1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAfghanistan

Wajumbe wa UN wawasili Kabul kushinikiza haki za wanawake

18 Januari 2023

Wajumbe wa ngazi ya juu katika Umoja wa Mataifa akiwemo mwanamke aliye na cheo cha juu zaidi katika umoja huo Amina Mohammed, wamewasili Kabul Afghanistan kushinikiza haki za wanawake na wasichana.

UN Amina Mohammed Rede in New York
Picha: Xie E/Xinhua/picture alliance

Hatua hiyo ni jibu la matukio ya hivi ya karibuni ya watawala wa Taliban kukandamiza haki za wanawake, wasichana na waandamanaji.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed, ambaye ni waziri wa zamani nchini Nigeria na vilevile Muislamu, ameongozana na Sima Bahous, mkurugenzi mtendaji wa shirika la Haki na Masuala ya Wanawake katika Umoja wa Mataifa kwenye ziara hiyo.

Hayo yamesemwa na naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa Farman Haq aliyeongeza kuwa afisa mwengine katika ujumbe huo ni Khaled Khiari ambaye ni Katibu Mkuu Msaidizi katika Umoja wa Mataifa anayeshughulika na masuala ya siasa.

Haq hata hivyo amesema hawezi kutoa taarifa kamili kuhusu ratiba zao au mikutano haswa watakayofanya wakiwa Kabul, kwa sababu za kiusalama.

Mifululizo ya mashauriano kuhusu haki ya wanawake na wasichana Afghanistan

Wanawake wa Afghanistan wakiandamana kupinga marufuku ya serikali dhidi yao kupata elimu ya vyuo vikuu.Picha: Getty Images

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wamekuwa wakifanya misururu ya mashauriano ya ngazi ya juu kote eneo la Ghuba, barani Asia, na vilevile Ulaya, "kuhusu hali ya Afghanistan, kwa lengo la kukuza na kulinda haki za wanawake na wasichana, kuishi kwa amani, na maendeleo endelevu," Haq amesema.

Taliban yaombwa kubatilisha marufuku ya wanawake kufanya kazi

Kabla ya kuwasili mjini Kabul, maafisa kwenye ujumbe huo walikutana na viongozi wa nchi 57, ambao ni wanachama wa Ushirikiano wa Mataifa ya Kiislamu.

Kulingana na Haq, ujumbe huo pia ulikutana na maafisa wa Benki ya Maendeleo ya Kiislamu, makundi ya wanawake wa Afghanistan walioko Ankara Uturuki na Islamabad, kundi la mabalozi na wajumbe maalum wanaowakilisha mataifa yao nchini Afghanistan lakini ambao wako Doha, mji mkuu wa Qatar.

Uturuki, Saudi Arabia walaani msimamo wa Taliban

"Kote walikozuru, nchi na washirika mbalimbali walitambua juhudi muhimu za Umoja wa Mataifa, katika kutafuta suluhisho la kudumu na haja ya kuendelea kutoa misaada ya kuokoa maisha Afghanistan, na walitaka juhudi hizo kuimarishwa ili kuakisi haja ya dharura iliyopo," amesema Haq.

Mashirika matatu ya kimataifa yaanza tena kuwashirikisha wanawake kazini Afghanistan

Ziara yao imejiri mnamo wakati mashirika yasiyopungua matatu ya kimataifa yameanza tena kusambaza msaada wa kiutu nchini Afghanistan, baada ya kuhakikishiwa na utawala wa Taliban kuwa wanawake wanaweza kuendelea kufanya kazi katika sekta ya afya.

Ipi hatma ya wanawake nchini Afghanistan chini ya Taliban?

This browser does not support the audio element.

Mashirika ya CARE, Save the Children na International Rescue Committee yaliahirisha shughuli zao mwezi Desemba kupinga hatua ya serikali mjini Kabul kupiga marufuku wanawake kufanya kazi katika mashirika ya msaada.

Shirika la Save the Children limethibitisha katika taarifa yake kuwa limeanzisha tena shughuli zake kufuatia hakikisho la Taliban.

Taliban yawazuia wanawake kujiunga na elimu ya juu

Amri iliyotangazwa na Taliban mnamo Disemba 24 ya kuyapiga maruku mashirika ya kutoa misaada kuwaajiri kazi wanawake, inahujumu utoaji huduma muhimu ambazo zimekuwa zikiyanusuru maisha ya mamilioni ya Waafghanistan. Aidha tangazo hilo limekuwa tishio kwa huduma za kiutu kote katika taifa hilo.

Kutokana na marufuku hiyo, maelfu ya wanawake waliokuwa wakifanya kazi na mashirika hayo kwenye taifa hilo linalozongwa na vita, sasa wanakabiliwa na hatari ya kupoteza mapato yao wanayohitaji sana kukidhi mahitaji ya familia zao.

Masharti makali ya wanawake na wasichana kusafiri ndani na nje ya Afghanistan

Awali, utawala wa Taliban uliwapiga marufuku wasichana kupata mafunzo ya shule za sekondari na na vyuo vikuu. Isitoshe utawala huo uliweka masharti makali kwa wasichana wanaposafiri ndani au nje ya nchi.

Kundi la Taliban lilichukua madaraka Agosti 2021 baada ya wanajeshi wa Marekani na wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO kuondoka Afghanistan baada ya miaka 20.

Baadhi ya nchi za Kiislamu ikiwemo Uturuki na Saudi Arabia zimeitaka Taliban kubadili msimamo wake kuhusu elimu ya wanawake na wasichana.Picha: AFP

Mwaka mmoja wa Taliban madarakani

Kama tu ulivyofanya katika utawala wake kati ya mwaka 1996 hadi 2001, utawala wa Taliban umerudisha sheria za Kiislamu yaani Sharia, kuwaondoa wanawake kwenye ajira, utoaji misaada na kuwataka wakae majumbani.

Haq ameeleza kuwa maafisa wa mataifa mengine ambao ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulikutana nao, walisema ni muhimu kwa jumuia ya kimataifa kuungana na kuzungumza kwa sauti moja kuhusu masuala ya msingi yanayowahusu wasichana na wanawake wa Afghanistan ikiwemo haki yao ya kupata elimu, kuajiriwa na kuwa huru katika maeneo ya umma.

Haq amesema makundi hayo yamekubaliana kimsingi kuandaa mkutano wa kimataifa wa wanawake na wasichana katika Ulimwengu wa Kiislamu mwezi Machi.

(Vyanzo: APE, AFPE)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW