1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajumbe wa COP28 watoa ahadi za fedha

4 Desemba 2023

Ahadi za fedha zimepewa nafasi kubwa kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa juu ya mabadiliko ya tabia nchi unaoendelea Dubai baada ya wajumbe kuangazia pengo kubwa katika mahitaji ya fedha kwa ajili ya mazingira.

VAE COP28 in Dubai
Mtu akizungumza kwa simu kando na bango la mkutano wa COP28 huko Dubai.Picha: Amr Alfliky/REUTERS

Umoja wa Falme za Kiarabu, mwenyeji wa mwaka huu wa mkutano huo, umeahidi dola bilioni 270 katika ufadhili wa miradi ya mazingira ifikapo mwaka 2030 kupitia benki zake, huku benki kadhaa za maendeleo zikichukua hatua mpya za kuongeza juhudi za ufadhili, ikiwa ni pamoja na kukubaliana kusitisha ulipaji wa madeni wakati maafa yanapotokea.

Soma pia: COP28: Ahadi za kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi hazitekelezwi ipasavyo

Kiasi cha pesa kinachohitajika kwa mabadiliko ya nishati, hatua za kupambana na mabadiliko ya tabia nchi na msaada wa maafa ni kikubwa mno.

Ripoti iliyotolewa Jumatatu ilikadiria kuwa masoko yanayoibukia na nchi zinazoendelea zitahitaji uwekezaji wa dola trilioni 2.4 kwa mwaka ili kupunguza uzalishaji na kukabiliana na changamoto zinatokana na mabadiliko ya tabianchi.

Nchi zilizo hatarini ambazo tayari zinakabiliwa na gharama kubwa ya majanga ya hali ya hewa zinaomba mabilioni ya fedha zaidi kupitia hazina mpya ilianzishwa ya maafa, ingawa kufikia sasa ahadi zilizotolewa zinakaribia dola milioni 700 pekee.

soma pia: Marekani yaahidi dola bilioni tatu kwa mfuko wa mazingira

Waziri Mkuu wa Barbados Mia Mottley, ambaye amekuwa maarufu duniani kwa kutilia mkazo kuhusu kutenga fedha za hali ya hewa, katika kikao na waandishi wa habari amezitaka nchi kwenda mbali zaidi ya ahadi za hiari na maombi kwa mashirika ya misaada na wawekezaji binafsi na badala yake kuzingatia kodi kama njia ya kuongeza ufadhili wa hali ya hewa.

Wajumbe wengine akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, wametoa wito wa kukomeshwa kwa ruzuku ya mafuta ambayo imefikia rekodi ya dola trilioni 7 kwa mwaka.

Soma pia; Kansela Olaf Scholz ahimiza kuachana na nishati ya mafuta

Rais wa COP28 akosolewa

Sultan Ahmed Al JaberPicha: Thaier Al-Sudani/REUTERS

Huku haya yakijiri rais wa mazungumzo ya hali ya hewa ya Umoja wa Mataifa katika Umoja wa Falme za Kiarabu Sultan Al Jaber ametejitetea kwa kusisitiza imani yake katika sayansi ya hali ya hewa, siku moja baada ya video iliyovuja kumuonyesha akihoji makubaliano ya kisayansi kwamba kukomesha mafuta ni muhimu ili kupunguza ongezeko la joto duniani na kuzuia athari mbaya zaidi za mabadiliko ya hali ya hewa.

Al- Jaber amesema, "Nimeshangazwa sana na majaribio ya mara kwa mara ya kutaka kudhoofisha nafasi ya urais wa COP28 na majaribio ya kudhoofisha ujumbe ambao tunaendelea kurudia linapokuja suala la jinsi tunavyoheshimu sayansi,"

Video hiyo ilizua gumzo miongoni mwa mashirika yasiyo ya kiserikali, pamoja na wanaharakati wa mazingira wakihoji kwamba al-Jaber hana uwezo wa kuongoza mkutano wa kilele ambao unalenga katika kupunguza uzalishaji wa gesi chafu, ambayo husababisha mabadiliko ya hali ya hewa.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW