1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakaazi wa Busia waanza kuhama wakihofia El Nino

Michael Kwena22 Septemba 2023

Familia zinazoishi karibu na Ziwa Victoria katika jimbo la Busia nchini Kenya zimeanza kuhama makwao kutokana na hofu ya kutokea mafuriko katika eneo hilo.

Mafuriko ya Budalangi 2020
Raia wakitumia boti baada ya nyumba zao kusombwa na mafuriko katika kaunti ya Busia mwaka 2020Picha: Reuters/T. Mukoya

Eneo la Budalangi jimboni Busia, limekuwa likikumbwa na mafuriko kwa miaka mingi na hali bado imesalia vivyo hivyo licha ya serikali kujenga vizuizi kuepusha mkondo wa maji kuingia katika makaazi ya watu.

Mafuriko ya Kenya 2010: Mafuriko nchini Kenya

Wakati huu ambapo mvua za El Nino zinatarajiwa kunyesha,wakaazi wa eneo hili wameingiwa na hofu kubwa kutokana na athari za mafuriko ambazo zimekuwa hapa kwa muda mrefu.

Kufikia sasa, baadhi ya familia zimeondoka sehemu hizo na kuhamia kwingine wakati nyingine zikiendelea kujitayarisha kuhama ili kuepukana na athari za mafuriko. Mmoja wa wakaazi wa eneo hilo amesema kwamba "mvua za El Nino zikinyesha ,itabidi tuhame hapa. Hajui itakuwa vipi lakini tunaomba serikali isitusahau."

Picha ya angani inayoonyesha mafuriko katika kaunti ya Busia mwaka 2020Picha: Reuters/T. Mukoya

Waziri wa huduma kwa umma katika serikali ya jimbo la Busia Pamela Awuor ,ameeleza kwamba,serikali ya jimbo hilo imeweka mikakati ya kuwaokoa wakaazi kutokana na janga la mafuriko ambalo limekuwa likiripotiwa kila mara mvua zinaponyesha eneo hilo.

"Watu wamepewa mafundisho na pia tumejitayarisha kwa sababu idara ya majanga imewajumuisha watu watakaoshugulika kwa haraka endapo maji yatakuwa mengi zaidi."

Takriban watu elfu saba wako katika hatari ya kuathirika na mafuriko iwapo mvua zilizotabiriwa zitanyesha mwezi ujao.

Fukwe za Ziwa Victoria Siaya-Kenya zakumbwa na mafuriko

03:01

This browser does not support the video element.

Kulingana na meneja wa shirika la msalaba mwekundu kanda ya magharabi mwa kenya Hellen Cheruto,tahadhari inapaswa kuchukuliwa kabla ya mvua kuanza kunyesha.Bi Cheruto amesema kuwa,iwapo hilo halitafanyika kwa haraka,athari zake zitakuwa mbaya zaidi.

"Tumekuwa tukishirikiana na wanajamii wa hapa pamoja na machifu na manaibu wao katika kuhamasiha wakaazi kuhusu athari za mvua za El Nino.Tunataka hatua za dharura kuchukuliwa ili wananchi wsiathirike na mvua hizo."  

Wahanga wa mafuriko ya Budalngi pia wanaishinikiza serikali kuwanunulia vipande vya ardhi au kuwahamisha katika ardhi ya serikali kama suluhu la kudumu kwa mahangaiko ya mafuriko eneo hilo.Mafuriko yasababisha maafa magharibi mwa Kenya

Wakaazi wengi waliowahi kuathirika na mafuriko ya eneo hilo kwa wakati huu wanaishi kandokando ya shule ya msingi ya Bukoma huku wakiitaka serikali kupitia idara ya majanga kujenga kituo cha kuwasitiri wahanga wa mafuriko eneo hilo.

Serikali kwa ushirikiano na mashirika ya kijamii,inaendelea kupelea vyakula vya msaada eneo hilo kama mbinu ya kuwasaidia wakaazi wa budalng'i kujiandaa kwa ajili ya mvua za El Nino.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW