1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

Wajumbe wa Baraza la Usalama la UN kuzuru kivuko cha Rafah

11 Desemba 2023

Wajumbe kadhaa wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamesafiri hii leo hadi nchini Misri ambako wanatarajiwa kuzuru kivuko cha mpakani cha Rafah.

Ägypten Palästinenser Rafah Grenzübergang
Lori la misaada likiruhusiwa kutumia kivuko cha mpakani cha Rafah kuelekea Gaza: 04.12.2023Picha: AFP/Getty Images

Wajumbe 12 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa watazuru kivuko hicho cha Rafah kwenye mpaka kati ya Misri na  Ukanda wa Gaza , lakini ujumbe huo hautajumuisha mwakilishi kutoka Marekani.

Hata hivyo Nate Evans, msemaji wa Ujumbe wa Marekani katika Umoja wa Mataifa amesema nchi yake inafahamu vyema hali ilivyo ngumu huko Rafah na kuwa inajaribu kuboresha hali hiyo. Kivuko cha Rafah ni sehemu muhimu ya uwasilishwaji wa misaada ya kibinadamu huko Gaza.

Soma pia:Mataifa ya kiisalam yaikosoa Marekani katika vita ya Gaza 

Wiki iliyopita, Marekani ilipinga azimio lililopendekezwa la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likitaka kusitishwa mara moja kwa mapigano kutokana na sababu za kiutu. Hapo kesho, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kupigia kura azimio kama hilo.

Maazimio ya Baraza Kuu huwa hayana uzito katika Umoja wa Mataifa lakini tofauti na yale ya Baraza la Usalama, Marekani haiwezi kutumia kura yake ya turufu kuyazuia, kitendo kilichokosolewa na Mao Ning, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa China.:

"Ikiwa Marekani inajali kweli haki za binadamu, haipaswi kuzuia kupitishwa kwa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka kusitishwa kwa mapigano kwa sababu za kiutu ili kukabiliana na janga la kibinadamu linalozidi kuwa baya huko Gaza."

Maafa zaidi katika vita vya Gaza

Kifaru cha Israel kikirusha makombora kusini mwa Ukanda wa Gaza: 10.12.2023Picha: Leo Correa/AP/picture alliance

Wakati Israel ikiendeleza mashambulizi yake katika Ukanda wa Gaza na kulilenga zaidi eneo la kusini, nchi hiyo imefahamisha kuwa wanajeshi wake wapatao 100 wameuawa huko Gaza tangu kuanza kwa operesheni yao ya ardhini huko Gaza.

Soma pia: Netanyahu awataka wanachama wa Hamas kujisalimisha haraka

Vita vya Gaza vilianza Oktoba 7 baada ya wanamgambo wa Hamas kuivamia Israel na kuua watu 1,200 na kuwachukua mateka wengine karibu 240. Nayo Wizara ya Afya inayodhibitiwa na Hamas imesema karibu Wapalestina 18,000 wameuawa huko Gaza tangu kuanza kwa vita hivyo.

Ingawa kuna mjadala juu ya kutofautisha idadi ya vifo vya raia na wapiganaji, mashirika ya Umoja wa Mataifa na taasisi nyingine za kimataifa zinaamini kuwa idadi ya vifo inayotolewa na ya wizara hiyo ni sahihi kwa kiasi kikubwa.

Wito wa vikwazo vya EU kwa kundi la Hamas

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell akizungumza na waandishi wa habari mjini Brussels nchini Ubelgiji kabla ya mkutano wa kujadili sera ya kigeni ya umoja huo: 11.12.2023Picha: Kenzo Tribouillard/AFP

Wakati mawaziri wa mambo ya nje wa nchi 27 za Umoja wa Ulaya walipokutana mjini Brussels, Ubelgiji leo Jumatatu, Ujerumani, Italia na Ufaransa zimetoa wito kwa Umoja wa Ulaya kuchukua vikwazo thabiti dhidi ya Hamas na wafuasi wake.

Soma pia: Gaza ni 'jehanamu ya dunia' - Lazzarini

Wito huo ulitolewa katika barua iliyotumwa kwa mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell na imeweka wazi kuwa kupitishwa haraka kwa aina hii ya vikwazo, kutatuma ujumbe mzito wa kisiasa kuhusu ahadi ya Umoja wa Ulaya ya mshikamano na Israel na mapambano dhidi ya kundi la Hamas.

Katika hatua nyingine, mataifa kadhaa ya Kiarabu yameshuhudia mgomo wa wafanyakazi huku biashara na taasisi zikifungwa ili kudhihirisha mshikamano na watu wa Palestina lakini pia kutoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano huko Gaza. Mgomo kama huo umeshuhudiwa pia mashariki mwa Jerusalem na Katika  Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Israel.