaguzi huu.

Wakati huohuo chama cha SPD kikionekana kujaribu kuzima juhudi zozote za CDU kuanza mazungumzo ya kutafuta kuungwa mkono kuunda serikali ya mseto,Chama hicho cha siasa za wastani za mrengo wa shoto, kimesema leo kwamba kitakuwa tayari kuanza mazungumzo na Kijani na FDP wiki hii.

Rolf Mützenich kiongozi wa SPD bungeni amefafanua kwamba wiki hii wataanza mazungumzo ikiwa Kijani na FDP watakuwa tayari na mazungumzo sio tu yatakwenda kwa kasi kwa upande wao lakini pia yatakuwa ya uwazi na ikiwa kutakuwa na matatizo yatakayojitokeza baina ya vyama yatatatuliwa kwenye mchakato huo.