Wakaazi wa Kivu Kusini washerehekea Krismasi kwa hofu
25 Desemba 2018Nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo watu wanasherehekea pia sikukuu ya Krismasi. Ila wakaazi wa jimbo la kivu kusini, mashariki mwa nchi hiyo, wanasema furaha yao inakabiliwa na hofu kutokana na hekaheka za uchaguzi unaopangwa kufanyika mwishoni mwa juma nchini humo.
Wakaazi wa mji wa Bukavu ulioko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wanazidi kuhofia hali ya kisiasa ya sasa kuhusu uchaguzi ulioahirishwa mara kadhaa na unaopangiwa kufanyika siku tano zijazo. Watu wanajiuliza iwapo tume ya uchaguzi CENI iko tayari kwa uchaguzi huo wa Jumapili tarehe thelathini Desemba, pia wanatafakari je ikiwa hautafaanyika ni kipi kitatokea?.
Wagombea wa Bukavu wanasema wameshangazwa na tangazo lililotolewa na meya wa mji huo akiwataka walipe kiasi fulani cha pesa kwa kuwa wamebandika picha na mabango ya kampeni kwenye maeneo ya umma mjini Bukavu. Pesa hizo zitachangia kwa usafi wa mji, amesema meya wa Bukavu Meschac Bilubi.
Ameongeza kusema fedha hizo zinapaswa kulipwa hadi ifikapo Januari 15, mwaka ujao wa 2019 na kwamba atatangaza kwenye vyombo vya habari na kubandika kwenye ofisi yake majina ya wale waliolipa na wale ambao hawatafanya hivyo.
Hatua hii ya meya wa Bukavu imepuuzwa na wanaharakati wa asasi za kiraia pamoja na wagombea, wakisema kwamba hakuna sheria yoyote inayowalazimu walipe malipo hayo wakati wa kampeni.
Kiongozi wa tume ya uchaguzi Kivu Kusini, Gaudens Maheshe amehakikisha kwamba kampeni za uchaguzi zilihitimishwa rasmi Desemba 21 kutokana na kalenda ya uchaguzi, ila wagombea wanaruhusiwa kuweka mabango na picha kwenye maeneo ya umma hadi saa ishirini na nne kabla ya uchaguzi.
Licha ya hofu hiyo ya wapigakura na wagombea, wakaazi wa kivu kusini wanasherehekea sikukuu ya Krismasi kulingana na uwezo wao. Na kuna wengine ambao hawakusherehekea kutokana na sababu tofauti au za kiimani, kiafya, na kiuchumi.
Mwandishi: Mitima Delachance, DW, Bukavu
Mhariri: Zainab Aziz