1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajerumani wanasubiri kwa hamu serikali mpya ya muungano

29 Septemba 2021

Wajerumani wanasubiri kwa hamu kujua ni chama gani kitakachounda serikali ijayo ya muungano baada ya uchaguzi wa siku ya Jumapili ambapo chama cha sera za wastani za mrengo wa kushoto, SPD kilipata ushindi mwembamba.

Bildkombo | Scholz - Linder - Baerbock

Chama hicho cha SPD, muungano wa vyama vya kihafidhina CDU/CSU, pamoja na chama cha Kijani na kile kinachoelemea biashara huru cha FDP vimekuwa vikifanya mkutano wa kujadili mustakabali wao wa kisiasa huku vyote vikionyesha matumaini ya kuwa sehemu ya serikali ijayo.

Kiongozi wa chama cha CDU Armin Laschet anakabiliwa na mvutano unaoendelea ndani ya chama chake baada ya kushindwa katika uchaguzi uliofanyika siku ya Jumapili.

Umaarufu wa Laschet wapungua

Wakati Laschet na viongozi wa vyama vingine wakikutana kuamua hatua zijazo za kuchukua, matumaini ya kuungwa mkono na vyama vya CDU na CSU katika kushiriki mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano yanafifia, huku umaarufu wake ukizidi kupungua ndani ya vyama hivyo.

Laschet aliyekuwa mgombea wa Ukansela wa vyama vya muungano wa kihafidhina vya CDU na CSU, amesema anapanga kufanya mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano na chama cha Kijani na FDP.

Akizungumza Jumanne usiku, Laschet mesema watazungumza na vyama hivyo katika siku zijazo. Matamshi hayo ameyatoa baada ya kukutana na kundi la wabunge wapya wa CDU na CSU.

Kiongozi wa chama cha CSU, Markus Soeder na Kiongozi wa CSU, Armin LaschetPicha: Tobias Schwarz/Pool/picture alliance

Kiongozi wa chama cha CSU, Markus Soeder ambaye pia ni Waziri Mkuu wa jimbo la Bavaria amesema kiongozi wa chama cha SPD, Olaf Scholz ana nafasi nzuri ya kuwa kansela na kumrithi Angela Merkel kutoka chama cha CDU, ambaye ameiongoza Ujerumani kwa miaka 16.

Kiongozi wa wabunge wa SPD, Rolf Muetzenich, amesema tayari SPD imevialika vyama vya Kijani na FDP kwa mazungumzo wiki hii. Scholz aliwahutubia wabunge wapya wa chama chake siku ya Jumanne kupitia ukurasa wake wa Twitter. Muetzenich amesema SPD iko tayari kwa mazungumzo ya haraka na ya kweli.

Katika mazungumzo yaliyofanyika Jumanne Berlin, CDU na CSU vilifikiria kumuomba Soeder aongoze mazungumzo ya kuunda serikali na vyama vya Kijani na FDP. Wito umekuwa ukitolewa kumtaka Laschet akubali kushindwa na ajiuzulu.

Soma zaidi: Wajerumani wamtaka Laschet akae pembeni

Ellen Demuth, mbunge wa CDU katika bunge la jimbo la Rhineland-Palatinate amemtaka Laschet ajiuzulu na kuepusha madhara zaidi. Aidha, mkuu wa tawi la vijana la CDU, Tilman Kuban, amesema wameshindwa katika uchaguzi na hakuna mjadala.

Michael Kretschmer, Waziri Mkuu wa Jimbo la Saxony amesema haoni mamlaka yoyote ya wazi kwa CDU kujaribu kuunda serikali. Anasema ameshuhudia ujumbe mzito kutoka kwa wapiga kura, ambao wamesema wazi kuwa CDU na CSU sio chaguo lao la kwanza kwa wakati huu.

Michael Kretschmer, Waziri Mkuu wa Jimbo la Saxony Picha: Jens Krick/Flashpic/picture alliance

Waziri wa Uchumi wa Ujerumani, Peter Altmaier, mshirika wa karibu wa Merkel amevipongeza vyama vya SPD, Kijani na FDP kutokana na ushindi walioupata katika uchaguzi huo. Altmaier ameviambia vituo vya utangazaji vya RTL na ntv kuwa muungano wa vyama vya kihafidhina hauna mamlaka ya kuendelea na mazungumzo ya kuunda serikali ya mseto.

Masuala yatakayoangaziwa

Mwanasiasa wa CSU, Alexander Dobrindt amesema ukuaji wa uchumi, sera za kuyalinda mazingira na usalama wa ndani na nje, ndiyo maeneo ya kuzingatiwa iwapo watafanya mazungumzo na chama cha Kijani na FDP, katika muungano uliopewa jina ''Jamaica'' kutokana na rangi za vyama hivyo vitatu ambazo ni nyeusi, njano na kijani kuendana na zilizoko kwenye bendera ya nchi hiyo ya Caribbean.

Wakati huo huo, Ralph Brinkhaus wa CDU amechaguliwa tena kuliongoza kundi la wabunge wa CDU na CSU katika Bunge la Shirikisho la Ujerumani. Laschet na Soeder wamemuunga mkono Brinkhaus kuendelea kushikilia wadhifa huo kwa mara nyingine.

Hata hivyo, Brinkhaus aliyepitishwa kwa kura 164, atadumu kwenye nafasi hiyo kwa miezi saba na sio mwaka mzima kama ilivyo utamaduni kwa sababu hadi sasa haijafahamika iwapo vyama vya muungano wa kihafidhina vya CDU na CSU, vitaingia kwenye serikali au vitakuwa vyama vya upinzani.

(DPA, AFP, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW