1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama tawala Tanzania CCM, kumchagua mrithi wa Kinana

17 Januari 2025

Chama tawala nchini Tanzania cha CCM kinafanya mkutano wake mkuu maalumu siku ya Jumamosi, ambao pamoja na mambo mengine utamchagua makamu mwenyekiti wa chama hicho, Tanzania Bara.

Mwenyekiti wa CCM, Samia Suluhu Hassan, akiongoza kamati  kuu 2023
Mwenyekiti wa CCM taifa, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, akiongoza kamati kuu 2023Picha: CCM office

Wajumbe wameanza kukusanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete ulioko katikati ya jiji hili la Dodoma na kwamba shughuli yao ni kupokea taarifa za kiutendaji kutoka kwa viongozi wa chama kabla ya kupewa mwelekeo wa kumpata mrithi wa Kinana.

Makamu mpya atakayechaguliwa anatazamiwa kuwa na ushawishi mkubwa ndani ya chama na hata nje, hasa wakati huu ambao karibu vyama vyenye usajili wa kudumu vimeanza kuota kuhusu uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu utakaowahusisha madiwani, wabunge na rais. CCM yawaonya makada wake kuelekea mbio za uchaguzi

Kwa kawaida, makamu mwenyekiti wa chama hicho tawala ndiye anayekuwa mwenyekiti wa kamati ya maadili ambaye moja ya majukumu yake ni kuwamulika makada wa chama wanaokwenda kinyume wakati wa mchaka mchaka wa kuwania nafasi mbalimbali za kuteuliwa na chama katika uchaguzi mkuu.

Katibu Mkuu wa CCM Emmanuel John NchimbiPicha: CCM

Mchambuzi wa siasa za Afrika, Gwandumi Mwakatobe anasema chama hicho tawala kinapaswa kuchanga vyema karata zake ili kumpata makamu mwenyeti mahiri na ambaye atakayevaa  vyema viatu vilivyoachwa na Kinana.

Chama hicho tawala cha CCM kimekuwa kikiwaonya makada wake kujiweka kando na ndoto za kuchukua fomu za kuwania nafasi za urais kikisema fomu itakayotolewa ni moja tu, kikimaanisha Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye mwenyekiti kuwa ndiye atayepeperusha bendera ya chama katika uchaguzi wa mwaka huu.

Hatua hiyo inafuatia hisia zilizokuwa zikitanda ndani ya chama za kuwepo makundi yanayotaka kujaribu kusogeza majina yao kuwania nafasi hiyo. Akilitazama suala hilo, mchambuzi Mwakatobe anasema "hali hiyo haishangazi" na huenda ikajitokeza pia katika mkutano huo wa Jumamosi kwa vile makundi yanayotaka kutingisha hali ya chama wakati huu wa kuelekea katika uchaguzi mkuu bado yangali yakijivinjari.

Mwenyekiti wa CCM taifa, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, akiongoza kamati kuu 2023Picha: CCM office

Hata hivyo, wengi wanaofuatilia mkutano huu wanaamini kuwa chama hicho tawala kina ushawishi wa kutosha kuwakusanya pamoja wanachama wake na hatimaye wakiondoka Dodoma wakiwa tayari wamemuunga mkono makamu mwenyekiti mpya.

Soma: Wadau Tanzania wajadili upatikanaji wa katiba mpya

Benard Erick ambaye anajitambulisha kama ni mtu mwenye kuzifuatilia kwa karibu siasa za chama hicho anasema mafanikio ya CCM kuelekea uchaguzi mkuu yataanza kudhihirika kutokea Dodoma.

Kumekuwa na majina kadhaa yanayochomoza vichwani mwa wachambuzi wengi wa siasa kuhusu yule atakayerithi nafasi ya Kinana, kuwa makamu mpya mwenyekiti wa chama.

Lakini hakuna ubashiri wa moja kwa moja kati ya majina hayo yanayopewa alama kubwa ya kuibuka kinara.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW