Wajerumani wanapiga kura leo
22 Septemba 2013Baada ya kuuongoza uchumi mkubwa wa kwanza katika bara la Ulaya kupita katika msukosuko mkubwa wa madeni, Merkel amejitokeza kuwa maarufu zaidi kutokana na anavyotoa uhakika kama atoavyo mama kwa mtoto wake, kwa viongozi ambao wameingia matatani kama vile nchini Ufaransa, Ugiriki, Italia na Uhispania.
Wachunguzi wa maoni ya wapiga kura wanaashiria kuwa wapiga kura watamchagua tena kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 59, ambaye jina lake la utani , ni "Mutti", yaani mama anayeonekana kushabihiana zaidi na jina analotambulishwa nalo kila mara la mwanamke mwenye nguvu duniani.
Nani atakuwamo katika serikali
Lakini suala muhimu hapa litakuwa nani ataunda serikali nae? "Ni mara chache hali imekuwa ya karibu hivyo. Muungano wa Merkel una wingi mdogo tu kwa mujibu wa maoni ya wapiga kura , limesema gazeti la Sueddeutsche Zeitung, na kuongeza kuwa wengi wa wapiga kura wapatao milioni 62 wanaamua katika dakika za mwisho nani wampigie kura.
Merkel anajigamba kuwa muungano wake wa sasa wa siasa za wastani za mrengo wa kulia umekuwa na mafanikio makubwa tangu baada ya Ujerumani mbili kuungana mwaka 1990, kwa kuwa na uchumi imara na kiwango cha ukosefu wa ajira kikiwa chini ya asilimia saba.
Lakini lengo alilojiwekea kwa ajili ya chama chake cha Christian Democratic Union (CDU) kubaki madarakani na washirika wake wadogo katika serikali, chama kinachopendelea wafanyabiashara cha Free Democratis, FDP, linategemea majaaliwa ambayo hayana hakika kwa chama hicho kidogo. "Kuendelea kutawala pamoja na washirika wake wa sasa ni suala ambalo halina uhakika," Gero Neugebauer, mtaalamu wa masuala ya siasa kutoka chuo kikuu huria cha mjini Berlin amesema.
Iwapo muungano huo utafeli kupata wingi wa kutosha kuweza kutawala, Merkel anaweza kulazimika kuingia katika mikono ya mahasimu wake wa jadi, chama cha Social Democratic , SPD, ambacho alikishirikisha katika kile kinachojulikana kama muungano mkuu, lakini usio na mapenzi, katika kipindi chake cha kwanza cha uongozi.
Chama mbadala
Huku washirika wake wa Ulaya wakikodolea macho, chama kinachopinga muungano wa Ulaya , chama chaguo mbadala kwa Ujerumani, The Alternative for Germany, (AfD) kinaweza pia kupata mafanikio, ama kwa kuvutia kura za kutosha kuingiza wabunge katika bunge la Ujerumani ama kwa kuzipoteza kura za wapiga kura wa siasa za wastani za mrengo wa kulia.
"Kwa kansela Merkel chama hicho kisichopendelea muungano wa Ulaya kinakuwa tatizo," limesema gazeti la Spiegel mtandaoni katika mkesha wa uchaguzi. "Iwapo chama hicho kinachopinga kitafaulu kuvuka kizingiti cha asilimia tano na kuingia bungeni , hali hiyo inataigharimu mno muungano wa njano na nyeusi yaani vyama tawala vya sasa vya CDU,CSU na FDP," limeongeza gazeti hilo.
Chaguzi tatu za kabla ya uchaguzi huu, zimeonesha kuwa chama cha AfD, ambacho kinataka kuachana na sarafu ya euro na kuvunjwa kwa muungano wa mataifa ya eneo la euro, kimeshindwa kuvuka kiunzi cha asilimia tano zinazotakiwa kwa chama kuingia katika bunge.
Lakini baadhi ya wadadisi na wachunguzi wa maoni ya wapiga kura hawajaondoa uwezekano wa chama hicho kufanya vizuri huku kukiwa na hofu mpya ya Ugiriki kuomba msaada mpya, na kusisitiza kuwa ni vigumu kutathmini nafasi za chama hicho kwasababu hakina rekodi maalum ya uchaguzi na waungaji wake mkono huenda wasikiunge mkono kama walivyofanya katika uchunguzi wa maoni.
Merkel kwa mara nyingine amesisitiza umuhimu wa Ulaya kwa Ujerumani katika kampeni ya dakika za mwisho kuweza kupata kura mjini Berlin jana Jumamosi (21.09.2013), akisema kuwa nchi yake " inaweza tu kufanya vizuri kwa muda mrefu iwapo Ulaya nzima itafanya vizuri".
"Hii ndio sababu uimarishaji wa sarafu ya euro sio tu ni mzuri kwa ajili ya Ulaya lakini pia kwa maslahi ya Ujerumani," amesema wakati bendi ya muziki ikiimba , "Angie auokoe ulimwengu". Waungaji mkono wa hatua imara za kuchochea ukuaji wa uchumi wameweka matumaini yao kwa chama cha SPD ambacho mgombea wake Peer Steinbrück , mwenye umri wa miaka 66, amekuwa akihangaika kupata kitu kinachoweza kuwavuta wapiga kura na bado yuko nyuma ya Merkel katika maoni ya wapiga kura kwa alama 13.
Waziri wa zamani wa fedha katika uongozi wa Merkel mwaka 2005-2009 katika ule muungano mkuu, Steinbrück amejiingiza katika matatizo wakati wa kampeni hii, hivi karibuni kabisa akionesha kidole cha kati kikiashiria matusi katika picha iliyochapishwa katika kurasa za mbele za magazeti, ikiwa ni jibu la kimya kimya kwa swali aliloulizwa kuhusiana na kuyumbayumba kwa nafasi yake ya kugombea ukansela.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre
Mhariri: Bruce Amani