1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakaazi Gaza wasema Israel imeendelea kuishambulia Rafah

13 Juni 2024

Wakaazi wa Gaza wamesema helikopta za Israel zimeushambulia mji wa Rafah hii leo huku wanamgambo wa Hamas wakiripoti mapigano ya mitaani katika mji huo wa kusini baada ya Blinken kusema bado anayo imani ya mapatano

Israel
Israel imeendeleza mashambuliozi yake huko RafahPicha: Mostafa Alkharouf/Anadolu/picture alliance

Wakaazi wa Gaza wamesema helikopta za Israel zimeushambulia mji wa Rafah hii leo huku wanamgambo wa Hamas wakiripoti mapigano ya mitaani katika mji huo wa kusini baada ya Waziri wa Mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken kusema kuwa mapatano bado yanawezekana.

Soma zaidi. Vikosi vya Israel bado vyaushambulia mji wa Rafah

Vikosi vya ardhini vya Israel vimekuwa vikiendesha harakati zake mjini Rafah, karibu na mpaka wa Misri, tangu mwanzoni mwa mwezi wa Mei kuwafuata wapiganaji wa Hamas wa Palestina, licha ya wasiwasi mkubwa wa kimataifa kuhusu hatima ya watu waliokimbia makazi yao waliojaa katika mji huo.

Mapema leo wakizungumza na shirika la habari la AFP kusimulia yanayoendelea katika ukanda huo wakaazi wa Rafah wamesema Israel imeendeleza kufanya mashambulizi ya anga, nchi kavu na na baharini.

Shirika la habari la AFP limesema kuwa Israel imeendeleza mashambulizi na idadi ya vifo imeendeleza kuongezekaPicha: Mostafa Alkharouf/Anadolu/picture alliance

Itakumbukuwa kuwa mwezi Mei mwaka huu, Mahakama ya Kimataifa ya Haki ilitoa uamuzi wa lazima kwa Israel kusitisha mashambulizi yoyote huko Rafah na kwingineko ambayo yangeweza kuleta maafa makubwa kwa Wapalestina.

Soma zaidi. Makabiliano makali yaendelea Rafah licha ya wito wa Blinken

Lakini Israel ilijibu kwamba haijashiriki na haitojihusisha na operesheni kama hizo dhidi ya Wapalestina lakini juhudi za kufikia mwafaka zilikwama wakati Israel ilipoanzisha operesheni za ardhini huko Rafah.

Pamoja na mapigano yaanyoendelea huko Rafah, Shirika la habari la AFP limeripoti leo kutokea kwa mashambulizi mengine katika eneo la Pwani la Nuseirat ambako watu watatu wamekutwa wamefariki baada ya shambulizi la Israel.

Kwa mujibu wa wizara ya afya huko Gaza inayoongozwa na Hamas ni kwamba idadi ya vifo hadi sasa vilivyotokana na vita hivyo imefikia watu 37,232.

Soma zaidi. Ukatili dhidi ya watoto katika migogoro ulifikia viwango vya juu zaidi 2023

Kwingineko, Ving'ora vya uvamizi wa anga vimesikika katika miji ya kaskazini mwa Israeli hii leo ambapo maafisa wamesema kuwa takriban roketi 40 zilirushwa na kundi linaloungwa mkono na Iran la Hezbollah kutoka Lebanon kuelekea katika miji ya mpakani ya Israel.

Raia wa Rafah wakiwa wanayakimbia makazi yao kufuatia mashambulizi ya IsraelPicha: Eyad Baba/AFP/Getty Images

Chombo cha habari cha Serikali cha Kan kimerusha kanda za video zinazoonyesha muingiliano wa mawimbi wa roketi zilizopo juu ya hiyo ya  miji ya Israel iliyoko mpakani.

Mawaziri wa Iraq na Iran wakutana kuijadili Gaza

Hii leo pia Mawaziri wa Mambo ya kigeni wa Iran na Iraq wamekutana mjini Baghdad kujadili juu ya athari ya vita vinavyoendelea Gaza, Katika mkutano huo, Waziri wa Mambo ya kigeni wa Iraq Fuad Hussein amesema ni wakati wa kumalizika sasa kwa vita.

“Bila shaka, suala la Gaza, vita dhidi ya Gaza na kuwasaidia watu wa Palestina ulikuwa mhimili mkuu wa mazungumzo yetu. Pia, tulijadili suala la kusitisha mapigano na msimamo wa Iraq uko wazi. Tuko kwenye usitishaji mapigano, na sio tu usitishaji mapigano mara wa mara lakini tunahitaji usitishaji wa kudumu wa mapigano huko Gaza'' amesema Fuad.

Mapema leo Marekani imeonya kuwa mapigano kati ya mpakani kati ya Israel na Hezbollah yanaweza kuingia katika vita kamili na hivyo kutoa mwito wa mipango mipya ya usalama.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW