1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi yaongezeka kwenye mipaka ya Urusi na Ukraine

20 Machi 2024

Maeneo ya mipakani kati ya Urusi na Ukraine bado yanakabiliwa na mashambulizi makali kutoka pande zote mbili ambayo yamesabisha uharibifu mkubwa. Wakati huo huo Rais wa Ukraine ameokea msaada mpya wa ulinzi

Belgorod
Majengo na vitu vingine ikiwemo magari yameharibiwa katika mji wa mpakani wa Urusi na Ukraine wa Belgorod kufuatia mashambulizi yanayoendelea baina ya pande mbiliPicha: Governor of Belgorod Region via REUTERS

       
Maeneo ya mipakani kati ya Urusi na Ukraine bado yanakabiliwa na mashambulizi makali kutoka pande zote mbili ambayo yamesabisha uharibifu mkubwa. Wakati huo huo Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy ametoa shukrani kwa ahadi mpya za msaada wa ulinzi zilizotolewa na washirika wake kwenye mkutano uliofanyika nchini Ujerumani. 

Soma zaidi: Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine kuelekea India wiki ijayo


Mashambulizi kati ya Urusi na Ukraine katika maeneo ya mipaka ya nchi hizo yameendelea kupamba moto, Maafisa wa Urusi wamesema mifumo ya ulinzi wa anga katika maeneo yao ya mipakanai imeharibiwa kwa makombora na ndege zisizo na rubani zilizorushwa na Ukraine katika miji Belgorod, Kursk na Voronezh inayopakana na Ukraine. 

Ndege hizo zisizo na rubani zilirushwa pia katika mji mwingine wa ndani kabisa wa Saratov.

Wanajeshi wa Urusi wakitandaza mchanga katika eneo lililoshambuliwa na Ukraine Picha: Belgorod Region Governor/dpa/picture alliance

Kama kujibu mashambulizi hayo, Urusi nayo imefanya mashambulizi kwenye mpaka wa kaskazini mashariki mwa Ukraine katika mkoa wa Sumy na kupelekea mamlaka za Ukraine kuagiza kuondoka kwa raia wake katika eneo hilo.

Soma zaidi: Urusi imehamisha watu elfu tisa kutoka mji wa Belgorod

Kupitia mtandao wa kijamii wa Telegram, Wizara ya Ulinzi ya Urusi imetoa taarifa kwamba vitengo vyao vya ulinzi imefanikiwa kuyanasa makombora mawili katika mji wa Kursk ambapo kwa mujibu wa taarifa hiyo ni kwamba mtengenezaji wa makombora hayo ni Marekani.

Mapema siku ya leo, Gavana wa mkoa wa Saratov, Roman Busargin, amesema kuwa kuwa ndege mbili zisizo na rubani za Ukraine zilinaswakaribu na jiji la Engels katika eneo la karibu na kambi ya jeshi la Urusi.

Watu watakiwa kuhama

Katika mji wa Belgorod, mamkala zimesema kuwa  watoto 1,200 kutoka maeneo yaliyo hatarini ya mpakani watasafirishwa mwishoni mwa wiki hii hadi katika mikoa mingine ya Urusi huku watu wengine 9,000 wakitakiwa kuhama pia katika maeneo hayo.

Afisa wa usalama akiwasaidia watu kuhama katika nyumba iliyoharibiwa na shambulio la Urusi katika mji wa Sumy, Ukraine.Picha: Andrii Marienko/AP/dpa/picture alliance

Wakati mapigano hayo yakiendelea, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy akiwa nchini Ujerumani kwenye kambi ya jeshi la anga la Marekani ya Ramstein amepokea msaaada mpya wa vifaa vya ulinzi kutoka kwa washirika wake, akikabidhi msaada huo Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin amesema ''Marekani inasimama na Ukraine kwa sababu ni jambo sahihi kufanya na kwa sababu Marekani inajali wakati uhuru ukiwa hatarini, na pia tunasimama na Ukraine kwa sababu ni muhimu kwa usalama wetu wenyewe''.

Kwa upande mwingine, Nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya na wabunge mapema hii leo wamefikia makubaliano ya kuzuia uagizaji wa nafaka za Ukraine bila ushuru, ambao hapo awali uliruhusiwa kufuatia uvamizi wa Urusi lakini baadae mjadala mkubwa ulizuka na kupelekea maandamano makali kutoka kwa wakulima katika umoja huo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW