Wajumbe wa China na Dalai Lama wakutana kuhusu Tibet
5 Mei 2008Pande mbili husika katika mgogoro wa jimbo la Tibet zimeanza mazunguzo ya kutafuta suluhu.
Mkutano huo umefuatia shinikizo kutoka kwa mataifa ya magharibi, yakiitaka serikali ya Beijing kujadiliana na kiongozi wa kidini wa Tibet ,Dalai Lama ambae inamlaumu kwa kuchochea ghasia katika eneo hilo,madai anayokanusha.
Mkutano huu kati ya wajumbe wa serikali ya China na wale wa kiongozi wa kiroho wa Tibet ,Dalai Lama, ulifanyika jana jumapili katika mji wa kusini wa Shenzhen. Na ndio wa kwanza wa aina hiyo tangu ghasia za Tibet za mwezi wa Machi.
Mazunguzo hayo yalipendekezwa mwezi uliopita na utawala wa Beijing baada ya kushinikizwa na serikali za magharibi kuanzisha mazungumzo na Dalai Lama.
Serikali ya Tibet ilioko uhamishoni imesema leo kuwa duru mpya ya mazunguzo na china imekuwa muhimu na kuongeza kuwa imeridhishwa na azma ya serikali ya China ya kutaka kuendelea na mazungumzo.
Lakini mkutano wa siku moja uliokuwa wa faragha,tena wa kwanza kati ya pande hizo kwa kipindi cha mwaka mmoja,ulimalizika jumapili bila ya kuripotiwa mafanikio yoyote katika kusuluhisha mgogoro mzima wa Tibet.
Hata hivyo kuna maelezo mawili matatu ambayo yameanza kujitokeza.Msemaji wa serikali ya uhamishoni ya Tibet iliona makao yake kaskazini mwa India,Thubten Samphel,ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, suala la Tibet ni gumu mno kuweza kupatikana ufumbuzi katika mikutano miwili au mitatu.Ameongeza kuwa jambo muhimu ni kuwa pande mbili kuwa zinazungumza akisema kuwa hilo litaweza kuondoa kutoaminiana kati ya pande zote.
Lakini Mtibet mmoja wa ngazi za juu amegusia kuvunjwa moyo na kutopatikana na maendeleo bayana katika mkutano huo. Amenukuliwa akisema kuwa alikuwa anataraji kupata hakikisho kuwa kamatakamata katika Tibet itamalizika.Ameongeza kuwa atasubiri neno la wale waliosiriki katika mkutano huo.
Wajumbe wanategemewa kurejea India aidha kesho jumanne ama kesho kutwa ili kumuelezea Dalai Lama kilichojiri.
Kiongozi mmoja wa chama kimoja cha kisiasa cha Tibet, Zhang Qingli anasema kuwa hali sasa ni tulivu na kusema kuwa yaliyopita si ndwele na inafaa wagange yaliyopo ama yajayo.
China, mara kadhaa imekuwa inamlaumu Dalai Lama,kwa kutaka eneo hilo kujitawala na kuchochea ghasia kwa lengo la kuhujumu michezo ya Olimpiki ya mwezi Agosti.
Vyombo vya habari vya serikali ya China leo jumatatu vimetoa maneno makali dhidi ya Dalai Lama licha ya serikali kuendeleza mazungumzo na ujumbe wake.
Katika toleo la leo la TheTibet Daily,makala moja imendika iksema kuwa,kufuatia tukio la Machi 14 mjini Lhasa,Dalai lama sio tu amekataa kukukirimyaliyokiita ,uhalifu mkubwa, lakini ameendelea kuendeleza uongo.
Hata hivyo makala hiyo haikugusia chochote kuhusu mazunguzo ya jana jumaili.Lakini yameendelea kuelezea madai ya Dalai Lama ya kutaka utawala wa ndani wa Tibet kama udanganyifu.
Tena gazeti la kiingereza la kila siku la China Daily,limelielezea kundi la vijana la Tibet,ambalo linaendeshwa na serikali ya Tibet ilioko uhamishoni kama kundi la kigaidi lenye nia ya kuimegua Tibet kutoka China.
Hata hivyo Dalai Lama ambae alipata tuzo la amani la Nobel la mwaka wa 1989,amekanusha madai hayo yote.Yeye kwa upande wake anasema anailaumu tu China kwa ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya watu wake.
Mbali na hayo serikali ya China imekubali kuendelea na mazungozo japo haikusema lini na wapi.