1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakaazi wahamishwa majengo ya ghorofa refu London

24 Juni 2017

Wakaazi wa nyumba 650 wamehamishwa kutokana na hofu za moto kufuatia kuteketea kwa jengo la ghorofa la Grenfell kulikosababisha maafa lakini watu 83 wamegoma kuzihama nyumba zao.

England London Hochhäuser Evakuierung
Picha: Picture alliance/empics/S. Rousseau

Majumba manne ya ghorofa kati ya matano ya Chalcoats Estate huko Camden  kaskazini mwa London yametajwa kuwa hayako salama baada ya kugundulika kutumika vifaa vya kuweka sura ya nje ya jengo sawa na vile viliotumika kwa jengo la Grenfell ambapo vinalaumiwa kwa kiasi kikubwa kusababisha kuenea kwa haraka kwa moto mkubwa wiki iliopita unaodhaniwa kuuwa takriban watu 79.

Msemaji wa kikosi cha kuzima moto cha London amesema "Kufuatia ziara na ukaguzi wa kina wa pamoja kikosi hicho kimeshauri kwamba kuna masuala kadhaa ya usalama kuhusu moto katika majengo hayo na kupendekeza wakaazi hawapaswi kuendelea kubakia."

Uamuzi huo wa kushtuwa unafuatia ukaguzi wa dharura wa sehemu za nje za majengo ya ghorofa ambazo zimetengenezwa na kondarasi huyo huyo aliefanyia ukarabati jengo la ghorofa la Grenfell.Wakaazi wa majengo yote matano ya ghorofa ya Chalcots awali walihamishwa lakini mojawapo ya majengo hayo matano lile la Blashford lilionekana kuwa liko salama na wakaazi waliruhusiwa kurudi katika nyumba zao.

Ilikuwa ni vurugu

Wakaazi wakihamishwa kutoka jengo la ghoroga refu la Teplow.Picha: Reuters/H. Mckay

Wakaazi wengine walikabiliwa na vurugu ambapo makaazi ya muda yalitolewa katika kituo kimoja cha mapumziko katika eneo hilo na mahoteli lakini baadhi yao waligoma kuhama.

Kiongozi wa baraza la manispaa la Camden Georgia Gould amekiambia kituo cha BBC News kwamba wakaazi 83 wamegoma kuondoka na kwamba suala hilo litakuwa la kikosi cha kuzima moto kulishughulika.

Mkaazi Renee Williams mwenye umri wa miaka 90 amesema yeye na majirani zake hawakupewa onyo lololote kabla.Ameliambia shirika la habari la AP kwamba "Hakuna mtu aliekwenda kuwaambia nini kinachotendeka, ameona kwenye TV kwa hiyo amefunga mkoba wa kuupitisha usiku."

Ameendelea kusema lakini sasa wanawaambia kwamba watatoka kwenye nyumba zao kwa wiki mbili hadi nne zijazo.Anaona hakuna maandalizi na ni vurugu.

Wakati wa hofu

Majengo ya ghorofa refu ya Chalcots huko Camden.Picha: Reuters/H. Mckay

Kiongozi wa baraza hilo la manispaa Gould amekiri kuwa ni "wakati wa hofu" lakini ameahidi "kuhakikisha kwamba wanabaki salama." na kwamba suala la gharama watalishughulikia baadae.

Baraza hilo limekuwa likitowa taarifa za kukodi hoteli na mapema mjini kote London na kazi hiyo inategemewa kuchukuwa wiki moja.Michelle Urquhart ambaye amekuwa akiishi kwenye jengo la ghorofa la Bray Tower la Chalcoats Estate amesema "hali inatisha" na kwamba hajuwi wanakwenda wapi.

Hapo Ijumaa polisi imesema mashtaka ya mauaji bila ya kukusudiwa yanaweza kufunguliwa kutokana na moto huo wa jengo la Grenfell Tower baada ya kugundulika moto huo umeanza na hiltilafu ya friji na kwamba vifaa vilivyotumika kufunika sura ya nje ya jengo vilishindwa kutimiza vigezo vya usalama.

Vifaa hivyo viliwekwa kwenye jengo hilo la ghorofa 24 linalomilikiwa na baraza la manispaa ambalo limejengwa hapo mwaka 1974 kama sehemu ya ukarabati ambao umemalizika hapo mwaka jana.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri : Lilian Mtono

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW